Tamu, chungu tozo miamala

Muktasari:
- Licha ya asilimia 90 ya Watanzania kukubali kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi, asilimia 75 wanasema viwango vya kodi hizo ni vikubwa.
Dar es Salaam. Licha ya asilimia 90 ya Watanzania kukubali kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi, asilimia 75 wanasema viwango vya kodi hizo ni vikubwa.
Hayo yameelezwa katika ripoti ya utafiti wa Sauti za Wananchi wenye jina: ‘Maoni ya wananchi kuhusu uchumi wa Taifa na tozo za miamala ya fedha kupitia simu za mkononi’, iliyotolewa na taasisi ya Twaweza jana jijini Dar es Salaam.
Utafiti huo umekuja wakati kukiwa na mjadala wa ongezeko la tozo, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, ambapo pamoja na mengine imepitisha tozo ya miamala ya benki.
Mwananchi lilizungumza na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa, aliyekiri kuiona ripoti ya utafiti huo na kusema Serikali inaifanyia kazi na itatoa tamko leo.
“Mimi nimeziona leo wamezindua, hizo ni za kwao na sasa hivi sisi tunazifanyia kazi ili kutoa taarifa rasmi kama Serikali,” alisema.
Hata hivyo, alisema takwimu walizotoa siyo rasmi.
Matokeo ya utafiti
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 88 ya wananchi walisema wangependa kulipa kodi bila shuruti na wengine (asilimia 67) wanasema si vema kuficha kipato ili kulipa kodi chini ya kipato.
“Hata hivyo, wananchi wanne kati ya 10 (asilimia 42) wanasema wangekwepa kulipa kodi kama wangeweza kufanya hivyo,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Utafiti huo pia umeonyesha asilimia 39 ya wananchi wanakwepa kulipa kodi kwa kuwa wanaona viwango ni vikubwa mno.
“Sababu nyingine zilizotolewa ni pamoja na dhana kwamba hawalipwi mishahara mizuri (asilimia 20), kwamba kodi haitumiki vizuri (asilimia 15) au kwamba watu hawajui namna ya kuwasilisha kodi zao (asilimia 11),” ilibainisha ripoti hiyo.
Sababu nyingine iliyotajwa kukwaza watu kukwepa kodi ni kupanda kwa gharama za maisha, huku ripoti hiyo ikionyesha kuwa suala hilo ni miongoni mwa matatizo makubwa matatu yanayolalamikiwa zaidi na wananchi.
“Karibu nusu ya wananchi wote waliohojiwa (asilimia 48) wanataja kupanda gharama za maisha kuwa miongoni mwa matatizo matatu makubwa yanayozikabili kaya zao kuliko matatizo mengine. Matatizo mengine ni ukosefu wa ajira na fursa nyingine za kipato (asilimia 29) na tatizo la njaa na uhaba wa chakula (asilimia 26),” ilisema taarifa hiyo.
Kupanda gharama za maisha
Katika suala hilo, ripoti hiyo ilisema kupanda kwa gharama za maisha ni miongoni mwa mambo matatu ambayo asilimia 46 ya wananchi waliohojiwa wamesema wangemwambia Rais ayashughulikie.
Mengine ni huduma za afya (asilimia 42) na huduma za jamii zikiwemo usafiri (asilimia 35), elimu (asilimia 28) na ukosefu wa ajira (asilimia 27).
Hata hivyo, kutokana na malalamiko ya wananchi ya kupanda kwa gharama za maisha kulikotokana na ongezeko la bei ya mafuta, Serikali iliahidi kutoa ruzuku ya Sh100 bilioni ili kupunguza makali ya bei ya mafuta nchini.
Akizungumza bungeni Mei 10, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema ruzuku hiyo iliyoanza kutumika Julai Mosi ililenga kupunguza matumizi ya Serikali kwa kipindi kilichosalia cha mwaka wa fedha 2021/22.
Wananchi wapunguza kutuma, kupokea fedha kwa simu
Utafiti huo pia umebainisha kupungua kwa utumaji wa fedha kwa njia ya simu tangu Julai 2021 (asilimia 44) kuliko wale wanaoripoti kuongeza kutuma fedha kwa njia hiyo (asilimia 15).
“Idadi ya wanaopokea fedha kwa njia ya simu imepungua tangu Julai 2021 (asilimia 46) kuliko wale wanaoripoti kupokea zaidi (asilimia 14).
“Wakazi wengi wa Dar es Salaam wanaripoti kupunguza kutuma/kutumia pesa kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu (asilimia 71),” ilisema ripoti.
Pia utafiti huo umetoa mfano wa taarifa ya Vodacom Tanzania PLC ikionyesha kupungua kwa asilimia 4.4 ya idadi ya watumiaji wa huduma ya M-Pesa kati ya Juni 2021 na Juni 2022 na kushuka kwa jumla kwa asilimia 9.2 ya wastani wa mapato kwa kila mtumiaji (ARPU).
