Mjema awashukia viongozi, ataka wawafuate wananchi

Katibu wa Itikadi, siasa na Uenezi wa CCM Taifa Sophia Mjema
Muktasari:
- Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameagizwa kushuka chini kwa wananchi ili kujua matatizo, kero zao na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri kupelekewa.
Mpwapwa. Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameagizwa kushuka chini kwa wananchi ili kujua matatizo, kero zao na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri kupelekewa.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Juni 16, 2023 na Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa Sophia Mjema katika salamu zake Kwa wanachama wa shina namba nane Kata ya Kingiti wilayani Mpwapwa.
Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Katibu Mkuu wa chama hicho Daniel Chongolo wakati akikagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wanachama wa chama hicho.
Mjema amesema siri mojawapo ya kuyafikia maendeleo shirikishi ni kuanza miradi na wananchi kwa ngazi ya chini ambako wanaibua watu wenyewe.
"Tatizo letu hatuoni umuhimu wa kuwasikiliza na kuzungumza na wenzetu walio ngazi ya chini, unataka kusaidia watu lakini umekaa huko juu huendi kuanza nao chini, lazima tubadirike ndugu zangu," amesema Mjema.
Amesema CCM Kwa upande wake kitaendelea kuunga Mkono juhudi za wananchi ambao wanapambana katika kujitafutia maendeleo yao kwa njia halali.
Kingine amesema chama hicho hakiwezi kuwa na ngazi kisipowekeza kwa ngazi ya chini ambako ndipo iliko nguvu yake.
Mwenyekiti wa shina namba 8 Daniel Msihi amesema changamoto inayowakabili wananchi ni kutoona umuhimu wa kulipa ada za mwaka.
Msihi ametaja sababu ya kutolipia ada za wanachama inatokana na changamoto za kimfumo ambapo hasa ulipaji ada kielektroniki ambapo vijijini hakuna mfumo huo.