Sura mbili za Mchungaji Msigwa katika siasa

Uamuzi wa mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kujiunga na CCM, umeonyesha sura mbili za mwanasiasa huyo, aliyekuwa mwiba kwa chama hicho tawala kutokana na maneno yake ya ukosoaji.

Muktasari:

  • Juni 30, 2024, Msigwa alitambulishwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla kama mwanachama mpya wa chama hicho akitokea Chadema, chama alichokitumikia kwa zaidi ya miaka 20.

Dar es Salaam. Uamuzi wa mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kujiunga na CCM, umeonyesha sura mbili za mwanasiasa huyo, aliyekuwa mwiba kwa chama hicho tawala kutokana na maneno yake ya ukosoaji.

Jana, Juni 30, 2024, Msigwa alitambulishwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla kama mwanachama mpya wa chama hicho akitokea Chadema, chama alichokitumikia kwa zaidi ya miaka 20.

Akiwa Chadema, Msigwa aliwahi kutoa kauli zilizoonyesha upande wake mmoja kama mwanasiasa mwenye msimamo mkali kukitetea chama chake, na baada ya kuhamia CCM, ametoa kauli zinazoonyesha upande wake wa pili.


Kauli zake za zamani

Juni 12, 2021, kupitia mahojiano na kituo cha televisheni cha Star TV, Msigwa alisema hawezi kutweza utu wake kwa vipande 30 vya fedha au cheo ili ahamie CCM.

Alisema aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai aliwahi kumuita ofisini kwake na kumwambia ndugu yake (hayati John Magufuli) anataka ahamie CCM na asipofanya hivyo, hatopata ubunge tena.

“Nilimwambia CCM siendi na bora nisiwe mbunge na wakati watu wengine walishakwenda  Ofisi ya Spika wakati huo, ilisaidia wengi kuihama Chadema,’’alisema.

Aprili 2024, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Dodoma baada ya maandamano ya amani yaliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Msigwa aliwahoji wananchi wa Dodoma kama wanaridhika na ugumu wa maisha uliosababishwa na CCM.

“Ukienda nchi nyingi duniani, kwenye makao makuu ndio kuna watata, ukienda Ghana upinzani ni mkubwa Acra, ukienda Afrika Kusini, Johanesburg upinzani ni mkubwa kwa sababu watu ni wajanja lakini ukija Tanzania, wajanja tupo kule Iringa Wanyalukolo, ninyi hapa Dodoma mnaridhika na maumivu mnayopewa na CCM,” alisema.

Mei 2024, kwenye mkutano wa hadhara Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa alisema hali ya Watanzania ni ngumu na viongozi wameshindwa kupanga nchi kila mtu aweze kunufaika.

“Paka anayeweza kula simba aache tamaa za kula panya, kama una ndoto kubwa achana na CCM yenye mambo madogo madogo waza vitu vikubwa.Tunataka tuibadilishe nchi hii, na nchi hii itabadilika kwa kuwa na fikra pana tuachane na fikra ndogondogo,”alisema.

Agosti 2020, Msigwa akizungumza na wananchi wa Iringa Mjini alisema CCM ipo kwenye bendera lakini Chadema kipo moyoni mwa wananchi

“Kiongozi wa CCM anakwenda kukodi wananchi kupandisha bendera kwenye taa za barabarani, wanachukua wafungwa magerezani kwenda kufunga bendera ya CCM. Uchaguzi ukiwa wa huru na haki CCM hawana chao Iringa,” alisema.

Alisema muda mrefu ulitumika kumshawishi kwenda CCM lakini amekataa na wakati mwingine watu ndani ya familia walitumika.

Pia kupitia video nyingine fupi inayoonyesha mahojiano ya Mchungaji Msigwa na waandishi wa habari, aliwataka wananchi wa Iringa kumchomea nyumba na magari yake endapo watasikia amehamia CCM.

“Kwanza hao wanaonipigia ni dharau sana mimi sio mtu wa hivyo wakawarubuni watu wengine… Wakome kabisa sijawa mbinafsi kiasi hiko kwamba nataka hela kuuza utu wa wananchi,”alisema.

Hata hivyo, Juni 30, mwaka huu, baada ya kutangazwa kujiunga na CCM, Msigwa alibadilisha msimamo na kusema: “Nitashirikiana na wengine kuzunguka Tanzania nzima kuwaambia wananchi usanii wa Chadema ambao viongozi wa juu wanawaaminisha wananchi vile ambavyo hawako, na ni kitu kibaya sana.”

Msigwa alianza kutofautiana na chama chake cha zamani baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa kanda ya Nyasa na kushindwa uchaguzi huo dhidi ya mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Baada ya uchaguzi huo wa Mei 29, 2024, Msigwa alijitokeza na kulalamikia uchaguzi huo akidai kuchezewa rafu, huku akiutuhumu uongozi wa juu  kutoa maelekezo ya yeye kuangushwa kwenye uchaguzi huo.