“Jambo hili limesababisha kampuni kulipa ushuru pungufu wa mapato kwa asilimia 74 kati ya Aprili na Juni 2022 kuliko kipindi kama hicho mwaka uliopita. Wanazitaja athari za ushuru kwenye miamala ya utumaji na utoaji wa pesa kwenye simu za mkononi kama sababu kuu ya kushuka huku,” imeeleza.
Tozo ya miamala ya simu ya kutuma na kupokea kwa njia ya kielektroniki ilianzishwa Julai 2021, lakini kutokana na malalamiko ya wananchi ilipunguzwa kwa asilimia 30 ilipofika Septemba 2021 na ilipunguzwa tena Julai 2022 na hivyo kufanya punguzo kuwa asilimia 60.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha kuwa wananchi hawakubaliani (asilimia 23) au hawakubaliani kabisa (asilimia 34) na tozo tangu ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza.
Maoni ya wadau
Akitoa maoni kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema licha ya utafiti kuonyesha kuwa gharama za maisha zimepanda, Serikali imefanya juhudi kubwa kupunguza makali.
“Wakati mwingine tunailaumu tu Serikali kwamba wapunguze tozo. Kwa mfano, ukiangalia bei ya mafuta, Serikali ilitoa ruzuku bei haikupanda sana,” alisema.
Alisema ili wananchi wafurahie kulipa kodi, Serikali inapaswa kuweka uwazi katika mipango ya bajeti kwa wananchi na kuwaonyesha matokeo ya kodi wanazotoa.
Suala la uwazi katika ulipaji wa kodi liliungwa mkono na Katibu Mwenezi wa chama cha NCCR -Mageuzi, Edward Simbeye aliyesema: “Wananchi wanataka waambiwe fedha za tozo zinakwenda wapi.”
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Agosti 20, 2022 Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema fedha za tozo zitakuwa sehemu ya bajeti ya Serikali na zitatumika katika shughuli zilizoidhinishwa kwenye wizara, mikoa, halmashauri, kata, mitaa na vijiji katika sekta mbalimbali.
“Miongoni mwa maeneo zitakapotumika ni pamoja na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji na barabara na utoaji wa ruzuku za elimu kwa shule za msingi na sekondari,” alisema.
Juma Amir, mkazi wa Tabata jijini hapa, akichangia mjadala huo jana kwa simu alisema: “Kwa kuwa tozo hizi zinalenga kutuletea maendeleo, itabidi tuzilipe. Tutaumia kwa kipindi fulani, lakini hatimaye tutapata maendeleo
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo alitahadharisha wingi wa tozo, akisema utasababisha wananchi kukata tamaa ya kulipa kodi.
“Serikali haijui kuwa unapoongeza tozo unapunguza wigo wa kodi siku za usoni,” alisema.
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa biashara, Profesa Francis Matambalya aliyezungumza na Mwananchi kwa simu, alisema hatua ya wananchi kuelemewa na kodi katika nchi zinazoendelea, inatokana na uwezo duni wa nchi husika kuvitumia vyanzo vyote vya mapato.
Alifafanua kwa nchi kama Tanzania inatumia vyanzo vya msingi, lakini si mnyororo wote wa thamani wa vyanzo husika katika kupata mapato.
Mathalani, katika sekta ya kilimo na madini, alisema Serikali inatekeleza shughuli hiyo na kukiuza kinachopatikana kama malighafi. “Tunapata mazao lakini hatuyauzi kama bidhaa, tunauza malighafi, maana yake kodi tunayopata hapa ni ndogo hailingani na thamani halisi ya kinachozalishwa,” alisema.
Profesa Matambalya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), alibainisha eneo lingine ambalo nchi zinazoendelea zinapoteza mapato ni uwekezaji kutoka nje.
Kuhusu kodi na tozo zinazokusanywa, alipendekeza kuongezwa uwazi ili wananchi angalau waone na kujua matokeo ya kile wanachokilipa.
Kwa upande wake mtaalamu wa uchumi, Dk Josephat Werema aliishauri Serikali kutoa msamaha wa kodi na tozo hizo kwa wenye kipato cha chini na wazee.
Alisema kilio cha wananchi kuhusu tozo na kodi ni kielelezo kwamba uwezo wao wa kuhimili umefikia mwisho.
“Ukiona watu wanalalamika ujue uwezo wao wa kuhimili hizo kodi au tozo ni mdogo, wanapaswa kupunguziwa mzigo.
Kuhusu uwazi katika matumizi ya kodi, alisema si kila mwananchi anastahili kupelekewa taarifa kuhusu tozo ilivyotumika, badala yake Bunge ndilo lenye haki hiyo.