Prime
Simulizi kifo cha mwanachuo Ustawi wa Jamii

Muktasari:
- Chuo cha Ustawi wa Jamii katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana Aprili 25, 2025 kimelaani vitendo vya kinyama na kikatili, ambavyo ni kinyume cha misingi ya utu, haki za binadamu, sheria za nchi na maadili ya Kitanzania.
Dar es Salaam. Wakati mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Elizabeth Maguha, ukitarajiwa kuzikwa leo, Aprili 26, 2025, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, familia na majirani wamesimulia mkasa wa kifo chake.
Elizabeth (23), aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya usimamizi wa rasilimali watu akiwa mwaka wa pili wa masomo, alifariki dunia Aprili 23, 2025, kwa kuchomwa na kisu. Mtuhumiwa wa mauaji hayo anadaiwa kuwa mpenzi wake.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Yombo Dovya, wilayani Temeke, Dar es Salaam, hatua chache kutoka nyumbani kwao alikokuwa akiishi na mama yake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alipotafutwa na Mwananchi Aprili 25 na 26, simu yake haikupatikana hewani.
Rahma Mnyeto, mama wa Elizabeth, amesema anatarajia Jeshi la Polisi litachukua hatua ili mtuhumiwa akamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
Ilivyokuwa
Stella Setebe, mtoto wa mama yake mdogo na Elizabeth, amesema awali ndugu yake huyo alikuwa na rafiki yake aitwaye Elizabeth kwenye banda lao la biashara ya samaki lililopo barabara ya Mcharingeni, ambako alikuwa akifanya kazi baada ya kutoka chuoni.
Amesema siku ya tukio, ilipofika saa mbili usiku, kwa kuwa mvua ilikuwa ikinyesha, hapakuwa na biashara wakaamua kufunga.
Amesema aliomba mwamvuli kwa rafiki yake Elizabeth, lakini wakaondoka pamoja, hivyo yeye aliachana nao njiani.
"Niliachana nao njiani nikaenda kwetu kumwangalia mtoto wangu, wao wakaendelea na safari kwa kuwa wanakaa mtaa wa mbele unaoitwa Uwazi," amesema Stella.
Amedai kuwa wakati wawili hao wakielekea nyumbani, mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa akiwafuatilia bila wao kujua.
"Ghafla aliwavamia na kutaka kumchoma kisu Elizabeth, rafiki yake aliwahi kwa kumkinga kwa mkono akimtaka akimbie. Alishindwa kuondoka na kumuacha mwenzake ndipo alipochomwa kisu mara tatu ndugu yetu na kusababisha umauti," amesema.
Amesema kabla ya tukio la mauaji lililotokea saa 2:00 usiku, mchana saa nane walipokuwa wakiuza samaki, walimuona mtuhumiwa akiwachungulia na kujificha.
"Tulipomuona mchana anatuchungulia, hatukujua kuwa alikuwa na mipango ya kumuua ndugu yetu, laiti tungejua tungechukua tahadhari mapema," amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Yombo Dovya, Denis Moyo, amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa mkoani wiki tatu zilizopita kabla ya kurejea na kutekeleza tukio hilo.
Amedai kwa namna walivyomfuatilia ni kama alijipanga kutekeleza mauaji, kwani hata chumba alichokuwa anaishi walikuta amehamisha vitu vyote na kubakiza mkeka pekee.
Amesema mtuhumiwa alikuwa akijulikana nyumbani kwa kina Elizabeth, ikidaiwa alikuwa na uhusiano naye kwa muda mrefu tangu akisoma ngazi ya astashahada (cheti).
Paulo, mtoto wa mmiliki wa nyumba waliyokuwa wakiishi Elizabeth na mama yake, amedai mtuhumiwa walikuwa wakimfahamu na walishawahi kushuhudia wakigombana mara kwa mara.
Amedai siku tatu kabla ya kifo cha Elizabeth walikimbizana hadi ndani ya geti nyumbani hapo na mtuhumiwa alionywa na majirani kwa kitendo hicho.
Daniel Obuya, anayeishi jirani na eneo la tukio la mauaji lilipotokea, amesema lilipotokea mvua ilikuwa ikinyesha.
Amesema alisikia kelele za watu kuomba msaada, na alipotoka nje alikuta Elizabeth akiwa amelowa damu kwenye fulana aliyokuwa amevaa, mgongoni kukiwa na kisu kimenasa.
"Baada ya muda mfupi akaja jirani mwingine, tukasaidiana kumbeba, tukatafuta usafiri wa kumpeleka hospitali. Rafiki yake alikuwa amejeruhiwa mkononi," amesema Obuya.
Amesema mazingira ya eneo la tukio kuna kichochoro kirefu cha mita zaidi ya 100, kikizungukwa na kuta za nyumba za watu.
"Kwa kuwa kuta hizo hazina madirisha, ni ngumu kujua hata kelele zinapotokea, kwani kila mtu anakuwa kajifungia ndani," amesema.
Kutokana na mazingira ya eneo hilo, amesema waliwahi kuweka ukuta lakini kelele za wananchi zikawa nyingi ukavunjwa, ila si sehemu salama kwa watu kupita.
Amesema matukio ya uhalifu yamekuwa yakitokea eneo hilo mara kwa mara, watu wamekuwa wakikabwa na kuibiwa mali zao.
Kauli ya chuo
Chuo cha Ustawi wa Jamii katika taarifa kwa umma iliyotolewa jana, Aprili 25, kimelaani vitendo vya kinyama na kikatili vya namna hiyo, ambavyo ni kinyume cha misingi ya utu, haki za binadamu, sheria za nchi na maadili ya Kitanzania.
"Menejimenti na watumishi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wanajumuiya wa chuo kufuatia tukio hili baya na la kusikitisha," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko.
Chuo kimetoa wito kwa wanafunzi kutoa taarifa mapema pindi wanapoona viashiria vya ukatili wa aina yoyote katika madawati ya jinsia chuoni, vituo vya polisi au kwa kupiga namba 116, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya ukatili katika jamii.