Sheria za elimu kuhuishwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Muktasari:
- Baada ya kukamilika kwa rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023, sasa ni zamu ya mapitio ya sheria za elimu.
Dodoma. Serikali imetangaza kuanza kufanya mapitio ya sheria za elimu nchini mara baada ya kukamilika na kupitishwa kwa rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Adolf Mkenda ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule kwa wakuu wa shule za msingi mjini Bagamoyo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Oktoba 14, 2023 na kitengo cha mawasiliano ya wizara hiyo, imesema mchakato huo utaanza mara baada ya tamko la kuanza kwa utekelezaji wa sera hiyo.
Taarifa imemnukuu waiziri huyo akisema kuwa ili sera hiyo itekelezwe kwa ufanisi, Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 na sheria nyingine zinazohusu elimu ni lazima zifanyiwe mapitio, ili ziendane na mabadiliko ya elimu yatakayofanyika nchini.
"Rasimu ya sera inayotarajiwa kuanza kutumika mwakani imeweka mkazo katika ubora wa walimu, mkazo katika kuwaendeleza walimu walio kazini na pia tutawachuja wanaoingia katika kada hiyo ili kulinda hadhi walimu, tunataka walimu bora na si bora walimu," Waziri Mkenda amesema katika taarifa hiyo.
Profesa Mkenda amesema mabadiliko ya mitaala yamekwenda sambamba na mapitio ya sera kwa kuwa katika sera kuna mabadiliko makubwa yamefanyika; na kwamba mitaala hiyo ipo katika tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania na kuwataka wadau na wananchi kuisoma na kuielewa.
Amewataka wakuu wao wa shule kuwa vinara na chachu ya kuhakikisha mageuzi hayo makubwa ya elimu yanafahamika kwa wadau na wananchi, lakini pia kuhakikisha wanasimamia maadili ya walimu hasa katika suala la malezi na usalama wa watoto wanaowafundisha.
Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo Waziri Mkenda amesema Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo kwa walimu kazini kwa kupitia Vituo vya Walimu (TRCs) na kwamba yatakayokuwa yakifanyika katika kimkoa, kikanda na kitaifa ili kuwajengea umahiri.
Aidha, Mkenda amewataka Wakuu hao wa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk Sixtone Masanja amesema mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza yanahusisha mikoa saba.
Amesema walimu wakuu 4,516 wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea umahiri katika uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule.
Amesema kuwa mafunzo mengine yaliyotolewa ni pamoja na uendeshaji wa ofisi ya mkuu wa shule, ukusanyaji wa takwimu na uaandaaji wa mpango wa jumla wa maendeleo ya shule na motisha kwa walimu.
"Mafunzo haya yameandaliwa baada ya kufanyika kwa utafiti na kusoma tafiti nyingine za wanazuoni wengine juu ya uongozi na usimamizi wa shule na elimu kwa ujumla,”amesema.
Dk Masanja amesema tafiti hizo zilionyesha uhitaji wa mafunzo kwenye maeneo hayo, hivyo wanaimani kubwa baada ya mafunzo wakuu wa shule wataenda kusimamia shule zao kwa ufanisi zaidi na kuinua ubora wa elimu.