Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

'Ilikuwa suala la muda Msigwa kutimkia CCM'

Dar es Salaam. Lilikuwa suala la muda kwa Mchungaji Peter Msigwa kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kueleza baada ya kada huyo wa zamani wa Chadema kutimkia katika chama hicho tawala.

Msigwa ametambulishwa kuwa mwanachama mpya wa CCM leo Jumapili, Juni 30, 2024, mbele ya wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho (NEC), katika kikao kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Uamuzi wa mwanasiasa huyo umethibitisha tetesi zilizokuwa zikiibuliwa mara kwa mara na wadau zikimhusisha Msigwa na CCM, tangu enzi za utawala wa Hayati John Magufuli.

Kwa mujibu wa wanazuoni na wanasiasa, uamuzi wa Msigwa kuihama Chadema na kujiunga na CCM ulitarajiwa, kutokana na mienendo yake ndani ya chama hicho cha upinzani na kauli zake za hivi karibuni.

Mei mwaka huu, wakati anatangaza kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi wa Kanda ya Nyasa ulimtupa nje kwenye nafasi ya mwenyekiti, Msigwa alisema mifumo ya chama imetumika kumhujumu asishinde na kumshutumu mwenykiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kitendo alichosema kinaifanya Chadema kukosa uhalali wa kuikosoa CCM.

“Kama Chadema tunalalamikia Serikali ya CCM haitendi haki katika kusimamia uchaguzi, tulitakiwa tuwe mfano wa kuigwa lakini katika chaguzi zetu haki haitendeki.

“Hali hii inaleta mashaka na harufu ya uvundo wa ukiukwaji mkubwa wa haki ndani ya chama ambacho kinatakiwa kiwe mstari wa mbele katika demokrasia,” alisema Msigwa.

Hata Machi mwaka 2020, alipohukumiwa kulipa faini au kwenda jela katika kesi iliyokuwa ikimkabili yeye na viongozi wengine saba wa Chadema waliolipa faini kwa kuchangiwa na wapenzi na wafuasi wa chama, yeye alilipiwa faini hiyo ya Sh38 milioni na Hayati Magufuli, kati ya Sh40 milioni zilizohitajika na kuibua mjadala, japokuwa ilielezwa kuwa Rais huyo alikuwa na uhusiano naye kifamilia.

Sambamba hilo, Msigwa alifuatwa na gari za Serikali na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM wa wakati huo, Humphrey Polepole, jambo ambalo liliongeza dhana za nasaba yake na chama tawala. Hata hivyo, Msigwa aligoma kupanda gari hilo, badala yake aliondoka kwa gari la wakili wa Chadema.


Lilikuwa suala la muda

Kutokana na matukio hayo na mengine, uamuzi huo wa kujiunga na CCM, umeeleza ulikuwa unasubiri tu muda, kama inavyoelezwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema.

Akizungumza na Mwananchi, Mrema amesema intelijensia ya Chadema ilishatoa taarifa za mwenendo wake na kulikuwa na dalili zote za Msigwa kujiunga na chama tawala.

“Tulikuwa tunasubiri muda ufike na muda umefika leo, kwa sababu ameamua kwenda CCM tunaendelea kukijenga chama chetu,” amesema.

Mrema amezihusisha harakati za Msigwa katika siku za mwisho mwisho ndani ya Chadema na vurugu za maandalizi ya kupandisha thamani yake ili aondokea.

“Hata uko CCM Mch.ungaji Msigwa akikosa cheo ataondoka,” amesema.

Kuhusu rufaa yake ya kupinga ushindi dhidi ya Joseph Mbilinyo “Sugu”, Mrema amesema ilikuwa isikilizwe katika kikao cha Baraza Kuu, kwa sababu mwanasiasa huyo alikuwa mjumbe wa kamati kuu.

“Tulikuwa tunasubiri chaguzi zote zimalizike ndipo tuitishe Baraza Kuu kujadili rufaa ya Msigwa, tusingeweza kujadili rufaa yake pekee, maana huenda zingine zingejitokeza na kufanya vikao mara kwa mara vya Baraza Kuu kwa kuwa ni gharama,” amesema Mrema na kuwa kwa uamuzi huo na mchakato wa kusikiliza rufaa yake utakuwa umejifia hapo.

Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema angetamani kubaki kuwa naye ndani ya chama hicho.

“Nilitamani tuendelee naye kufanya kazi, lakini ni uamuzi wa mtu huwezi kuuzuia. Msigwa alikuwa ni kama kaka yangu, nilitamani tuendelea kuwa timu moja (Chadema),” amesema Lema.

