Simulizi za waraibu wa dawa za kulevya na maisha ya kutengwa, kudharauliwa
Suleyman Abbas wakati akitumia dawa za kulevya (kushoto) na baada ya kupata tiba ya kuacha dawa hizo na kuendelea na maisha ya kawaida (kulia).
Muktasari:
- Mkoani Mwanza, zaidi ya watu 2000 walikutwa katika vijiwe wakijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi, skanka, heroin pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa mwaka 2025.
Mwanza. “Nilitengwa na jamii, hadi familia yangu... hata paka wa nyumbani alikuwa na thamani kubwa. Nikienda kuchukua chakula napewa nje ya geti kwenye mfuko.”
Hiyo ni simulizi ya kijana Suleyman Abbas aliyeanza kutumia bangi akiwa na miaka 14, alipokuwa darasa la saba, na kufikia kidato cha kwanza tayari alikuwa ameanza kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, alizovuta kwa miaka saba kabla ya kupata tiba ya kuacha.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya yaliyofanyika Kisesa mkoani Mwanza leo Ijumaa Juni 26, 2026, Suleyman amesema maisha yake yalibadilika vibaya kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Amesema aliwahi kupelekwa jela na mama yake ili abadilike, lakini jitihada hizo hazikufua dafu hadi alipofikishwa katika kituo cha tiba ya uraibu (sober house), ndipo alipotambua kuwa alikuwa na tatizo la uraibu.
“Rimoti ikipotea nyumbani naambiwa Suleyman alikuwepo. Nilishapelekwa kwa waganga wa jadi, kwa ma Ostadhi, Wachungaji lakini ilishindikana,” amesema.
Ameongeza: “Nilikuwa mraibu wa heroine, pombe, bangi, ugoro lakini nashukuru nimerudi kuwa tofauti na kijana aliyekuwa tegemezi wa madawa.”
Sasa Suleyman ana familia na anashukuru Serikali kwa juhudi za kudhibiti dawa za kulevya, akisema yeye ni miongoni mwa waliodhalilika na kupoteza ndoto zao kutokana na athari za dawa hizo.
“Sober house si lazima utumie heroin, hata kama unatumia pombe na kushindwa kuendesha maisha yako we mwenyewe...kuna mtu bila kunywa pombe hafanyi kazi,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng'wilabuzu Ludigija akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Kimatiafa ya Kupambana na dawa za kulevya yaliyofanyika Kisesa, mkoani Mwanza.
Mratibu wa Lake Zone Sober House Mwanza, Jovin Onesmo amesema hata yeye alipitia changamoto kama hizo kabla ya kupata tiba.
“Nyumbani kwetu mimi nilikuwa siruhusiwi kuingia ndani... wanaambiwa mpeni chakula huko huko lakini leo hii nashukuru Mungu kwa kuzileta hizi mamlaka na sober house....” amesema.
Amesema aliwahi kwenda jela zaidi ya mara nne lakini hakupata msaada wa kweli.
“Nilikuwa sisaidiwi bali nilikuwa nazidi nikitoka kule nahasira sana lakini nilivyoenda sober house nikapata vitu vingi sana,” amesema.
Amesema baada ya kupata tiba, aliamua kusaidia vijana wengine kupitia kituo hicho ambapo hadi sasa zaidi ya vijana 100 wameachana na uraibu wa dawa za kulevya.
Mnufaika wa dawa za methadone, Abdallah Nassib, ambaye alitumia dawa hizo kwa zaidi ya miaka 16, amesema changamoto kubwa iliyokuwepo awali ilikuwa ni ukosefu wa elimu.
“Ugumu uliyokuwepo ni sisi kufikiwa na elimu siyo kama sasa hivi tunakwenda masikani na kuwapa elimu wenzetu…kwa hiyo sisi tulikuwa tunaamini hiki kitu hakiwezekani,” amesema.
Amesema baada ya kupata tiba, yeye na wenzake walianza kufanya shughuli za ujasiriamali ili kujipatia kipato, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kutokuaminika kutokana na historia zao.
“Tunahitaji kusajili kikundi chetu hivyo tunapata ugumu labda kwa sababu ya majina yetu au sifa ambazo zilikuwa huko nyuma lakini tunaomba kupata sapoti vikundi vyetu viwe vinasajiliwa ili tupate namna ya kujikwamua,” amesema.
Kwa upande wake, Neema Julius amesema alijikuta akiingia katika matumizi ya dawa za kulevya baada ya kushawishiwa na marafiki.
Kaimu Kamishina Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Ziwa, Wamba Msafiri amesema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika operesheni zao, lakini wanapambana nazo kwa namna zinavyokuja.
“Tunapata changamoto mbalimbali katika operasheni zetu hasa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakibadilisha mbinu za kuingiza dawa hizo jijini Mwanza, ufanyaji biashara na matumizi.
“Lakini na sisi tumekuwa tukibadilika kadri wanavyobadilisha mbinu... tunaendana nao sambamba wakipanda juu na sisi tunapanda juu,” amesema.
Amesema badala ya kuendelea kubadilisha mbinu, ni vyema wahusika wakaachana na biashara hiyo na kujikita katika shughuli halali zenye manufaa kwa jamii.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umeathirika kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani kama bangi na mirungi.
Hata hivyo, amesema operesheni mbalimbali zilizofanywa zimeanza kuleta mafanikio, ambapo uzalishaji na matumizi ya dawa hizo umeanza kupungua na jamii kuanza kuelewa madhara yake.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng'wilabuzu Ludigija amesema mwaka 2025 zaidi ya watuhumiwa 300 walikamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya na kufikishwa mahakamani, ambapo baadhi yao walihukumiwa kifungo cha maisha, wengine miaka 30 na wengine kulipa faini.
Ameongeza kuwa kupitia operesheni hizo, zaidi ya watu 2000 walikutwa katika vijiwe wakijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi, skanka, heroin pamoja na dawa tiba zenye asili ya kulevya.