Prime
Sababu wanawake wa Kiluguru kuwa wababe, jasiri

Muktasari:
Nguvu ya pesa inayotokana na kilimo cha mbogamboga, jiografia, hali ya hewa na elimu vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya wanawake wa Kiluguru kutoka kata ya Mgeta, Wilaya ya Mvomero kuwa wababe, wakakamavu na wenye misimamo.
Morogoro. Waluguru ni kabila kuu katika Mkoa wa Morogoro. Wanawake wa Kiluguru wametofautiana kulingana na mazingira ya maeneo wanakotoka, ambapo wanaotoka Mgeta wilayani Mvomero wanaonekana kuwa wababe, wakakamavu, wenye nguvu na misimamo kuliko wanawake wa Kiluguru kutoka maeneo mengine.
Zipo sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha wanawake wa Mgeta kuwa sifa hizo, mojawapo ikiwa ni kuwa na nguvu ya kiuchumi inayotokana na kilimo cha mbogamboga na matunda wanachofanya wanawake hao.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wanawake wa Kiluguru kutoka Mgeta Madukani, Catherine Casper anasema fedha anazopata kutokana na kilimo cha mbogamboga zinamfanya aishi bila kumtegemea mume, ndugu wala watoto wake, hivyo hawezi kusumbuliwa na mtu.
“Kutokana na hali ya hewa ya huku kwetu, nalima mboga mwaka mzima, napata pesa, napanga mwenyewe nile nini, niishi vipi. Nina nyumba yangu niliyojenga kwa jasho langu, mwanaume akiletea ujinga namtimua hata usiku wa manane na hana mahali pa kwenda kunishtaki.”
“Kwa ufupi, huku Mgeta, wanawake ndiyo wenye sauti, wanaume lazima watusikilize, hata mabinti zetu huku tumeshawafundisha kutafuta pesa ndiyo maana hatutaki waende mjini kufanya kazi za ndani kwa sababu hiyo Sh50,000 anayokwendwa kulipwa kwa mwezi, akikomaa shamba muda wa kuvuna ukifika anaipata hiyo pesa kwa siku moja tu,” amesema.
Mwanamke huyo amesema wanaume wengi wa Mgeta sio wakulima, bali wamekuwa wakikaa vilabuni na kunywa pombe, hivyo wanawake ndio wenye kuendesha maisha na kutunza familia zao kupitia kilimo cha mbogamboga.
“Mboga tunazolima ni zile zinazopendwa na kuliwa zaidi na Wazungu na ambazo hazijazoeleka na wengi kama vile kotimoli, koniflower, kabeji, njegele, maharage mabichi, karoti, hoho, bitiruti, viazi mbatata.
“Pia tunalima nyanya na matunda kama tufaa, strawberry na vanila ambapo kilimo chetu huku ni cha kumwagilia kwa sababu tuna mito na mifereji ya kutosha,” amesema Catherine.
Kwa upande wake, Lenada Vicent, mkazi wa Mgeta Nyandira, amesema sababu nyingine ya wanawake wa Mgeta kuwa na nguvu ni jiografia ya eneo hilo ambayo ni ya milima mirefu na mabonde. Pia, hali ya hewa ya baridi kali katika kipindi cha mwaka mzima.
Lenada amesema wanawake wa Mgeta ndio wamekuwa wafanyaji kazi kuliko wanaume, hivyo zile safari za kwenda shamba, mtoni kuchota maji, gulioni na kupeleka mtoto kliniki zimekuwa zikifanywa na wanawake kwa kupanda milima na kushuka.
“Kwa mazingira yaliyopo huku Mgeta, lazima wanawake tukomae miili, tuwe na msuli na wakakamavu na wenye nguvu za ajabu, maana tunapandisha milima huku kichwani tukiwa na tenga la kabichi au kiloba cha karoti, ndio maisha yetu ya kawaida tena wakati mwingine unakuta nimebeba na mtoto mgongoni,” amesema Lenada.
