Simulizi soko la Simu 2000 lilivyoteketea, laacha vilio
Muktasari:
- Tukio hilo limetokea Jumamosi, Aprili 4, 2026, ambapo moto huo kwa mujibu wa mashuhuda ulianza saa 10 kuelekea 11 jioni na kuteketeza zaidi ya vibanda 500 huku mashedi sita yaliyokuwa yamejengwa na halmashauri na vibanda 280 vikinusurika.
Dar es Salaam. Ilianza kama siku nyingine za kawaida katika soko la Simu 2000 jijini Dar es Salaam, kelele za wafanyabiashara kuwavuta wateja, pamoja na makondakta wa daladala kuwahimiza abiria kupanda daladala zao ili waweze kufika maeneo mbalimbali.
Wote hao wakiwa na matumaini ya kupata chochote kitu kwa ajili ya kuendesha familia zao.
Lakini ghafla, ndoto za wafanyabiashara katika soko hilo ziligeuka kuwa moshi mzito uliotanda angani baada ya soko hilo kuungua Aprili 4, 2026 saa 10 kuelekea saa 11 jioni kwa mujibu wa mashuhuda na kusababisha na kuteketeza zaidi ya vibanda 500.
Hakuna aliyedhani kuwa ndani ya saa chache tu, eneo hilo lingebadilika na kutanda moto na moshi mzito, ikiteketeza ndoto za mamia ya wajasiriamali waliokuwa wakitegemea vibanda vyao kama chanzo pekee cha maisha.
Mabaki ya mabanda yaliyoteketea kwa moto uliozuka Aprili 4, 2026 katika soko la Simu 2000 lililopo katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Moto huo si tu uliteketeza vibanda na bidhaa, bali pia akiba za maisha, mipango ya familia na matumaini ya kesho ya wafanyabiashara katika eneo hilo.
Leo, mabaki ya mabanda yaliyoteketea yanaonekana kama kumbukumbu ya ndoto zilizopotea ghafla.
Mwananchi imefika katika eneo hilo na kuwashuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamesimama karibu na majivu wakitazama kwa huzuni eneo ambalo jana lilikuwa chanzo cha riziki zao.
Wengine tayari wanaanza kupanga namna ya kuanza upya, hata kama ni kwa kuweka meza ndogo pembeni ya barabara.
Tumpesifa Mwakasege ni mmoja wa wafanyabiashara walioathirika na kuungua kwa soko hilo aliyekuwa akijishughulisha na uuzaji wa nguo za mtumba na duka.
Tumpesifa ambaye ni mama wa watoto wanne amesema Aprili 4, 2026 ilianza na matumaini ya kukua zaidi kwa biashara yake baada ya kufanikiwa kwenda Kariakoo na kufunga mzigo kwa ajili ya kuongeza bidhaa katika biashara zake.
“Hapa sokoni nilikuwa ninavibanda viwili, siku ya tukio niliwahi kwenda Kariakoo na kufunga mzigo wenye thamani ya zaidi ya milioni tatu na majira ya saa 9 alasiri nikafanikiwa kufika dukani na kuukabidhi kwa vijana ili waufungue na kuanza kuupanga ili niweze kuwahi kanisani kuabudu na kumshukuru Mungu”amesema Tumpesifa.
Mabaki ya mabanda yaliyoteketea kwa moto uliozuka Aprili 4, 2026 katika soko la Simu 2000 lililopo katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa muda mchache baada ya kufika kanisani alishangaa kuona amepigiwa simu nyingi na vijana waliokuwa wakimsaidia kuuza biashara pamoja na wafanyabiashara wenzake wa karibu jambo lililompa hofu.
“Nilitoka nje kupiga simu ili nijue kulikoni ndipo nikapewa taarifa kuwa soko limeungua na hawakufanikiwa kuokoa bidhaa zaidi ya midoli miwili ya kutundika nguo hadi mzigo mpya niliokuwa nimetoka kuufunga nao umeungua nilihisi naota nikatoka mbio kwenda kushuhudia”
“Ndipo nilipokuta vibanda viwili vyote vimeteketea hadi sasa sijui nitaishije, sijui nitasomeshaje watoto wangu, akiba yote niliikomba na kuiwekeza katika biashara ambayo ndani ya muda mfupi ikateketea yote,”ameeleza Tumpesifa huku machozi yakimbubujika.
Aisha Shabani ambaye alikuwa akijishughulisha na uuzaji wa nguo za ndani katika soko hilo amesimulia kuwa alipokuwa akiendelea kuwahudumia wateja wake majira ya jioni alishtushwa na sauti kubwa iliyokuwa ikisema ‘moto moto’.
