Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Suala la gongo limeendelea kuibuka wabunge wakikomaa ihalalishwe

Muktasari:

  • Sichalwe ambaye aliwahi kuingia bungeni na pombe kali akitaka sheria itungwe kuruhusu gongo, ameendeleza msimamo huo akianza kuungwa mkono na wengine.

Dodoma. Wabunge Condester Sichalwe (Momba) na Cecil Mwambe (Ndanda) wameendelea kusisitiza msimamo wao, wakiiomba Serikali ihalalishe matumizi ya pombe ya gongo.

Wakati Sichalwe akitoa kauli hiyo leo, jana Mbunge wa Ndanda, mkoani Mtwara, Cecil Mwambe, naye aliitaka Serikali kutafsiri upya sheria zilizopo ili kuwaruhusu wakulima wa korosho kutumia zao hilo kuzalisha pombe aina ya gongo.

Leo, Aprili 15, 2025, mbunge Sichalwe kwa mara ya tano amehoji Serikali kuhusu sababu ya kuwepo kwa masharti makali ya kuzuia pombe ya gongo, ilhali aina nyingine nyingi za pombe zinaingizwa nchini na kuchangia mmomonyoko wa maadili kwa vijana.

Sichalwe, ambaye mwaka juzi aliwashtua wengi kwa kuingia bungeni na chupa za pombe kali, aliitaka Serikali kuwasaidia wabunifu wa pombe za kienyeji kufanya utafiti na kuziweka kwenye vifungashio vya kisasa ili kuzipatia soko rasmi.

Mbunge huyo, ambaye mwaka jana kwa mara ya nne, aliendelea kushikilia msimamo wake wa kuitaka Serikali iruhusu pombe ya gongo, leo ni mara ya tano kutoa msimamo huo.

Sichalwe katika msisitizo wake huo aliiomba Serikali kusaidia katika upatikanaji wa mtambo wa kutenganisha ‘ethanol’ ambayo ni kilevi salama na ‘methanol’, kemikali hatari inayopatikana kwenye pombe hiyo, ili kuifanya iwe salama kwa matumizi ya wanywaji.

Mbunge huyo katika swali lake la msingi leo bungeni amehoji ni mitambo mingapi ya kutenganisha ‘ethanol’ na ‘methanol’ kwenye gongo imesambazwa kwa watengenezaji wa pombe hiyo ili iwe salama kwa wanywaji.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Naibu Waziri wa Madini, Dk Stephen Kiluswa amesema mpaka sasa viwanda vya kutengeneza pombe kali nchini inayokidhi viwango, vinaendelea kuanzishwa kwa kupata mafunzo na ushauri wa kitaalamu kutoka Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido).

Dk Kiluswa ametaja taasisi zingine zinazotoa elimu ni Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na miongoni mwao wanaendelea kupata alama ya ubora kwa kukidhi vigezo.

Amesema Sido itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za maendeleo ya teknolojia ikiwemo Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (Temdo), Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec).

"Na kwa ushirikiano wa karibu wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kuboresha teknolojia za kuchakata pombe kali kwa teknolojia rahisi, ili watengenezaji wengi waweze kutengeneza pombe bora inayostahili kwa matumizi ya binadamu," amesema Dk Kiluswa.

Dk Kiluswa amesema gongo ni pombe yenye kilevi ambayo imekuwa ikitengenezwa kienyeji.

Ameliambia Bunge kuwa Serikali haijahalalisha pombe ya gongo kwa sababu ya kuwa na madhara makubwa katika mwili wa binadamu, na mpaka sasa hakuna mitambo ya kutengeneza kinywaji hicho iliyosambazwa kwa wananchi.

Dk Kiluswa amesema kwa sasa, Serikali haijaanzisha mpango wa kusambaza mitambo ya gongo kwa wananchi wanaojishughulisha na uzalishaji wa pombe hiyo.

Jana, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, alijibu swali la mbunge Mwambe kuhusu hoja yake ya kutafsiri upya sheria zilizopo ili kuwaruhusu wakulima wa korosho kutumia zao hilo, kuzalisha pombe aina ya gongo.

Kwa mujibu wa Sagini, Sheria ya Intoxication Liquors Act inaweka utaratibu wa kuwasimamia watengenezaji na wauzaji wa pombe za asili, na mtu yeyote anayekusudia kutengeneza au kuuza pombe ya asili anapaswa kuomba leseni kwa mamlaka husika ya serikali za mitaa.

Ameongeza kuwa, kwa sheria hiyo gongo siyo miongoni mwa pombe za asili (local liquid) kama inavyotafsiriwa katika kifungu cha tatu cha sheria husika.