Tani 14 za shaba zawatia matatani watuhumiwa 15

Muktasari:
- Wadaiwa kuhujumu miradi ya SGR, Tanesco, watuhumiwa 13 wafikishwa makahakamani.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli limekamata kilo 14,264.1 (zaidi ya tani 14) za nyaya za shaba zilizokatwa kwenye njia ya reli ya kisasa (SGR) kwenye maeneo mbalimbali na kuuzwa kama chuma chakavu.
Pia, linawashikilia watuhumiwa zaidi ya 15, wakiwemo raia wa China na Kenya wanaodaiwa kuhusika na uharibifu huo.
Kati ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo, wamo mafundi walioshiriki ujenzi wa miundombinu ya SGR, fundi umeme na wafanyabishara wanaojishughulisha na uuzaji na ununuzi wa chuma chakavu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Desemba 17, 2024, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Gallus Hyera amesema waliwakamata watuhumiwa na kiasi hicho cha nyaya za shaba kupitia misako na operesheni walizofanya maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Hyera amesema Novemba 28, 2024 maeneo ya Mdaula mkoani Pwani, walikamatwa watuhumiwa wakiwa na nyaya za shaba kilo saba.
"Mmoja kati ya watuhumiwa ni fundi umeme, mwajiriwa wa kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza ujenzi wa miundombinu ya SGR. Huyu ndiye anayekata nyaya maeneo mbalimbali. Jumla ya watuhumiwa watatu wamekamatwa," amesema.

Amesema Novemba 30, 2024 katika eneo la Visiga mkoani Pwani kwenye kampuni ya The African Light Investment Ltd inayomilikiwa na raia wa kigeni (China na Kenya) zilikamatwa nyaya za shaba zenye uzito wa kilo 882.5.
"Desemba 2, 2024 huko maeneo ya Visiga, Pwani ulifanyika upekuzi kwenye nyumba inayomilikiwa na The African Light Investment Ltd (Raia wa China na Kenya), katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa na nyaya mbalimbali za shaba zenye kilo 3687.9.
"Nyaya hizi zimetambuliwa kuwa zimetokana na uharibifu kwenye miradi ya SGR na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania). Jumla wamekutwa na nyaya kilo 4,570.4 na raw copper bars (vipande vya shaba) 44 zenye uzito wa kilo 971.5," amesema.
Kupitia taarifa za kiintelijensia, amesema eneo la Kisemvule zilikamatwa nyaya za shaba kilo 608.6 za Tanesco, kilo 37.6 (za SGR) na vipande vya shaba zilizozalishwa kwa kuyeyushwa nyaya za shaba kilo 5,517.4 kwenye kiwanda cha chuma chakavu cha Metal Chem International Co. Ltd. Watuhumiwa wawili wamekamatwa.
Desemba 5, 2024 eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti amesema walikamata kilo 65.5 za nyaya hizo kutoka kwa wanunuzi wa chuma chakavu. Pia walikamatwa watuhumiwa wakiwa na waya wa shaba kilo 6.5 wakiwa katika harakati ya kuuza.

Amesema Desemba 13, 2024 mkoani Pwani walikamatwa wamiliki wa kiwanda cha Balochistan Group of Industrial (BGI) kutokana na taarifa za kiintelijensia wakiwa na waya wa shamba kilo 61, vipande vya shaba 19 vyenye uzito wa kilo 141 kutoka kwenye gari lenye namba T 141 DQG aina ya Fuso.
Amesema upekuzi ulipofanyika kiwandani zilikamatwa nyaya za shaba kilo 67 na vipande 426 vyenye uzito wa kilo 7,728 ambavyo ni zao la waya wa shaba.
Amesema shaba hiyo imetoka kwenye miundombinu ya miradi ya SGR na Tanesco na kwamba watuhumiwa wawili wamekamatwa.
Amesema jumla ya watuhumiwa 13 wamefikishwa mahakamani, kati yao wanane wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha kwa makosa ya uhujumu uchumi na watano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa makosa sawa na hayo.
"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote anayejipanga kufanya uhalifu huu wa kukata nyaya za shaba kwenye miradi ya SGR na Tanesco, watasakwa kwa nguvu zote, kukamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria," amesema.
Meneja Ishara na Umeme kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Felix Mutashobya amesema uharibifu wa miundombinu unaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo hitilafu katika mfumo wa mawasiliano na umeme katika SGR.
"Matokeo yake inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa," amesema.