Sophia Mjema ateuliwa kuwa mshauri wa Rais

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Sophia Mjema kuwa mshauri wake.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Sophia Mjema kuwa mshauri wake kwenye masuala ya Wanawake na Makundi Maalumu.
Sophia anaukwaa wadhifa huo, akitoka kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi alioutumikia kwa miezi tisa tangu alipoteuliwa Januari 14 mwaka huu.
Uteuzi wa Mjema umetangazwa leo, Oktoba 22, 2023 kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus.
Hata hivyo, Mjema anateuliwa kushika wadhifa huo mpya katikati ya wimbi la taarifa kuwa huenda CCM ikafanya mabadiliko katika wajumbe wa sekretarieti yake.
Gazeti la Mwananchi hivi karibuni liliripoti juu ya kufanyika kwa kikao cha NEC ya dharura leo, ambayo pamoja na mambo mengine, inatarajiwa kuja na mabadiliko katika wajumbe wa sekretarieti ya CCM.
Mbali na mabadiliko hayo, ajenda nyingine kulingana na vyanzo ambavyo gazeti la Mwananchi limevinukuu, kikao hicho kitajadili kuhusu mikataba wa uendelezaji na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam, kati ya Serikali ya Tanzania na DP World ya Dubai.
Kwa muktadha huo, uteuzi mpya wa Mjema ni kama umeanza kujibu kile kilichoelezwa na vyanzo mbalimbali ambavyo Mwananchi imekuwa ikivinukuu.
Oktoba 10 mwaka huu, akiwa na wadhifa wake wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia aliwahi kunukuliwa kuwa kutokana na kinachofanywa na Rais Samia anastahili kuendelea kusalia madarakani kwa miaka 10 (kuanzia 2025 hadi 3035)
Kauli hiyo iliibua mjadala ndani na nje ya CCM ambapo walimlaumu kwa kupotosha na kwenda kinyume na Katiba ya Tanzania.
Hoja ya waliokuwa wakimpinga ni kuwa ibara ya 40 (4) ya Katiba inayosema endapo Makamu wa Rais atashika kiti cha Rais kitakachokuwa wazi kwa mujibu wa ibara ya 37 (5) kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea urais mara mbili.
Lakini, ibara hiyo inaeleza iwapo atashika nafasi hiyo kwa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea mara moja tu.
Na kwa kuwa, Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 na mwaka 2025 atatimiza miaka mitatu madarakani, hivyo kwa mujibu wa Katiba ataruhusiwa kugombea mara moja tu.
Huyu ndiye Mjema
Kujulikana kwake katika siasa, kulianza mwaka 2005 alipowania ubunge wa viti maalum katika Mkoa wa Kilimanjaro, hata hivyo hakufanikiwa alishika nafasi ya tano.
Milango ya kuyaishi maisha ya siasa, ilimfungukia mwaka 2006, alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete wa wakati huo, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Utumishi wake katika wadhifa huo, ulikoma mwaka 2012, alipohamishiwa wilayani Temeke na baadaye Ilala.
Uamuzi wake wa kuwania ubunge katika Jimbo la Ilala, ulimtenganisha na wadhifa huo, lakini baadaye Oktoba 8, 2021 aliteuliwa na Rais Samia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Hata hivyo, miaka miwili baadaye aliteuliwa kuwa sehemu ya sekretarieti ya CCM, Januari 14, mwaka huu.