Ameongeza: “Pamoja na kwamba sasa hivi usafiri wa bodaboda umerahisisha, lakini sio mara zote unaweza kutumia bodaboda kwa sababu huko mashambani kuna maeneo hazifiki kutokana na milima na barabara yenyewe. Hivyo, inabidi mwanamke abebe tenga la mboga mpaka sehemu ambayo bodaboda inafika au wakati mwingine mpaka gulioni kuokoa gharama za usafiri.”
Amesema wanawake wa Mgeta ni wacheshi, sio wagomvi isipokuwa ukiwachokoza hawana uvumilivu na ni wepesi kupigana bila kujali mazingira waliopo wala jinsia ya huyo anayepigana naye.
“Wanawake wa Mgeta hawajui kujibizana, ukimuudhi anakunja ngumi mpigane, na ukipigana naye lazima upigwe kwa sababu wana ngumi nzito kutokana na mizigo wanayojitwisha kichwani, kazi ngumu wanazofanya shambani. Pia, miguu yao ina nguvu kutokana na kupanda na kushuka milima, kwa hiyo akikupiga ngwala, lazima uanguke tu,” amesema mwanamke huyo.
Kauli ya wanaume
Kwa upande wake, Prosper Mkunule, mwanaume wa Kiluguru ambaye pia ni diwani wa kata ya Bunduki Mgeta, amekiri kuwa wanaume wengi wa Mgeta sio wafanyaji kazi na kwamba mfanya kazi na anayehudumia familia ni mwanamke.
Kutokana na hali hiyo wanawake wa Mgeta wanalazimika kufanya kazi ngumu za shamba na kubeba mazao kutoka shamba hadi kwenye magulio tena wengine wakiwa na watoto mgongoni.
“Kwa msingi huo, lazima mwanamke awe mbabe, awe na sauti kwa sababu ana pesa, lazima akomae na awe na nguvu, kwa sababu yeye ndiyo mkulima na yeye ndio kuli, kweli wanawake wa Mgeta wana pesa kwa kuwa mboga wanazolima haziuzwi kwenye masoko ya kawaida, bali makubwa, supermarket na wanalima kitaalamu,” amesema Mkunule.
Ameongeza: “ukimchokoza mwanamke wa Mgeta, akakwambia nitakupiga, basi kimbia haraka sana, vinginevyo anaweza akakupiga mitama na ngumi mpaka akakung'oa meno. Kwao mwanaume sio hitaji kubwa, muda wao mwingi wanamalizia shamba na magulioni, mwanaume ukileta gubu au wivu wa kijinga, utapigwa na utafukuzwa kwenye nyumba,” amesema.
Asili ya Waluguru
Chimbuko la jamii ya Waluguru katika Mkoa wa Morogoro linatoka Mgeta, Matombo, Mkuyuni na Kolelo ambapo kila eneo wana sifa zao za kipekee.
Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15, ambaye ni kiongozi wa jamii wa Waluguru, amesema tofauti ya tabia za wanawake wa Mgeta na wa maeneo mengine, inatokana na watawala wa kikoloni waliotawala maeneo hayo.
“Wazungu ambao ni wamishionali waliingia Mgeta kutangaza injili na ili wafanikiwe, walijenga shule na kuhimiza watoto hasa wa kike kusoma huku wakijua kuwa wakimuelimisha mwanamke, wameelimisha jamii, hivyo wataweza kutangaza injili kirahisi.
“Ndiyo maana watawa wengi kwenye makanisa ya Kikatoliki, ukikutana na Mluguru, ujue ni wa Mgeta, viongozi wa Serikali, wataalamu na wakuu wa taasisi ambao ni Waluguru, ujue ni wa kutoka Mgeta,” amesema Chifu Kingalu.
Ameongeza kuwa kutokana na ubabe, ukakamavu na utafutaji wa pesa kwa wanawake wa Mgeta, ni nadra kuwakuta wanaolewa na Waluguru wa maeneo mengine.