Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siri ya maisha ya Mbowe

Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Jina la Freeman Mbowe ni maarufu katika siasa na kidogo kwenye biashara, lakini ukimsikiliza mwenyekiti huyo wa Chadema akizungumzia maisha yake unabaini kwamba kuna upande wake mwingine usiofahamika.

Dar es Salaam. Jina la Freeman Mbowe ni maarufu katika siasa na kidogo kwenye biashara, lakini ukimsikiliza mwenyekiti huyo wa Chadema akizungumzia maisha yake unabaini kwamba kuna upande wake mwingine usiofahamika.

 Akizungumzia maisha yake hatua kwa hatua alipohojiwa na Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe ameeleza mambo mbalimbali aliyopitia, ikiwemo alivyotimuliwa ofisini na aliyekuwa naibu gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bob Makani akaamua kuacha kazi moja kwa moja BoT.

Siri ya maisha ya Mbowe

 “Mzee Makani akasema, unauona ule mlango, nikiinuka hapa nisikuone. Kweli niliondoka nikiwa nahema kwa nguvu, nikafika kwa sekretari wake akaniuliza mbona unahema? Nikamwambia nilichokutana nacho huko hapana.

Hiyo ndiyo siku niliyoondoka Benki Kuu, sikurudi tena,” alisema Mbowe akieleza alivyotimuliwa BoT na Makani mwaka 1986. Katika mahojiano hayo yaliyopo katika Podcast ya NADJ KHAMIS & TUNDU LISSU iliyopo mitandaoni, Mbowe alisema alianza kazi BoT Aprili 1982 akiwa ofisa wa benki katika idara ya fedha za kigeni, ikiwa ni ajira za moja kwa moja kwa wahitimu wa kidato cha sita na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa katika kambi za Ruvu na Lugalo.

Kupitia programu hiyo inayoitwa Speaking out with Tundu Lissu, mwanasiasa hiyo anayeishi Ubelgiji amepanga kuwahoji watu mbalimbali na kurusha mahojiano hayo mtan[1]daoni kila Jumanne.

Kupitia mahojiano hayo, Mbowe anasema akiwa BoT, gavana alikuwa Edwin Mtei, ambaye baadaye akawa mwanzilishi na mwenyekiti wa kwanza wa Chadema na Bob Makani, aliyewahi kuwa katibu mkuu na mwenyekiti wa pili chama hicho alikuwa naibu gavana.

Akieleza sababu ya kuondoka BoT, Mbowe, aliyekuwa akifanya kazi kwa kutekeleza Sheria ya Azimio la Musoma la kila mhitimu kufanya kazi miaka miwili kabla ya kujiunga na chuo kikuu, anasema pia alikuwa akimsaidia baba yake, Aikaeli Mbowe katika biashara zake na hivyo kuelemewa na kazi nyingi.

 “Kwa kuwa biashara za Mzee (Mbowe) zilikuwa Dar es Salaam, nikaanza kumsaidia Mzee biashara hizo. Kwa hiyo wakati nikiwa kazini tukipata mapumziko nakimbia kwenye ofisi ya baba nasaidia kazi, narudi tena saa nane kuendelea.

Freeman Mbowe

“Baada ya mama ambaye alikuwa ni mkurugenzi mwenza kufariki, baba aliniteua kuziba nafasi yake. Lakini kabla ya hapo alimteua dada ambaye baadaye alikwenda Marekani, hivyo nikapewa mimi.

 Kwa hiyo nikawa nafanya kazi Benki Kuu lakini pia ni mfanyabiashara wakati huohuo.” Kutokana na kuwa na majukumu mengi, baada ya miaka miwili ya kufanya kazi kwisha ambapo alitakiwa ajiunge na chuo kikuu, alishindwa kwenda baada ya kutingwa na biashara za baba yake.

Hata hivyo, anasema ilipofika mwaka 1986 aliamua kuendelea na shule.

“Nikaenda kwa gavana msaidizi aliyehusika na utawala wakati ule, Bob Makani ili niombe likizo bila malipo nikamilishe masomo yangu, halafu niendelee na biashara kwa sababu niliona nazidiwa.

“Nilikwenda ofisini kwake nikamweleza, ulikuwa ni wakati wa chakula cha mchana. Nikitambua kuwa Makani alikuwa anafahamiana na baba, nikadhani atanisaidia. Mzee Makani akasema, unauona ule mlango? nikiinuka hapa nisikuone,” alisema Mbowe.

Alisema baada ya hapo alijikita kwenye biashara za baba yake na nyingine alizoanzisha mwenyewe.

Aanzisha kampuni

Akifafanua alivyoanza biashara zake, Mbowe alisema hadi mwaka 1985 akishirikiana na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Martin Omary, walianzisha biashara ya kuvua na kuuza samaki nje ya nchi. “Tukaunda kampuni ya FM Exports (Freeman and Martin Export) ilikuwa mwaka 1985.

 Ilikuwa ngumu wakati huo kwenda kukamata kamba kochi wanaopatikana kwenye miamba ya bahari na kusafirisha. “Nikaingia rasmi kwenye uvuvi nikanunua boti. Nakwenda kuchukua prawns, kuna eneo lilikuwa linaitwa Mwamba Mkuu, tunakwenda na boti mpaka Nyamisati.

