Prime
Stendi ya mabasi Kijichi ilivyogeuzwa uwanja wa mpira
Muktasari:
- Stendi hiyo, iliyofanya kazi kwa siku chache Oktoba 2022, ni miongoni mwa miradi ya uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), uliolenga kuifanya Mbagala kuwa na stendi kubwa ya daladala na mabasi.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa inabuni miradi mipya ya kuwasogezea wananchi huduma karibu, baadhi ya miradi hiyo imekosa tija baada ya wananchi kukataa kuitumia.
Moja ya miradi hiyo ni stendi ya mabasi ya mikoa ya kusini iliyojengwa Mbagala Kijichi, Wilaya ya Temeke kwa zaidi ya Sh3 bilioni, lakini haijafanya kazi iliyokusudiwa badala yake imegeuzwa uwanja wa mpira.
Stendi hiyo, iliyofanya kazi kwa siku chache Oktoba 2022, ni miongoni mwa miradi ya uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), uliolenga kuifanya Mbagala kuwa na stendi kubwa ya daladala na mabasi yanayotoka mikoa ya kusini, kwa kuwa stendi inayotumika sasa inamilikiwa na mtu binafsi.
Mwonekano wa kituo cha mabasi ya kwenda mikoa ya kusini kilichojengwa na Manispaa ya Temeke eneo la Kijichi jijini Dar es Salaam, ambacho kimebadilishwa matumizi baada ya madereva wa mabasi kugomea kupeleka mabasi kutokana na changamoto ya ufinyu wa miundombinu ya barabara. Picha na Said Powa
Pia, stendi hiyo ilitarajiwa kuwa moja ya vyanzo vya mapato vya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, lakini mambo hayakwenda kama ilivyopangwa. Baada ya siku chache tangu kuanza kutumika, wadau wake wakiwemo wenye magari na abiria waliikataa na kurejea katika stendi ya awali iliyopo Mbagala Rangi Tatu.
Moja ya malalamiko kutoka kwa madereva ni kuwa eneo hilo halikuwa rafiki kutokana na kuwa na mchanga mwingi uliosababisha magari kukwama.
Katibu wa Umoja wa Madereva wa Mabasi ya Kanda ya Kusini, Said Abdallah, alisema wakati huo kuwa barabara za kuingia stendi hiyo ni nyembamba, hali inayofanya magari kusubiri ili kupishana.
Kwa upande wa abiria, baadhi yao walieleza kuwa eneo hilo liko mbali kufikika, hivyo wakaona ni bora kuendelea kutumia stendi ya Mbagala Rangi Tatu.
Kituo cha mabasi ya kwenda mikoa ya kusini kilichojengwa na Manispaa ya Temeke eneo la Kijichi jijini Dar es Salaam, ambacho kimebadilishwa matumizi baada ya madereva wa mabasi kugomea kupeleka mabasi kutokana na changamoto ya ufinyu wa miundombinu ya barabara. Picha na Said Powa
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Joomary Satura, aliwahi kuliambia Mwananchi kuwa kutokana na kukataliwa kwa stendi hiyo, walikuwa na mpango wa kubadili matumizi yake kwa kuweka vivutio vitakavyowashawishi watu kwenda eneo hilo, ikiwemo michezo ya watoto, jambo ambalo hadi sasa halijatekelezwa.
Akizungumzia suala hilo sasa, Satura amesema hawajaweza kuweka michezo ya watoto kama walivyoahidi kwa sababu hawajapata mwekezaji wa kufanya uwekezaji huo.
Mwananchi imefika katika stendi hiyo na kukuta hakuna shughuli zinazoendelea, zaidi ya magoli ya mpira wa kikapu na mpira wa miguu yaliyowekwa kwa ajili ya michezo ya watu wazima.
Mbali na magoli hayo, eneo ambalo mabasi yalikuwa yakiegeshwa sasa limechorwa mistari ya alama za michezo hiyo.
Mabasi yakiwa katika Stendi ya Kijichi iliyojengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo mikoa ya Kusini na kugharimu Sh3.9 bilioni. Picha na Maktaba
Pia, sehemu ya abiria ya kusubiria imeonekana kutumiwa na watu kwa ajili ya kupumzika au kukutana na ndugu, marafiki na wenza wao.
