Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tafakuri ya Askofu Bagonza juu ya Pasaka, maisha halisi

Askofu Benson Bagonza

Muktasari:

  • Nianze kwa kuwapongeza wasomaji wote kwa kusherehekea Pasaka. Hii ni sikukuu ya kidini iliyozoeleka kiasi cha kuwafanya watu wasitafakari maana yake ni nini.

Karagwe. Nianze kwa kuwapongeza wasomaji wote kwa kusherehekea Pasaka. Hii ni sikukuu ya kidini iliyozoeleka kiasi cha kuwafanya watu wasitafakari maana yake ni nini.

Si kawaida yangu kuandika moja kwa moja katika magazeti. Huwa natafakari katika ukurasa wangu wa Facebook na wasomaji huwa huru kuchota na kupeleka katika makundi sogozi. Safari hii nimeombwa maalumu kuandika moja kwa moja na nimekubali shingo upande.

Wakati natafakari ombi hilo nilikuwa nasoma kitabu kimoja cha zamani kabatini kwangu kiitwacho HOW TO BECOME A BISHOP WITHOUT BEING RELIGIOUS (Jinsi ya kuwa Askofu bila kuwa mtu wa dini).

Mwandishi Charles Smith amenisaidia sana tangu niteuliwe kuwa askofu mwaka 2002 katika kutambua wajibu wangu kwa wenye dini na wanaodhani hawana dini au hawajali maisha ya kidini dini.

Tunaishi katika nyakati ambazo majibu ya kidini kwa maswali ya kisekula hayakidhi kiu ya wanaohoji. Matokeo yake ni kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu.

Wataalamu wetu ambao ndio viongozi wa dini kubwa, tumejikuta tuna majibu mengi ya maswali tusiyoulizwa na jamii na wakati huohuo hatuna majibu ya maswali yanayoulizwa.

Tulienda shule tangu majiundo yetu, tukaandaliwa na kupewa majibu ya maswali ambayo hatuulizwi mara kwa mara. Tuna uwezo wa kueleza kwa nini Mungu anawaacha wenye dhambi wanastawi au kwa nini Mungu anawaacha watu wema wanateseka. Lakini hayo maswali hatuulizwi, badala yake tunaulizwa kwa nini magereza yamejaa vibaka walioiba kuku lakini wezi waliovaa suti na tai wako mitaani.

Tukimwona mgonjwa tumejifunza kwamba tuhamasishe matendo ya huruma ili mgonjwa apate dawa na maji safi ya kunywa. Lakini tukikuta mgonjwa huyo tukaanza kuhoji kwa nini hana dawa au kwa nini amekunywa maji machafu akaugua, tunasutwa na macho makali kuwa tumepotoka na kupotosha.

Kwa upande wa wataalamu wetu wa kijamii na taasisi za elimu ya juu, nao wana rundo la sera zinazojibu matatizo yasiyokuwapo na hawana hazina ya kutumia kujibu maswali ya matatizo yanayoulizwa sasa hivi.

Katika makala hii fupi napenda kutoa mchango wangu kuhusiana na Pasaka.

Mimi si Myahudi. Sikuwahi kupelekwa utumwani Babeli wala Misri. Mimi siyo Musa aliyetokewa na Mungu na kutumwa kwenda kuwakomboa watu wa Mungu waliokuwa wanateseka huko Misri.

Lakini kuna ukweli fulani usioweza kupuuzwa. Musa alikuwa kijana alipoitwa na Mungu na kutumwa huko Misri. Kwa nini Mungu hakuchagua mzee kwa kazi hii ngumu, jibu analo Mungu mwenyewe.

Baadaye sana anakuja Yesu Kristo. Huyu pia alikuwa kijana na alifanya kazi yake yote na kuondoka akiwa bado kijana. Wote wawili, Musa na Bwana Yesu, ni kiini na kielelezo cha kuieleza Pasaka ina maana gani?

Upo mjadala mkali kuhusu mmomonyoko wa maadili katika jamii. Mjadala huu una makundi matatu. La kwanza ni la viongozi wa dini wanaowalaumu vijana kwamba wana maadili mabaya. Kundi la pili ni la vijana (kizazi kipya) ambalo linawalaumu wazee na viongozi wa dini kwa kukosa ubunifu na kuchelewa kuchukua hatua za kutatua matatizo ya jamii. Kundi la tatu ni la wanasiasa wanaowalaumu viongozi wa dini kwa kushindwa kufundisha maadili mema katika jamii.

Kwamba mmomonyoko wa maadili katika jamii umesababishwa na viongozi wa dini kutofanya lililo wajibu wao na kujigeuza kuwa wanasiasa.

Kwa hiyo daraja la maridhiano kati ya kizazi kipya na kizazi cha wazee walioshikilia madaraka na mambo ya zamani linahitajika. Anahitajika msuluhishi wa haki kuongoza maridhiano haya. Kulaumiana hakusaidii tena.

Serikali yetu kwa mujibu wa Katiba, haina dini na kwa hiyo masuala ya dini yako nje ya shughuli za Serikali. Kwa hiyo, Serikali isiyo na dini kuwalaumu viongozi wa dini kwa kutotimiza wajibu wao wa kidini wa kufundisha maadili ni hatari.

Ninaelewa viongozi wa Serikali wana dini na inaweza kuwa sahihi kwao kutoa lawama au hata kuhoji kwa nini viongozi wa dini hawafundishi maadili. Cha msingi wanapofanya hivyo watangaze mgongano wa masilahi kuwa wanatumikia mabwana wawili wanaopingana. Wao ni waamini wa dini lakini upande wa pili wao wanaongoza Serikali isiyo na dini.

