Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru yawaomba viongozi wa dini kukemea rushwa kwa waumini uchaguzi mkuu

Muktasari:

Takukuru: Viongozi wa dini waelezeni waumini rushwa ni mbaya, haifai kuelekea uchaguzi

Dar es Salaam. Kutokana na umuhimu walionao viongozi wa dini katika kujenga maadili na mienendo ya jamii, viongozi hao wametakiwa kuwaonya na kuwakemea waumini kujihusisha na vitendo vya rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Hayo yanajiri huku joto la kisiasa likizidi kupanda wakati ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ambapo Tanzania itachagua Rais, wabunge na madiwani.

Akizungumza leo Julai 3, 2025 kwenye ufunguzi wa warsha ya wadau kujadili namna ya kuzuia na kupambana na rushwa katika Uchaguzi Mkuu 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila amesema warsha hiyo inalenga makundi maalumu kuelekea uchaguzi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila akizungumza nje ya warsha kati ya Takukuru na Viongozi wa dini. Picha na Sute Kamwelwe.

Amesema viongozi wa dini wanaushawishi mkubwa kwenye jamii kwa kuwa unawaunganisha watu wenye itikadi tofauti za kisiasa, kimichezo hivyo kukaa nao kuzungumza masuala ya rushwa wana nafasi nzuri ya kuwaelimisha waamini wao.

“Viongozi wa dini wamebeba dhamana katika kupambana na rushwa na ieleweke rushwa ni kikwazo inaathiri wananchi katika kuwapata viongozi wanaowataka, inaondoa uhalali wa viongozi, kudidimiza demokrasia,” amesema Chalamila. 

Akitaja madhara ya rushwa kwenye uchaguzi mkuu, mkuu huyo wa Takukuru amesema inavuruga usawa kwa wagombea, wenye sifa bora kukosa nafasi, kupata viongozi wasio waadilifu na waaminifu, kukosa imani na kudhalilisha watu.

Hivyo, amesema viongozi wa dini wananafasi kubwa ndio maana wamekaa nao ili wakawaambie waumini wao rushwa ni mbaya haifai.

“Ni Imani yetu kuwa kupitia warsha hii mtasaidia kuwapa elimu waumini wenu kuhusu madhara ya rushwa sababu tunajua kuwa dini zote zinakataa rushwa hivyo kufika uchaguzi mkuu waumini watajiepusha na vitendo hivyo,” amesema.

Akizungumza nje ya warsha hiyo, Sheikh wa Wilaya ya Ilala, Adam Mwinyipingu amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuzungumza na wananchi moja kwa moja ambao ndiyo wahusika wakuu wa uchaguzi.

“Rushwa inapoenea katika jamii huepelekea kupotea kwa haki, kuongezeka kwa dhulma na ufisadi, hivyo sisi kama viongozi wa dini tunapaswa kupambana kuzuia kuenea rushwa,” amesema.

Kwa upande wake kiongozi wa Buddha, Dk ILukpitiyaPannasekara amesema kwa misingi ya dini ya Buddha uongo ni moja ya kichocheo cha rushwa hivyo ni muhimu watu kuwa wakweli ili kuepuka vitendo vya rushwa.

Askofu William Mwamalanga amesema viongozi wa dini ni walimu na michango yao inatengeneza jamii yenye maadili na katika maadili mema rushwa haina nafasi.

Takukuru ilivyojipanga kudhibiti rushwa kueleka uchaguzi

Bosi huyo wa Takukuru amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi kuna msemo maarufu unaosema ‘Unatuachaje achaje’ hasa pale mgombea au mtia nia akienda kumwaga sera zake.

“Kauli hii ni mbaya na haifai kuendelezwa kwakuwa inakiuka misingi na taratibu nzuri za kidemokrasisa na inapelekea kutuletea viongozi wabovu wasiofaa,” amesema.

Chalamila amesema wataendelea kukutana na makundi mbalimbali wakiwamo wahariri wa vyombo vya habari, ingawa hadi sasa wamekutana na asasi za kiraia, viongozi wa kisiasa na wanahabari kuzungumza nao kuwaelimisha kuhusu madhara ya rushwa kwenye uchaguzi.


Jinsi ya kutoa taarifa za rushwa

Akiendelea kufafanua suala la utoaji taarifa kwa vitendo vya rushwa amesema wananchi wanatoa taarifa kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwafata maofisa, kwenda ofisini au kupiga simu na mwitikio umekuwa mzuri.

“Tunapata taarifa kutoka kwa wananchi na tunafanyia kazi kwa kuanza kufuatilia na kuanza uchunguzi,” amesema.


Rushwa ndani ya vyama vya siasa

Amesema wameshaongea na wanasiasa wakiwemo wabunge na wamewataka kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa kukaa mbali kwa kuwa hawatabaki salama.

“Tutawakamata hawatavuka salama wataharibu maisha yao ya kisiasa. Kwa sasa tunafuatilia vyama vinavyofanya mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa karibu sana,” amesema.

Akieleza mikakati zaidi amesema kwa sasa kuna njia nyingi za kutoa rushwa na wanafahamu hilo akisema wamejipanga vilivyo kudhibiti.

“Mbinu nyingi zinatumika na ni nadra kumpata mgombea akitoa rudhwa moja kwa moja. Niwahakikishie kote tumekaa vizuri na tunafuatilia na hakuna atakayesalimika huko.

Aidha ametoa rai kwa wagombea wa nafasi za uongozi kutochafuana na kukomoana kwa kutoa taarifa za uongo hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi bali wafanye siasa safi.

“Tukifanya uchunguzi na tukagundua kuwa taarifa zilizotolewa ni uongo zinalengo la kuchafuana na si za kweli tunachukua hatua,” amesema.