Kauli kama za Mrema zimetolewa pia na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo kuwa si jambo linaloshtua kwa Msigwa kufanya uamuzi huo.

Amesema tayari kulikuwa na tetesi na hisia juu ya alichokiamua na matukio kadhaa yaliakisi matarajio hayo.

Matukio hayo kwa mujibu wa Dk Masabo, ni tuhuma zilizoibuliwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu ambazo hazikumtaja moja kwa moja lakini kama mgombea ilionekana ujumbe unamhusu.


Si pigo wala turufu

Vilevile, mwanazuoni huyo alieleza uamuzi huo wa Msigwa si pigo kwa Chadema wala turufu kwa CCM kwa kuwa hakuwa tishio kwa CCM kabla ya kujiunga nayo na hakuwa mwanachama anayetegemewa zaidi ndani ya chama alichotoka.

Kwa mtazamo wa Dk Masabo, uamuzi wa mwanasiasa huyo unaweza kuwa umechagizwa ama na ahadi ya nafasi ya uongozi serikalini au ameshindwa kuvumilia joto ndani ya chama au kukosa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, ambao umemwondolea sifa ya kuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

“Angekuwa katika hali ngumu katika chama (Chadema) na uwezekano wa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama usingekuwepo, angebaki kuwa mwanachama wa kawaida.

“Ulikuwa mjumbe wa kamati kuu na sasa unaenda kuwa mwanachama wa kawaida inahitaji uwe umeiva sana kisiasa ili kuimudu hali hiyo,” amesisitiza.

Kwa uamuzi wake huo, Dk Masabo amesema amezidi kujiweka kwenye nyakati ngumu kwa sababu haionekani nafasi ambayo atapewa kuwaondoa waliopo sasa.

“Kwa ubunge itakuwa vigumu kwa sababu kwanza ndani ya CCM yenyewe nani utamtoa umuweke Msigwa, pia hakuwa tishio kwa CCM, labda nafasi nyingine,” alisema.

Mtazamo huo umetolewa pia na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda aliyeungana na wadau wengine kusema kuwa lilikuwa ni suala muda kwa mwanasiasa huyo kuhamia CCM, hasa baada ya kushindwa na Sugu kwenye uchaguzi wa Kanda ya Nyasa.

“Lilikuwa ni suala la muda tu, ni sawa kama vile unavyomzungumzia Mpina (Luhaga) halafu ukasikia amehamia Chadema au vyama vingine vya upinzani,” amesema.

Dalili za kuondoka kwake kwa mujibu wa Dk Mbunda, zilianza kujitokeza pale alipokuwa akilalamika kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa Kanda ya Nyasa akidai kuhujumiwa.

“Ni wazi kwamba alikuwa na kinyongo kwamba hakushindwa kihalali. Msigwa ni mwanasiasa machachari anayetaka kuendelea kubaki katika mstari wa siasa, sasa ukianguka katika chama unachotakiwa kufanya siasa itakula kwako.

“Nadhani Msigwa atakuwa ameshafuatwa mara nyingi sana na CCM, sasa alivyoona nafasi hii ameitumia. Ni kitu kilichotarajiwa hasa baada ya kushindwa uenyekiti wa Nyasa,” alisema Dk Mbunda.


Wananchi Iringa

Uamuzi wa Msigwa kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Iringa, Frank Nyalusi, umeacha pengo ndani ya chama hicho na alichokifanya ametimiza haki yake ya msingi kikatiba.

“Nikisema kuondoka kwa Msigwa hakujaacha pengo lolote nitakuwa muongo, amekuwa mbunge vipindi viwili, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na kiongozi wa Kanda ya Nyasa, ameacha pengo lakini ametimiza haki ya msingi ya kikatiba,” alisema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Lyata ambaye awali alikuwa Diwani wa Kwakilosa na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa kupitia Chadema, amesema mwanasiasa huyo amefanya uamuzi wa msingi.

“Ni haki ya kila Mtanzania kuchagua chama anachopenda, hiyo ni haki yake ya msingi kabisa. Hakuna anayemzuia mtu kuchagua chama anachopenda,” amesema.

Lakini, kada wa Chadema anayeishi Frelimo mkoani Iringa, Juma Ndonde anaona Msigwa alipaswa kuvumilia, badala ya kufanya uamuzi huo.

“Nimepata mshtuko kusikia amehamia CCM, angevumilia tu kwa sababu kwenye siasa kuna mambo mengi ambayo ni ya kawaida, hata huko CCM atakutana na pilikapilika kama alizokutana nazo Chadema,” amesema Ndonde.


Nyongeza na Tumain Msowoya (Iringa)