Kabla ya kukihama chama hicho, Msigwa aliwahi kueleza kwamba hawezi kukihama chama hicho,  huku akienda mbali zaidi akisema endapo atakihama chama hicho (Chadema), basi nyumba yake ichomwe moto.

Kauli akihama nyumba yake ichomwe

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi jana, Mchungaji Msigwa amefafanua kauli hiyo akisema aliitoa katika muktadha tofauti.

“Haihusiani na sasa, niliposema nikihama Chadema nyumba yangu ichomwe, nilizungumza hivyo wakati ule wimbi la watu kuhama likifanyika tukiwa bado wabunge na wengine madiwani.

“Nilizungumza kwa maana kwamba nilikuwa nimepewa dhamana ya ubunge na ilikuwa lazima nimalize muda wa ubunge, wanaolitafsiri wakati huu wanalizungumza nje ya muktadha,” amesema Msigwa.

Msigwa amesema yeye kwa sasa ni mchezaji huru, si mbunge wala diwani, ameondoka akiwa amemaliza muda wake Chadema.

Amesema kuna mambo kama yale ambayo akiwa Chadema walikilaumu CCM, hivyo akaona bora aende CCM ambako kuna sera zinazoweza kubadilisha hali hiyo, kuliko kuwa sehemu ya watu wanaojaribu kuwatoa CCM madarakani na wao wanafanya yaleyale huku akisisitiza kuwa huko ni kupoteza muda.

Amesema katika harakati zake za kuhamia CCM, ilikuwa ni uamuzi wa siku moja, ingawa alikuwa akitafakari hadi kufikia uamuzi huo.

Hata hivyo, Msigwa alizungumzia kufikia uamuzi kipindi ambacho rufaa yake dhidi ya Sugu ikiwa bado haijasikilizwa. 

“Zaidi ya mwezi, rufaa yangu haikuwa imeshughulikiwa, wakati nyingine huwa zinashughulikiwa haraka haraka. Hicho ni kiashiria cha ukiukwaji wa kusimamia katiba.

“Hizo ni dalili tosha kwangu mimi kama nilikuwa kiongozi nimetoa malalamiko hayajafanyiwa kazi, kunaashiria ndio mambo ya ukiukwaji wa katiba,” amesema Msigwa.


Wadau wamchambua

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza amesema katika siasa, mtu anaweza kubadilika muda wowote.

Amesema vyama vya siasa ndio vinatengeneza mazingira hayo, akiitaja CCM kutokuwa na itikadi huku akikifananisha chama hicho na mkandarasi.

“Mkandarasi akiitwa kujenga anapewa anakwenda kujenga popote, kwa hiyo hakuna kitu kinachoweka watu pale kama itikadi. Mazingira ya CCM yanavutia mtu yeyote anayetaka kuingia kwenye ukandarasi, kuingia pale na kupata mradi wake mambo yakaenda,” amesema.

Hata vyama vya upinzani, amesema havina Itikadi, bali wanaangalia kilichofanywa na CCM na kuikubali au kuikataa, hivyo katika mazingira hayo, haoni mtu atakayekataa kujiunga na CCM kama ana tabia za ukandarasi.

Buberwa amesema kwa nchi ambazo demokrasia imekomaa, haitarajiwi viongozi kuhamia vyama tawala wakitokea upinzani.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda ambaye amesema suala la wanasiasa kuhama vyama vyao linaibua hisia chanya na hasi.

Kwa hisia chanya, Dk Mbunda amesema kuhama kwa wanasiasa kwenda vyama vingine ni kutokana na uhuru uliopo wa vyama vingi.

“Kuna haki ya kushiriki siasa, mgombea huru hajapewa nafasi ya kushiriki siasa, sasa ili ushiriki lazima uwe  kwenye chama, ukivurugana na chama kimoja unapata nafasi ya kwenda kwenye chama kingine.

Kwa upande wa hisia hasi, Dk Mbunda amesema Msigwa alikuwa miongoni mwa viongozi muhimu ndani ya Chadema, hivyo kuondoka kwake kutateteresha chama chake.

Amesema kuondoka kwa kiongozi huyo kunaweza kusababisha upinzani nchini kutokuwa na uwezo wa kuhoji na kukiwajibisha chama kilichopo madarakani.

“Ili vyama vya siasa kuwa imara, lazima uwe na watu ambao wanaweza kujenga hoja na kuiwajibisha Serikali,  na Msigwa alikuwa mtu wa namna hiyo, hivyo kuondoka kwake ni pigo kwa Chadema,” amesema.