“Ilikuwa boti ya injini moja tunakwenda mpaka Mafia tunachukua samaki aina ya kamba, tunazisindika na kusafirisha nje ya nchi. Wakati huo soko kubwa ni Botswana, baadaye Oman na Spain,” alisema.

 Alisema pia biashara aliyoifanya ilikuwa ni ya kuuza matunda nje ya nchi akilitumia Shirila la Ndege la Gulf Air.

Nyerere na familia ya Mbowe

 Akirejea maisha yake ya awali, Mbowe alisema baba yake alikuwa mfanyabiashara maarufu kabla hata Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 na alikuwa na ushawishi mkubwa kwa watawala wa jadi wa mikoa ya Kaskazini.

“Mzee Mbowe alikuwa na umashuhuri katika mikoa ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na alikuwa na uhusiano na watawala wa kiasili, kuanzia Mangi Maruma wa Rombo, Mangi Shangali wa Machame, alikuwa karibu nao kutokana na umashuhuri wake,” alisema.

 Katika mazingira hayo, alisema baba yake aliweza kuwashawishi watawala hao wa jadi kuikubaliTanu na kuunga mkono mapambano ua uhuru. “Mzee aliingia kwenye siasa akiwa rafiki mkubwa wa Kambona (Oscar) na baadaye Mwalimu (Julius) Nyerere na wengine waliokuwa wakipigania uhuru.

Mzee pia alikuwa amewekeza Dar es Salaam wakati huo ukiitwa Mkoa wa Pwani,” alisema.

Nyerere amsaidia kununua gari nje

Kutokana na ukaribu kati ya baba yake na Mwalimu Nyerere, Mbowe ameeleza jinsi alivyolazimika kumtumia kiongozi huyo ili kupata kibali cha kuagiza gari lake la kwanza nje ya nchi.

“Sasa wakati ule mimi naanza biashara zangu gari yangu ya kwanza kuingiza ilikuwa BMW 520i.

Wakati najaribu kuingiza gari yangu ya kwanza nilikwama kibali. Basi baba kwa kuwa alikuwa na ukaribu na Mwalimu akamfuata akamwambia mwanangu anataka kuingiza gari, akasema mpeni Mbowe kibali,” amesema.

 Katika uhusiano huo wa Nyerere na Mzee Aikaeli Mbowe, baba yake ndiye ndiye alimwakilisha Mwalimu Nyerere kupeleka posa ya Makongoro Nyerere wakati anamuoa Jaji Nyerere.

Maisha ya ujana

Katika mahojiano hayo, Mbowe alianza kwa kueleza historia ya maisha yake akisema kuwa aliza[1]liwa Septemba 14, 1961 akiwa mtoto wa 10 kwa baba Aikael Alfayo Mbowe na mtoto wa tisa kwa mama yake Aishi Ephraim Shuma.

Alizaliwa kijijini Machame na kubatizwa Desemba 9, 1961 siku ya Uhuru wa Tanganyika. Alisoma shule ya msingi Lambo mkoani Kilimanjaro kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba mwaka 1975. “Mwaka 1976 nikaenda kusoma shule ya sekondari Kolila na nilipofika kidato cha pili alihamishiwa shule ya sekondari Kibaha.

“Nikasoma mpaka mwaka 1979, wakati huo vita vya Kagera ina[1]pamba moto, nikaondoka hapo nikachaguliwa kuendelea na kida[1]to cha tano shule ya sekondari Ihungo Kagera,” amesema. Kutokana na hofu ya vita hiyo, amesema mama yake alitaka asiende mkoani Kagera na ilikuwa ahamishiwe shule ya sekondari ya Minaki ambako pia mchepuo aliokuwa akisoma wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE) ulikuwepo, lakini baba yake akakataa.

“Baba akasema kama wenzake wamekwenda kusoma huko na kama ni vita basi imkute huko huko, basi nikaenda huko uwanja wa vita, Ihungo. Nikasoma Ihungo tukamaliza.

Mbowe amekumbushia moja ya matukio yaliyotokea baada ya vita ya Kagera kwisha, wakati wanajeshi wanarejea kutoka uwanja wa mapambano eneo la Bunazi, wanafunzi wa shule za sekondari walitakiwa kwenda kuwapokea.

“Wakati huo shule kubwa za Ihungo, Rugambwa, Kahororo, Bukoba sekondari, Umumwani, Ntungamo, tulitakiwa tutembee mpaka Mutukula mpakani na tui[1]litembea usiku na mchana kwenda kuwapokea wanajeshi.”

Baada ya kunaliza kidato cha sita Kagera, anasema alipata ufaulu kwenda chuo kikuu, lakini alitakiwa kwanza kwenda Jeshi la Kujenga Taifa na alikwenda Ruvu JKT (Pwani) na baada ya kumaliza mafunzo ya ukuruta ndipo alijiunga na BoT. “Wakati huo unajaza fomu ya kazi ukiwa kidato cha sita, kazi ya kwanza niliyojaza ni kwenda Benki Kuu, kazi ya pili Mambo ya Nje kazi ya tatu sikumbuki,” alisema.

 Inaendelea, usikose kesho.