Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbunge mwingine aomba gongo ya korosho ihalalishwe

Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe wakati akiuliza swali kwa Naibu waziri wa Kilimo, David Silinde bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Aprili 14, 2025.

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Sheria ya Intoxication Liquors Act inaweka utaratibu wa kuwasimamia watengenezaji na wauzaji wa pombe za asili

Dodoma. Mbunge wa Ndanda (CCM), Cecil Mwambe leo Jumatatu April 14, 2025 bungeni jijini Dodoma ameihoji Serikali kama haioni haja ya kutafsiri sheria ili kuruhusu wakulima wa korosho wazalishe gongo.

"Je Serikali haioni haja ya kutafsiri Sheria ya Intoxication Liquors Act 1968 ili kutoa fursa kwa wakulima kupata kipato kwenye gongo ya mabibo," ameuliza Mwambe.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amejibu swali hilo akisema Sheria ya Intoxication Liquors Act inaweka utaratibu wa kuwasimamia watengenezaji na wauzaji wa pombe za asili.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yeyote anayekusudia kutengeneza au kuuza pombe ya asili anapaswa kuomba leseni kwa mamlaka husika ya Serikali za mitaa.

"Aidha kwa sheria hii, gongo siyo miongoni mwa pombe za asili (local liquid) kama inavyotafsiriwa katika kifungu cha tatu cha sheri husika," amesema Silinde.

Amezitaja pombe aina ya gongo, machozi ya simba, moshi au umeme kama ilivyotafsiriwa na kifungu cha 2 cha Sheria ya Kudhibiti Utengenezaji wa Pombe za Asili sura 384 kuwa inaweza kutengenezwa ikiwa mtengenezaji ana leseni.

Amekitaja kifungu cha 19 cha Sheria ya kudhibiti pombe za asili sura ya 384 ambacho kinataka leseni hiyo kutolewa na waziri mwenye dhamana ya viwanda.

Serikali imesema ni kosa la jinai kuzalisha pombe ya asili ikiwamo gongo bila leseni, hivyo wakulima wa korosho wana nafasi ya kujiongezea kipato kupitia gongo ya mabibo ikiwa wataomba leseni ya kuzalisha pombe hiyo.

Katika swali la nyongeza, Mbambe ameuliza kama Serikali itakuwa tayari kutoa elimu kuhusu utaratibu huo ili wananchi wapate fursa ya kuongeza thamani ya zao la korosho.

Mwambe amesema mpango huo ukikubalika wananchi wa Mkoa wa Mtwara na maeneo yanayolima korosho wataongeza thamani ya mazao yao.

Hii si mara ya kwanza kwa wabunge kuhoji kuhusu gongo kuruhusiwa, Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe mara kadhaa ndani ya Bunge amekuwa akiomba Serikali kuwapatia mtambo wa kisasa wananchi wake ili waruhusiwe kupika na kuuza pombe aina ya gongo.

Mei 22, 2024, akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2024/25, Sichalwe aliendelea kwa mara ya nne kuitaka  Serikali ya Tanzania kusaidia mtambo wa kutenganisha ‘ethanol’ ambayo ni kilevi na ‘methanol’ ambayo ni kemikali kwenye gongo ili iwe salama kwa wanywaji.

Mbunge huyo ambaye alisema yeye si mtumiaji wa pombe, aliendelea kutoa kilio chake kwa Serikali kuitaka iwajali wajasiriamali wadogo waliotoa wazo la kutengeneza pombe kienyeji aina ya gongo ambayo kwa mujibu wa sheria ni haramu.

Sichalwe kwenye Bunge la bajeti la mwaka 2023/24 aliingia bungeni na chupa kadhaa pombe kali zinazotengenezwa nje ya nchi na zinazotengenezwa ndani ya nchi, akihoji kama ni dhambi kwa nini zinaingizwa nchini, zinatengenezwa nchini, Watanzania wanapata ajira na mapato yake yanatumika kwenye familia na serikalini.

Mwaka 2018 akiwa bungeni, mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba akichangia hoja bungeni amesema kutokana na kuyumba kwa soko la mazao ni vyema Serikali ikaona kuna ulazima wa kuruhusu gongo izalishwe nchini ili kunyanyua soko hilo la mazao.