Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 10 za maumivu ya mgawo wa umeme

Muktasari:

Wakati ratiba ya mgawo wa umeme katika baadhi ya maeneo nchini wa siku kumi ikiwa haijatoka, wananchi, wakiwamo wafanyabiashara wadogo na sekta binafsi wanahofu shughuli zao kwenda mrama.

Dar es Salaam. Wakati ratiba ya mgawo wa umeme katika baadhi ya maeneo nchini wa siku kumi ikiwa haijatoka, wananchi, wakiwamo wafanyabiashara wadogo na sekta binafsi wanahofu shughuli zao kwenda mrama.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) juzi Ijumaa lilitangaza kuwapo maboresho ya vituo vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi l vinavyotegemewa kuzalisha megawati 185 na Ubungo lll megawati 112 kuwa vitasababisha mgawo nchini

Taarifa hiyo kwa umma inaeleza kuwa, upungufu huo wa umeme hautakuwa nchi nzima, isipokuwa kwa baadhi ya maeneo, lakini kila eneo litakaloathirika litapewa taarifa ni kwa muda gani kukosekana kwa umeme kutadumu.

“Lengo ni kuwawezesha wateja na wananchi kuweza kujipanga katika shughuli zao za kiuchumi na hata viwanda vikubwa vipange ratiba nzuri ya rasilimali watu kutokana na upatikanaji wa umeme,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande.

Pia, alisema Tanesco watatumia mwanya huo wa kukatika umeme kufanya matengenezo katika miundombinu ya usambazaji umeme, kwa kuwa kukatikakatika kwa huduma hiyo kunasababishwa na uchakavu.

Jackson Shayo, ambaye ni mfanyabiashara wa kuchonga na kuchomelea vyuma Tegeta Nyuki jijini Dar es Salaam alisema umeme ndiyo kila kitu kwake.

“Mimi nachonga bidhaa tofauti za vyuma na kuchomelea, hapa nina oda ya kufunga magrili kwenye nyumba ya mtu wiki ijayo, nawaza bila umeme itakuwaje, hata kazi ndogo ndogo za kufanya hapa ofisini zitasimama, jenereta la kusukuma mashine hii ni gharama kubwa, ngoja tusubiri tuone itakuwaje,” alisema Shayo.

Muuza duka la vyakula, Asnath Salomon alisema itabidi apunguze oda ya baadhi ya bidhaa, hasa zinazoharibika haraka ili kuepuka hasara kutakapokuwa na changamoto ya umeme.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)Francis Nanai alisema suala la kukatika kwa umeme linapaswa kuchukuliwa kwa ukubwa wake na si kuwataarifu watumiaji, bali kutafuta suluhisho la kuepusha kukatika kwake.

Alisema kukatika kwa umeme kutaleta athari za mauzo ya ndani na nje ya nchi na pia uzalishaji unapungua.

“Kuna ahueni tulikuwa tumeanza kuiona katika uwekezaji na ufanyaji wa biashara hapa nchini, hata mauzo yetu kwa nchi jirani yalianza kuimarika, lakini bila nishati ya umeme ya uhakika tutarudi nyuma kwa kasi, athari hasi za kukatika kwa umeme ni nyingi,” alisema Nanai.

Mkurugenzi wa Sera na Uchechemuzi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa alisema hali hiyo ya upungufu wa umeme huenda ikasababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na kupanda kwa bei za bidhaa sokoni kutokana na upatikanaji kuwa mdogo kuliko mahitaji.

“Kutakuwa na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa kuwa viwandani kutakuwa na jenereta za dharura ambazo hutumia dizeli, hiyo ni gharama kubwa kwenye uendeshaji wa kiwanda, lakini kuna viwanda vinavyotumia mitambo mikubwa ambayo sio rahisi mtu kuwa na jenereta za kuviendesha, hivyo itabidi visimamishe uzalishaji,” alisema Mnyenyelwa.

Mtaalamu wa Uchumi, Dk Abel Kinyondo alisema Tanesco inapaswa kutoa taarifa kamili mapema kuhusu mgawo utakavyokuwa, maeneo yatakayoathirika na siku ambazo watakosa huduma hiyo.

“Lengo la tangazo ni watu wajioangeze, kama ni wa kiwandani wajiandae kutumia nishati mbadala hata kama ni kuagiza kutoka nje, au kuongeza uzalishaji zaidi siku ambazo umeme bado upo ili kufidia siku utakapokatika na kupanga ratiba yao na mipango yao,” alisema Dk Kinyondo.

Pia, alisema kuna haja ya kutafuta wataalamu au utaalamu kutoka nje kuhusu suala la matengenezo kwa kuwa, nchi nyingi zilishatoka kwenye zama za kuzima umeme wakati wa matengenezo, badala yake matengenezo yanafanyika na huduma itaendelea kama kawaida.

Novemba 18, 2021 Tanesco ilitangaza kupungua kwa umeme, ikisema mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kupungua kwa maji katika vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa maji, hivyo kutakuwa na upungufu wa megawati 345.

Ilisema inachukua hatua za haraka kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kwa kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo ya Ubungo I inayozalisha megawati 25, ikisema itaendelea kutumia na vyanzo vingine mbadala kuhakikisha nishati hiyo inapatikana muda wote.

Hata hivyo, matarajio ya Watanzania, hasa waliounganishwa katika gridi ya Taifa ilikuwa ni kusahau adha ya umeme baada ya kujengwa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam lililogharimu Sh2.3 trilioni.

Mwaka 2015 Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alizindua mradi wa kwanza wa umeme unaotokana na bomba hilo (Kinyerezi 1), akisema alianza na tatizo la mgawo wa umeme na sasa anaondoka nalo.


Matengenezo ya miundombinu

Juzi, alipotembelea maboresho ya upanuzi wa huduma hiyo katika mradi wa Kinyerezi l, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande alisema mpaka sasa uzalishaji kutoka mitambo ya ubungo lll umefikia megawati 60 ambazo tayari zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Pia, alisema kazi ya upanuzi wa kituo cha Kinyerezi l inaendelea vizuri na megawati 70 zimeanza kupatikana na ifikapo Agosti 2022 kazi hiyo itakuwa imekamilika na kufikia uzalishaji wa megawati 335 kutoka megawati 150.

“Mitambo hii inaongezwa ili iweze kuzalisha umeme, hivyo mahitaji ya gesi asilia kuongezeka ambapo inalazimu kufanya uboreshaji wa mfumo wa gesi kwenye mifumo ya Tanzania Petroleum Development Company, (TPDC) na Pan African Energy Tanzania, (PAET),” alisema Maharage.