Msigwa ataja kilichomuondoa Chadema, atetea kauli yake kuchomewa ‘nyumba’

Muktasari:

  • Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu uamuzi wake wa kujiunga na CCM pamoja na masuala mengine, ikiwemo kauli yake ya kwamba akihama Chadema, nyumba yake ichomwe moto.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), mwanasiasa huyo ameeleza kuwa hakuondoka Chadema kwa sababu ya kushindwa uchaguzi wa uenyekiti kanda ya Nyasa.

Jana, Juni 30, 2024, Msigwa alitambulishwa kuwa mwanachama mpya mbele ya wajumbe wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam.

Uamuzi wa mwanasiasa huyo amethibitisha tetesi zilizokuwa zikiibuliwa mara kwa mara na wadau zikimhusisha Msigwa na CCM, tangu enzi za utawala wa Hayari John Magufuli.

Katika siku za hivi karibuni, Msigwa alianza kutofautiana na Chadema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa kanda ya Nyasa na kushindwa uchaguzi huo dhidi ya mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu.

Baada ya uchaguzi huo wa Mei 29, 2024, Msigwa alijitokeza kuulalamikia, akidai kuchezewa rafu huku akimtuhumu mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutoa maelekezo ya yeye kuangushwa kwenye uchaguzi huo.

Kabla ya kukihama chama hicho, Msigwa aliwahi kueleza kwamba hawezi kuhama Chadema, huku akienda mbali zaidi akisema endapo atafanya hivyo nyumba yake ichomwe moto.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi Digital, leo Julai mosi, 2024, Mchungaji Msigwa amefafanua kauli hiyo akisema aliitoa katika muktadha tofauti.

“Kauli ile haihusiani na sasa, niliposema nikihama Chadema nyumba yangu ichomwe, nilizungumza hivyo wakati ule wimbi la watu kuhama likifanyika tukiwa bado wabunge na wengine madiwani.

“Nilizungumza kwa maana kwamba nilikuwa nimepewa dhamana ya ubunge na ilikuwa lazima nimalize muda wa ubunge, wanaolitafsiri wakati huu wanalizungumza nje ya muktadha,” amesema Msigwa.

Amesema kwa sasa yeye ni mchezaji huru, si mbunge wala diwani, ameondoka akiwa amemaliza muda wake Chadema.

Hata hivyo, amesisitiza hajaondoka Chadema baada ya kushindwa nafasi ya uenyekiti wa kanda ya Nyasa dhidi ya Sugu, bali ni kwa sababu Chadema kimepoteza sifa ya kuwa mkosoaji wa CCM.

Amesisitiza kwamba maadui zake wanaeneza uvumi huo aonekane ameondoka kwa sababu hiyo.

“Ukweli sio kwa sababu hiyo, hata ningekuwa sio mwenyekiti au ningeshindwa kihalali kama nilivyoshindwa, nisingelalamika, kilichofanya niondoke ni kwamba Chadema imepoteza sifa na hadhi ya kuwa mkosoaji wa CCM,” amesema.

Mchungaji Msigwa amesema kuna mambo kama yale ambayo akiwa Chadema walikilaumu CCM, hivyo akaona bora aende CCM ambako kuna sera zinazoweza kubadilisha hali hiyo kuliko kuwa sehemu ya watu wanaojaribu kuwatoa CCM madarakani na wao wanafanya yaleyale, huku akisisitiza huko ni kupoteza muda.

Amesema katika harakati zake za kuhamia CCM, ilikuwa ni uamuzi wa siku moja, ingawa alikuwa anatafakari hadi kufikia uamuzi huo.

Hata hivyo, Msigwa amesema amefikia uamuzi huo kipindi ambacho rufaa yake dhidi ya Sugu ikiwa bado haijasikilizwa. 

“Zaidi ya mwezi, rufaa yangu haijashughulikiwa, wakati nyingine huwa zinashughulikiwa haraka haraka, hicho ni kiashiria cha ukiukwaji wa kusimamia katiba.

“Hizo ni dalili tosha kwangu mimi kama nilikuwa kiongozi nimetoa malalamiko hayajafanyiwa kazi, kunaashiria ndio mambo ya ukiukwaji wa katiba,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alizungumzia hilo akisema rufaa yake ilikuwa isikilizwe katika kikao cha Baraza Kuu kwa kuwa mwanasiasa huyo alikuwa mjumbe wa kamati kuu.

