Tamu, chungu kazi ya kufukua makaburi Dar es Salaam

Muktasari:
Desemba 27 hadi 29, Jiji la Dar es Salaam lilihamisha makaburi 238 yaliyopo Kata ya Vingunguti Mtaa wa Butiama kwenda eneo la Mwanagati.
Dar es Salaam. Waswahili wanasema ‘kazi ni kazi bora mkono uende kinywani’ hakika ndiyo dhana inayotumiwa na watu wanaofukua makaburi, kuchimba na kuyahamisha.
Desemba 27 hadi 29, Jiji la Dar es Salaam lilihamisha makaburi 238 yaliyopo Kata ya Vingunguti Mtaa wa Butiama kwenda eneo la Mwanagati.
Hatua hiyo ilikuja baada ya baadhi ya makuburi yaliyopo eneo hilo kusombwa na maji kulikosababishwa na kumomonyoka kwa kingo za mto Msimbazi uliopo pembezoni mwa makaburi hayo.
Mwananchi, iliyofika eneo hilo siku chache kabla ya kuanza kazi ya kufukuliwa kwa makaburi hayo, ilishuhudia baadhi ya majeneza yakiwa yanaonekana kwenye kingo za mto huo.
Ilipozungumza na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Butiama, Nimzihirwa Mjema, alisema tatizo hilo limekuwepo kwa muda wa miaka mitatu sasa na tayari walishahamisha baadhi, lakini hali kila mvua zinaponyesha inakuwa mbaya na hivyo Serikali iliamua kuyahamisha yaliyopo mita kumi kutoka ulipo mto, huku Ofisa Afya wa Jiji la Dar es Salaam, Reginald Mlay akisema shughuli nzima imetumia zaidi ya Sh30 milioni.
Hata hivyo, wakati shughuli hiyo ikiendelea makaburi mengine zaidi ya 100 yaligundulika na hivyo imesitisha kwa muda kazi hiyo ambayo itaendelea hivi karibuni baada ya fedha za kuifanya kupatikana.
Katika shughuli hiyo kulikuwepo watu walioifanya kazi hiyo ya kufukua na kuzika mabaki ya miili wapatao 40.
Watu hao walikuwa wamevalia nguo aina ya overoll za rangi ya bluu iliyopauka, mabuti na gloves ngumu na nyepesi.
Katika kuifanya kazi hiyo walikuwa wanatumia makoleo, majembe, sururu na wakati mwingine nyundo, kazi ambayo ukiangalia ilionekana kuwa ngumu, kwa kuwa wengine walionekana kuingia hadi na chupa za maji ndani ya kaburi ilimradi kutuliza kiu, huku wakiendelea na kazi.
Wakati maswali yakiwa mengi hivyo, Mwananchi lilifanya mahojiano na baadhi ya wafukuaji makaburi hao na kueleza mengi kuhusiana na kazi yao hiyo, changamoto wanaziokutana nazo na namna jamii inavyowachukulia.
Baadhi ya wafukuaji hao walisema kazi hiyo waliianza kama wafanyakazi wa mochwari katika hospitali moja kubwa jijini Dar es Salaam, kazi waliyofanya kwa miaka saba.
“Kazi ya mochwari niliifanya kwa miaka saba na hii ni baada ya kutokea nafasi ya kutakiwa wahudumu katika hospitali hiyo baada ya waliokuwepo kuondolewa kutokana na kashfa ya kuzika vichanga katika kaburi moja.
“Wakati huo nilikuwa nafanya kazi mapokezi, hivyo nilivyoomba nafasi hiyo ilikuwa rahisi kupokelewa, ukizingatia tayari nilikuwa nina uzoefu wa kupokea watu wa aina mbalimbali,” anasema Abdul Khalifa.
Hata hivyo, anasema baada ya mkataba wake kwisha ndipo akapata tena nafasi ya kuajiriwa Halmashauri kwa mkataba, ambapo kazi yao ni kuzika watu wasiokuwa na ndugu na kama hivyo ikitokea makaburi yanatakiwa kuhamishwa.
Changamoto
Hakuna kazi isiyokuwa na changamoto, hivyo ndivyo ilivyo kwa wafukua makaburi hawa, ambapo James Geofrey anasema huwa wanakutana na mambo mbalimbali wakati wa kufukua makaburi, yakiwemo yale ya kishirikina.
“Wakati wa kufukua makaburi tunakutana na mengi, zikiwemo hirizi, vichwa vya mbuzi, nguo, basi si unajua tena mambo haya ya kishirikina kwenye jamii hayakosekani,” alisema Geofrey.
Changamoto nyingine anasema wakati wa kufukua kaburi unaweza ukafika hadi chini na usikute mwili kwa kuwa katika kufanya kazi hii huwa wakifuatisha msalaba ulipowekwa kwa wale waliozikwa kwa dini ya Kikristo na kwa dini ya Kiislam hufuatisha kibao.
Lakini wakati mwingine vyote hivyo unakuta vinatofautiana na mwili ulipositiriwa, na hivyo kulazimika kuchimba pembeni na pembeni hadi kukuta mwili.
Rashid Mwangaza anasema yeye hakuna jambo linalomuudhi kama wakati wa kufukua watu wanakuwa wakiwaangalia wanavyofanya kazi hiyo na kutaka kama ni ndugu basi wawaamini, kwani kuna baadhi wamekuwa wakiwapa na maelekezo kabisa kwamba utampasua fuvu, chimba hivi bila kujua ile kazi wao wana uzoefu nayo.
Matumizi ya vilevi
Musa Njumani alisema kuwa dhana ya kuwa ni lazima watumie vilevi, sigara au kuvuta bangi ndipo wafanye kazi hiyo haina ukweli, kwakuwa hiyo ni kazi kama zilivyo nyingine.
Jamii inawachukuliaje
Bariki Fanuel anasema bado jamii haijakubali kazi hiyo ni kama kazi nyingine na ndio maana baadhi walipokuwa wakifanya kazi ya kufukua wakiona kamera za waandishi wa habari walijificha.
“Ilifika mahali watu wanaogopa kamera za waandishi, wanajificha ndani ya makaburi hadi waandishi waondoke.