Tanroads kutumia mfumo wa PPP ujenzi miradi ya barabara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi akifunga mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Tanroads, mkutano uliofanyika kwa siku mbili mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) unatarajia kuanza kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kupitia mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP).
Musoma. Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) unatarajia kuanza kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kupitia mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP).
Kabla ya kuanza kutekeleza miradi kupitia mfumo huo wataalamu kutoka taasisi hiyo watalazimika kujifunza kutoka ndani na nje ya nchi juu ya uendeshaji wa miradi ya mfumo huo ili kuleta tija mara watakapoanza kutekeleza miradi hiyo.
Hayo yalisemwa Juni 11, 2022 mjini Musoma na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Rogatus Mativila wakati wa kuhitimisha mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Tanroads uliofanyika kwa siku mbili.
Alisema kuwa uamuzi wa kutekeleza miradi ya Tanroads kupitia mfuno wa ushirikiano na sekta binafsi ni moja ya maazimio ya mkutano huo ambao unalenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi yake kwa maslahi ya watanzania kwa ujumla.
Mativila alisema kuwa mfumo huo utasaidia kuongezaka kwa idadi ya miradi ya barabara kuliko ilivyo sasa mabapo miradi yote hutegemea bajeti ya Serikali hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inapelekea baadhi ya maeneo kuchelewa kupata barabara za uhakika.
"Tumeazimia kuanza kutekeleza miradi kwa mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi na kabla ya kuanza wataalamu wetu wanakwenda kujifunza ndani na nje ya nchi juu ya utekekelezaji wa miradi ya aina hiyo sambamba na kujifunza teknolojia mpya za utekelezaji wa miradi ya barabara na miundombinu mbalimbali " amesema
Akifunga mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alisema kuwa azimio hilo la kutekeleza miradi kwa mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi umekuja kwa kuchelewa kwani Tanzania imekuwa ikihitaji miradi ya aina hiyo kwa muda mrefu.
Ametolea mfano wa miji yenye msongamano mikubwa ya watu kama Dar es salaama ambapo amesema kuwa suala la foleni limekuwa tatizo sugu ambalo linahitaji ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi kulitatuata.
"Mfano mnaingia ubia na mwekezaji ambaye ataamua kujenga barabara za juu ambazo wapitaji watalazimika kulipa gharama kidogo na wale wasiotaka kulipa watapita kwenye barabara za serikali hakika hii itakuwa suluhisho kwani na wahakikishia watu watakuwa tayari kulipia kupita barabara ya juu kwenda airport na kwingineko na kuepuka kuchelewa" amesema
Amesema kuwa hali hiyo pia itasaidia kupunguza foleni kwenye barabra za umma hivyo kuitaka Tanroads kuanza mchakato huo mara moja kwa maelezo kuwa watanzania wanausubiri kwa hamu.
Hapi amesema kuwa ushirikiano baina ya Tanroads na sekta binafsi pia utapelekea serikali kuelekeza fedha nyingi zaidi kwenye miradi mingine ya huduma za kijamii badala ya ujenzi wa barabara.