Sita wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya ndugu 17

Muktasari:
- Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu sita waliokutwa na hatia ya kufanya mauaji ya ndugu 17 wa familia moja.
Musoma. Mahakama Kuu Kanda ya Musoma imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu sita waliokutwa na hatia ya kufanya mauaji ya ndugu 17 wa familia moja.
Waliohukumiwa kunyongwa ni Juma Mgaya, Aloyce Nyakumu, Nyakangara Biraso, Marwa Mgaya, Nyakangara Mgaya na Sadok Ikaka ambao kwa pamoja wanadaiwa kushiriki mauaji hayo mwaka 2010 ambayo chanzo chake ni kulipiza kisasi.
Katika kesi hiyo namba 56 ya mwaka 2018 watu hao wanadaiwa kufanya mauaji eneo la Mungaranjabo manispaa ya Musoma usiku wa kuamkia Februari 16, 2010.
Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa Januari 15, 2021 Jaji Mustapha Siyani amesema mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa jamhuri juu ya watu hao kuhusika na tukio hilo la kinyama.
Katika hukumu hiyo, Jaji Siyani amewaachia huru washtakiwa watatu, Magigi Magigi, Kumbata Buruai na Ngoso Ngoso baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa hawakuwa na hatia na makosa waliyoshakiwa nayo.
Amesema kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo watu hao sita walikuwa na nia ya dhati ya kuwaua ndugu hao.