Tukiangalia kwa makini tutagundua kuenea kwa maadili mabovu kuna uhusiano wa karibu na utendaji wa taasisi hizi mbili, dini na Serikali. Hawa wawili wanatengenezeana matatizo. Serikali inadai dini zinatengeneza matatizo kwa kutofundisha maadili na dini zinadai Serikali inaharibu maadili kwa kutojali dini inasema nini.

Kila kona ya nchi na katika kila sekta, kuna vitendo vya wazi vya kukosekana kwa maadili ya kijamii (social ethics).

Mathalan, watoto wanafundishwa kuwa waaminifu na waadilifu nyumbani na kanisani/msikitini. Wanajitahidi sana kushika sheria hizo na kuzifuata. Lakini wanapofika elimu ya juu wanakuta uaminifu haulipi.

Watu waaminifu wanateseka makazini na kuonekana ni wabaya sana. Hata vyuoni mwanafunzi anayejitahidi kujisomea anakatishwa tamaa na wanafunzi wasiosoma lakini wanafaulu.

Akiingia mitaani kutafuta kazi anakuta mwenzake aliyeshindwa darasani ameajiriwa kazi nzuri tena kwa kuitwa na kukabidhiwa ofisi wakati yeye aliyeshinda vizuri anasaga kiatu kutafuta kazi.

Huko makazini, Serikali na taasisi zake wanaweka utaratibu wa kuwazawadia watu wanaotapeli na kuvuruga mifumo ili kuwanufaisha watu au taasisi za kiitikadi. Uaminifu wao unapimwa kutokana na utii wao kwa kutekeleza wanayoagizwa kutenda na siyo kutenda kwa uadilifu na dhamiri safi.

Wimbi la kukiuka taratibu za kazi na kukosa uaminifu kwa kivuli cha maelekezo kutoka juu ni ushahidi tosha kuwa kuna watu wanaokiuka sheria kwa kutii amri batili.

Yesu Kristo alipozaliwa, alikuta nchi yake ikiwa chini ya ukoloni wa Kirumi. Mifumo yote na taasisi ilikuwa imara na amani na utulivu vilikuwa vimetawala.

Lakini aliposimama hekaluni na kutangaza kuwa “amepakwa mafuta kuwatangazia maskini habari njema” alikuwa ameondoa pazia zito machoni pa watu. Mfumo ukatikisika na taharuki ikatawala.

Utawala ulianza kwa kupuuza lakini baadaye “wazee” wakakiri ulimwengu ulikuwa nyuma yake na kumuunga mkono. Ujumbe wa Yesu uliohoji hali ya mambo ukaamsha harakati za makundi mawili, yaani wanaomuunga mkono (maskini) na wanaompinga (tabaka tawala).

Kilele kilikuwa ni yeye kukamatwa na kuuawa. Yeye akatafsiri tendo hilo kuwa ukombozi sawa tu na lile la Musa kuwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri.

Kwa hiyo vijana Musa na Yesu Kristo ni mifano mizuri ya kuieleza maana ya Pasaka. Vijana hawa ni mifano ya kuigwa na vijana wa sasa. Badala ya vijana kusubiri wafanyiwe Pasaka, wanahitaji wao wenyewe watengeneze Pasaka ya kujikomboa. Wanachohitaji si mtaji, bali uadilifu na uzalendo usio na uchawa ndani yake.

Kundi kubwa la vijana linasumbuliwa na kukosa ajira na uraibu (ulevi wa madawa na pombe). Yote mawili haya hayawezi kutatuliwa na mfumo-tawala kwa sababu una mgongano wa masilahi.

Kwa ajira, mfumo huo haujaweza kutengeneza ajira na hauwezi kuzitengeneza. Unaweza tu kuwezesha sekta binafsi kutengeneza ajira. Kwa ulevi, mfumo hauwezi kutatua hili kwa sababu ni biashara inayouingizia kipato kikubwa kwa gharama ya kuharibu vijana. Katika hali halisi mkandamizaji hawezi kugeuka ghafla kuwa mkombozi.

Ninaelewa utamu wa kueleza Pasaka kuwa ni upendo, huruma, ukarimu na kuishi kwa amani na utulivu. Ujumbe wa namna hii ni mzuri kusikilizwa na viongozi wetu na watu ambao hawana shida ya kujiuliza wapate wapi karo, bima ya afya, chakula, mavazi, maji na umeme.

Lakini maskini wengi wanaolazimika kununua haki zao, wanaolazimika kulisha vijana waliomaliza vyuo na kubaki nyumbani, wanaosumbuliwa na ushuru wa kuuza nanasi moja na tozo za miamala - kwao hawa, Pasaka yao ni kudai mabadiliko yanayoweza kuleta unafuu katika mateso yao.

Pasaka ya watu maskini ni ile inayoondoa mifarakano kati yao na wale waliowachagua ili watatue matatizo yao wakaishia kuyaongeza. Huu utaratibu wa wao kuja wanapiga magoti kuomba kura halafu wakishazipata wanataka maskini ndio wapige magoti kuwashukuru, hauna amani endelevu ndani yake.

Kwetu sisi viongozi wa dini tunalo deni kubwa si kwa maskini hawa wala watawala wetu hawa, bali kwa Mungu tunayedai alituita, akatupaka mafuta, akatupatia upako na mbwembwe nyingiii tunazofanya kuonyesha tuna kibali cha Mungu.

Huyo Mungu tunayedai kumtumikia yumo ndani ya watu hawa. Mungu huyo anadhulumiwa, ananyanyaswa, anaporwa na kukosa mtetezi.


(Makala haya yameandaliwa na Askofu Bagonza)