Fremu zaidi ya 10 za maduka zilizopo pembezoni mwa stendi hiyo zimeonekana kufungwa, huku vibanda zaidi ya 50 vya biashara vilivyojengwa nje ya stendi vikigeuka magofu baada ya wafanyabiashara kuvikimbia.
Kuna utulivu
Mmoja wa wananchi wa eneo la Kijichi aliyekutwa kwenye stendi hiyo, amesema huwa jioni anapenda kwenda kukaa eneo hilo kwa sababu kuna utulivu, hasa akiwa hataki kuchangamana na watu.
“Hii stendi ina maeneo ya kukaa, hivyo nikiona kuna mambo yaliyonitinga kichwani na kuhitaji utulivu, huwa nakuja huku nakaa peke yangu na wakati mwingine napiga kabisa usingizi,” amesema Rajab Kibaya, mkazi wa Kijichi.
Kwa upande wake, Noel Sham amesema yeye ni mwanamichezo, hivyo nyakati za jioni huenda kucheza mpira katika eneo hilo na hakuna malipo.
“Kuna wakati huwa tunakuwa na mechi hapa za ujirani mwema, kwani kiwanja si unaona tunacho. Hivyo kwa namna nyingine stendi hii kuachwa imekuwa faida kwetu, kwani huku hatuna kiwanja kizuri cha kuchezea, japo ningetamani kibadilishwe na kuwekwa nyasi kama ingewezekana.”
Anita Joram, mchezaji wa mpira wa kikapu, amesema imekuwa faraja kwao kuwekwa kwa mchezo huo hapo, kwani imewaepushia adha ya kufuata viwanja vya mbali, jambo ambalo lilikuwa likimlazimu kutumia nauli na gharama nyingine.
Wakati wanamichezo hao wakifurahia hali hiyo, Enock Kilua, mkazi wa Mbagala Kuu, amesema kilichofanyika hapo ni uharibifu wa fedha ambazo zingeweza kupelekwa katika matumizi mengine ikiwemo huduma za afya na elimu.
“Hata wewe unavyoona (mwandishi), huku nani anaweza kuja kuleta basi au daladala yake, kulivyokaa kushoto halafu ni mbali kwa abiria wengi, labda waseme kama waliweka kwa ajili ya abiria wa Kijichi.
‘Hivi kuna mtu anaweza kutoka Chamazi aje hadi huku akiwa na mizigo? Hiyo gharama yake si sawa na kwenda mkoani? Kama unavyojua Dar es Salaam hii, ukiwa na mizigo kwenye usafiri wa umma ni mateso. Ukiacha kukataliwa, ukibebwa utapigwa hela hadi utamani kuahirisha safari.”
Baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo wamesema kwao imekuwa maumivu makubwa kuondolewa kwa stendi hiyo, ukizingatia walitumia gharama kubwa kujenga mabanda.
“Wakati stendi hii inakaribia kuanza kazi, tulikatiwa maeneo na kupewa wiki mbili tuwe tumejenga vibanda kwa gharama zetu, ambapo binafsi nilitumia si chini ya Sh500, 000 nikijua zitarudi baada ya stendi kuanza kazi.
“Lakini hali haikuwa hivyo kwani baada ya siku chache baadhi ya madereva na wakatishaji tiketi walitwambia, ‘Tutawaacha wenyewe huku na vibanda vyenu, hatupo tayari kuja huku’, na kweli ikawa hivyo,” anasema mfanyabiashara huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hadija.
Hata hivyo, amesema sasa anafanya biashara hapo kwa kuwa hataki kubaki nyumbani, na ilimlazimu kuomba kuhamia kibanda cha mbele kwani alichokuwa nacho kilikuwa mbali na barabara.
Mwendesha bodaboda, Andrew Nyoni, amesema baada ya stendi hiyo kuanza kazi ilikuwa kicheko kwao kwa sababu walikuwa wakipata wateja, lakini sasa wameishia kusubiri wanaokuja kupata huduma katika ofisi za Serikali zilizopo eneo hilo.