Serikali yajenga makinga moto bonde la maji Mzakwe

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akizungumza na wadau wa bonde la maji la Mzakwe kuhusi changamoto ya moto ya mara kwa mara.
Muktasari:
- Baada ya matukio ya moto matatu Agosti mwaka huu, Serikali imeanza kuchukua hatua ya kukabiliana na moto huo kwa kujenga makinga moto.
Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameagiza makinga moto yanayowekwa katika Bonde la Mzakwe jijini Dodoma yawekwe vizuri na siyo ovypo ili kurahisisha watu kupita wanapotembelea.
Katika kipindi cha mwezi mmoja, moto umezuka kwa mara tatu katika bonde hilo na kuunguza baadhi ya sehemu pamoja na nguzo za umeme tatu.
Mzakwe ni chanzo kikuu cha maji katika Jiji la Dodoma ambako asilimia 91 ya mahitaji ya maji yanayozalishwa kwa siku yanatoka kwenye chanzo hicho.
Mahitaji ya maji kwa siku kwa Jiji la Dodoma ni lita milioni 130 kwa siku wakati uzalishaji wa vyanzo vyote ukiwa ni kati ya asilimia 53 hadi 54.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 4, 2023, Shekimweri amesema katika kipindi cha Agosti mwaka huu kumezuka moto mara tatu na kwamba kazi inayofanyika ni kuhakikisha wanakinga bonde hilo.
Amesema katika kikao wachokaa pamoja na wadau wengine waliamua kuweka barabara (makinga moto) ili kukinga moto katika bonde hilo ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwenye jiji la Dodoma.
Amesema wadau wamechangia ammbapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limechangia Sh8 bilioni huku Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Duwasa) wakichangia Sh10 bilioni.
“Kazi inayofanyika hapa ni kutengeneza barabara ya kukinga moto (makinga moto), kazi itakayofanyika itakwenda kulinda hifadhi ya Bonde lenyewe, wataalam wameweka map (ramani) kila hatua ngapi kutakuwa barabara,”amesema
Amesema kwa kujengwa kwa makinga moto hayo kutasaidia katika kuwezesha watu kutembelea maeneo hayo, wanaofanya utalii na wanaotoa huduma ya miti kuweza kupita kwenye maeneo hayo.
Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Wami Ruvu (WRBWB), Elibariki Mmasi amesema wameaza kuhuisha ile mipaka kwa ajili ya kuona maeneo gani wananchi wanatakiwa kuishia wakati wanapofanya shughuli za kibinadamu.
“Pia kutoa elimu kwa watu wanaozunguka kwenye bonde hili ili kuwahakikisha tunashirikiana katika kutunza bonde hili,” amesema.
Ofisa Mazingira wa Duwasa, Maria Holela amesema kuwa wanashirikiana na wadau wengine kuhakikisha bonde hilo ambalo linategemewa kuzalisha maji kwa asilimia 91 linalindwa.
Meneja wa Tanesco Dodoma, Donasiano Shamba amesema hawajaweza kubadilisha nguzo zote zilizopo katika bonde hilo kutoka nguzo za miti kwenda kwenye zege.
“Kwa hiyo zimepata athari ya kuungua kwa nguzo hizo kwa hiyo sisi kama Tanesco wanajukumu la kuhakikisha kuwa nguzo hizo haziungui. Hivyo kwa kushirikiana na Duwasa na Bonde hili tumeunganisha nguvu kuhakikisha hii miundombinu yote iliyoko tunaitunza,”amesema.