Aisha amesema baada ya kutoka nje aliona moto mkubwa uliokuwa ukiteketeza vibanda vya jirani jambo lililomfanya kupata bumbuwazi asijue nini la kufanya.
Hata hivyo anasema wateja aliokuwa akiwahudumia walishirikiana kumsaidia kuokoa baadhi ya bidhaa, hata hivyo viliishia kuibiwa na baadhi ya watu waliokuwa katika eneo hilo kwa lengo la kuiba.
“Tulifanikiwa kukoa baadhi ya vitu na kuvipeleka barabarani hata hivyo viliibiwa na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu hivyo sikufanikiwa kuambulia kitu na kibanda chote kimeteketea,”
“Biashara hii ndio ilikuwa inanifanya namudu gharama za maisha kwangu na wazazi wangu hadi sasa nimechanganyikiwa sijui hatima yangu,”amesema.
Hamisi Omari ambaye naye ni mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo amesema alijikuta akiokoa midoli miwili ya kuuzia nguo baada ya kutumia muda mwingi kusaidia wenzake kuokoa bidhaa zao.
“Baada ya kuona moto unawaka nilikimbilia katika vibanda vya wafanyabiashara wenzangu kuwasaidia kuokoa bidhaa kwa bahati mbaya wakati narudi katika kibanda changu nakuta tayari moto umeshaunguza bidhaa zote, nimeokoa midoli miwili tu,”
"Wakati nachukua midoli miwili nipeleke chini nirudie mingine, moto ukanipiga usoni pa! nikakimbia," anasimulia Hamisi ambaye anasema amepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni mbili.
Mwenyekiti wa kamati ya soko hilo Musa Ndile, anaelezea kuwa alipata taarifa za moto huo saa 10:00 jioni kuelekea saa 11:00 jioni Aprili 4, 2026 ambapo ulianzia katikati ya mabanda ya wafanyabiashara.
"Tulipofika, tulikuta mabanda kadhaa yameshashika moto," amesimulia Ndile.
Amesema yeye na wenzake walijaribu mbinu ya kuondoa kingo za juu za mabanda ili kutengeneza mwanya ambao ungezuia moto usivuke kwenda upande mwingine.
Hata hivyo, jitihada hizo hazikufanikiwa kwani kikosi cha zimamoto kilipofika, moto ulikuwa umeshavuka tayari kutokana na kasi ya upepo na aina ya vifaa vya ujenzi vilivyotumika kujengea mabanda hayo.
Ndile ameshauri eneo hilo lisafishwe kwa haraka na kuruhusu wafanyabiashara kuweka hata meza za muda za kuendelea kupata riziki ya kulisha familia na kulipa mikopo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Aprili 4, 2026, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kinondoni, Joseph Chacha amesema walipata taarifa ya kutokea kwa ajali hiyo saa 11 jioni na kwa kushirikiana na vikosi vya Mbweni, Lugalo na Ilala walifanikiwa kutoa mitambo kwa ajili ya kwenda kuudhibiti moto huo, licha ya hadi wanafika zaidi ya nusu ya vibanda vilivyokuwepo hapo vilikuwa vimeungua.
"Kwa tathmini ya haraka hadi sasa zaidi ya vibanda 500 vimeungua huku 280 vikinusurika na mashedi sita," amesema Kamanda Chacha.Kwa mujibu wa kamanda huyo, katika vibanda hivyo kulikuwa na mchanganyiko wa biashara ambazo zimejengwa kwa malighafi ya mbao, jambo lililochangia moto kusambaa kwa haraka.
"Hata hivyo, pamoja na kutokea kwa ajali hii, tunashukuru hakuna majeruhi wala kifo zaidi ya kuteketea kwa mali," amesema Kamanda Chacha.
Kutokana na hilo, Kamanda huyo ametoa rai ya kujengwa kwa vibanda ambavyo si rahisi kushika moto, lakini pia kuwepo na vikinga moto ambavyo ajali itakapotokea vitasaidia moto kutosambaa maeneo mbalimbali.
Moto ukiteketeza mabanda Aprili 4, 2026 katika soko la Simu 2000 lililopo katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, amesema baada ya kumaliza shughuli ya uzimaji moto wataanzisha uchunguzi kubaini nini hasa kilisababisha moto huo.
Leo Aprili 05, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza mamlaka za uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo, kufanya tathmini ya madhara na hasara iliyotokea na kuchukulia kwa hatua stahiki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, Rais Samia amewapa pole waliopoteza mali zao na wateja watakaokosa huduma kwa muda.