“Tulikuwa tukisubiri chaguzi zote zimalizike ndipo tuitishe Baraza Kuu kujadili rufaa ya Msigwa, tusingeweza kujadili rufaa yake pekee, maana huenda nyingine zingejitokeza na kufanya vikao vya mara kwa mara vya Baraza Kuu ni gharama,” amesema.

Msigwa amesema ataendelea kuwa na msimamo wake hata baada ya kuhamia CCM, na kazi kubwa iliyo mbele yake ni kuzuia makosa yasifanyike kwa kuwa yuko kwenye chama tawala, hatosubiri hadi mambo yaharibike ndipo akosoe.

“Kuna tofauti kati ya kuzuia na kukosoa, hivi sasa niko chama tawala ambacho ndicho kimeshika Serikali, sio kwamba kuwepo kwangu huku ndiyo nitatetea mabaya kwa wale watakaoshindwa kutimiza majukumu yao, hapana.

“Msigwa nitabaki ni yuleyule ambaye naamini wananchi wanatakiwa wasemee, msimamo ni uleule, sijabadilika, sitanyamaza, kama kuna vitu vya hovyo vinafanyika kwa nafasi yangu na kwa kufuata taratibu za chama, nitavisemea,” amesema.

Ameongeza kwamba alipokuwa Chadema, alikuwa mkosoaji na hiyo haifanyi kuhamia kwake CCM ashindwe kufanya hivyo.

“Japo ukosoaji wa sasa utakuwa tofauti na ule wa mwanzoni, hivi ni vyama viwili, kingine kiko nje kingine kiko ndani.”

Msigwa amesema akiwa nje ya CCM alikuwa akitoa mawazo, maoni na ushauri na kutaka kuleta fikra mpya ambazo zitaleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.

“Lengo langu la kujiunga CCM ni kuendeleza hilo, pamoja na kwamba tuna vyama vya kisiasa, lakini tuna nchi ya kuijenga, hivyo maoni yangu nataka yasikilizwe kwa karibu kuliko nilivyokuwa Chadema ambako kimsingi nako nimeona kuna shida ya kidemokrasia,” amesema.

Kuhusu kugombea ubunge kwenye uchaguzi wa mwaka 2025, Msigwa amesema hiyo sio dhamira yake, kikubwa kilichompeleka CCM ni kuleta mabadiliko katika nchi.

“Hayo mengine tutajengea daraja tutakapofika, kama nitaona ni mwafaka kufanya hivyo, nitafanya na chama kikiona nafaa, kikanipa nafasi hiyo, nitasimama, lakini kwa sasa focus ni kukijenga chama na kuwaaminisha wananchi, hao wanaopitapita huko barabarani na kukosoa, sio kweli,” amesisitiza.

Msigwa amebainisha kwamba Watanzania wanahitaji uzalendo, kusimamia haki na haitakiwi kukosoa kila kitu, sehemu wanayofanya vizuri basi wapongezwe kwa kuwa wanajenga Taifa moja la Tanzania.

“Nakumbuka kuna wakati niliwahi kusifia Royal Tour ambayo ilichangia kukuza utalii, lakini ikawa nongwa, niliwahi kutoa maoni namna ya kuhifadhi Ngorongoro, napo ikawa shida.

“Hatuwezi kuwa watu wa namna hiyo, kila kitu tunakosoa, sisi sio maroboti, mimi nimekuwa mwandamizi Chadema, nimekaa miaka 20, lakini watu wajiulize imekuaje nimehama? Haiwezekani. Watu wajiulize kwanini wengi wanaoondoka Chadema wanamlaumu mtu yuleyule kuna nini? amehoji.

Mwanasiasa huyo amesema tatizo la Chadema, pamoja na mwenyekiti wake kukaa sana madarakani, hilo si tatizo kubwa, bali tatizo lililopo kwa sasa ni kwamba hakuna mambo mapya.

“Kizazi kimebadilika sana, tangu generationi (kizazi) yake (Mbowe) hadi hii ya sasa, kuna vizazi vimepita, lakini chama hakiendi na wakati, ulimwengu umebadilika. Chadema inahitaji mabadiliko makubwa, kuwajumuisha vijana na wanawake wapya, sio kuwa ileile tu,” amesema.