Tanzania, Kenya kufanya maadhimisho kutunza Mto Mara

Muktasari:
Nchi za Tanzania na Kenya zinatarajiwa kufanya maadhimisho ya siku ya Mara kwa muda wa siku nne kuanzia kesho lengo kuu likiwa ni kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira ya bonde la Mto Mara.
Musoma. Nchi za Tanzania na Kenya zinatarajiwa kufanya maadhimisho siku ya Mara kwa muda wa siku nne kuanzia leo lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira ya bonde la Mto Mara.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma Septemba 11, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika wilaya ya Serengeti mkoani humo yakishirikisha taasisi na mashirika ya umma na binafsi kutoka katika nchi hizo.
"Maadhimisho haya ni muhimu sana kwa uendelevu ya bonde la Mto Mara na yanalenga kutoa msukumo mkubwa kwa kuhifadhi bonde la Mto Mara ambalo lina mchango mkubwa katika tukio zima la kuhama kwa wanyama katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuifanya hifadhi hiyo kuwa moja ya maajabu saba ya dunia na hifadhi bora barani Afrika,"amesema
Amesema katika maadhimisho hayo shughuli kadhaa zitafanyika ikiwemo upandaji wa miti zaidi ya 50,000 katika hifadhi ya bonde hilo na usimikaji wa vingingi kwenye mpaka wa mto huo na vijiji vya Merenga na Nyansurura wilayani Serengeti.
"Pia kutakuwa na kongamano la kisayansi litakalojadili na kupanga namna bora ya kuhifadhi mto Mara ili uweze kuwa endelevu kwa ustawi wa nchi zetu hizi,"ameongeza Mtanda
Mtanda amesema mbali na sekta ya utalii, bonde hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo na ufugaji kutokana na mto Mara kuwa chanzo kikuu cha maji ndani ya Ziwa Victoria.
Wakizungumzia maadhimisho hayo,baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamesema umefika muda maadhimisho hayo yaende sambamba na utekelezaji wa maazimio yanayofanywa kila mwaka wakati wa maadhimisho.
“Haya maadhimisho yanafanyika kwa kupokezana kwa nchi zetu na huwa kuna makubaliano lakini sina uhakika kama yanatekelezwa kwasabu tumeshuhudia uharibifu wa mazingira ya bonde hili kwa pande zote hali ambayo inatishia uhai wa bonde hili muhimu kwa nchi zetu,"amesema Anna Masinde
Fazel Janja amesema kila mwaka miongoni mwa shughuli zinazifanyika ni pamoja na upandaji wa miti lakini usimamizi wa ukuaji wa miti hiyo hakuna nakusababisha miti mingi kutokukua.
“Ukienda hata hapo pembezoni mwa mto utakutana na miti ya asili ambayo pia imeanza kutoweka lakini miti inayopandwa kwenye maadhimisho hakuna usimamizi hivyo inakufa huku gharama ikiwa imetumika kubwa wakati wa kuipanda,"amesema Janja