Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi wanufaika wenye ulemavu walivyojikwamua kupitia fedha za Tasaf

Muktasari:

  • Walengwa wa fedha za Tasaf wameeleza namna walivyoanzisha biashara kupitia fedha hizo.

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, baadhi yao, wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), wamesimulia walivyojibana kupitia fedha walizokuwa wakizipata kwenye mfuko huo hadi kuanzisha biashara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na vyombo vya habari vilivyowatembelea kujionea maendeleo yao jijini Dar es Salaam, wamesema kupitia fedha hizo ambazo walikuwa wakipata kila baada ya miezi miwili, zimewasaidia kuanza kutengeneza na kuuza bidhaa kama sabuni, mikoba na urembo.

Nuru Ally (48), mkazi wa Kigogo Mbuyuni, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam amesema kwa sasa anajingiizia kipato kutokana na utengenezaji wa bidhaa za viungo vya pilau, chai, mikoba, urembo na sabuni za vyooni.

Nuru amenufaika tangu mwaka 2014, ni mama wa watoto wanne, amefanikiwa kupata ujuzi wa ujasiriamali na kuendesha shughuli za uzalishaji bidhaa hizo nyumbani kwake, hatua ambayo inawasaidia kujiendesha kimaisha yeye na familia yake.

Kwa upande mwingine amesikitishwa na kukosekana kwa soko la uhakika, jambo linalomfanya abaki na bidhaa kwa muda mrefu.

“Changamoto ni kupata fursa za kuuza bidhaa zangu. Naomba kama kuna uwezekano wa kuunganishwa na soko, kwa sababu hivi sasa nategemea kutembeza tu mtaani,” amesema.

Hata hivyo, amekiri imesaidia kubadilisha maisha yake na ya familia ukilinganisha na jinsi walivyokuwa kabla ya kuwa mnufaika.

Kwa upande wake, Amina Mrupe, mkazi wa Mlandizi Mtongani katika Kata ya Mtongani mkoani Pwani amesimulia alivyokuwa akipata Sh30,000 ikamsaidia kuanza kuinuka kimaisha hadi pale alipopatiwa kiasi cha Sh500,000 kilichomwezesha kuanza kuuza batiki pamoja na karanga mbichi na za kukaanga.

“Tasaf nimejiunga mwaka 2014 na ilipofika mwaka 2023 nikaondolewa ili kutoa nafasi kwa wengine. Kabla ya Tasaf nilikuwa nafanya biashara kama kutengeneza ubuyu, bisi, karanga mbichi na kavu lakini baada ya ya kuwa mnufanika nikaanza kupata ruzuku na sasa natengeneza batiki lakini wakati huohuo nikawa naendelea kuuza na karanga,” amesimulia.

Pamoja na kusaidiwa na Tasaf, ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa kuwapa ruzuku ambazo zitawasaidia kufanya shughuli za kiuchumi kujipatia riziki.

Ofisa Mawasiliano wa Tasaf, Meleckzedeck Nduya amesema mfuko unajivunia kuwawezesha walemavu, hasa wale wa kaya zinazonufaika na mradi.

“Walemavu wanahitaji kuwezeshwa sio tu kwa lengo la kuwezesha kumudu maisha yao ya kila siku, lakini kufanya wao ni sehemu ya mchango wa kiuchumi ukuaji; uchumi shirikishi unahitaji ushiriki wa makundi yote katika jamii.

Tasaf inawawezesha watu wenye ulemavu katika kaya kufaidika na mpango wa kuondoa umaskini,” amesema.

Mkurugenzi wa Miradi wa Tasaf, John Steven amewapongeza watu wenye ulemavu kutoka katika kaya za walengwa kwa jitihada wanazoonesha katika kupambana na umaskini.

"Tasaf inafarijika sana kuona mko vizuri katika kupambana na umaskini na hakika mnautendea haki msaada mnaopewa na mfuko wa huu," amesema.