Waziri wa Elimu azungumzia mwanafunzi aliyedai nafasi yake imeuzwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda
Rombo. Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ameona taarifa inayosamba mtandaoni ikieleza mwanafunzi aliyemaliza Shule ya Sekondari Mkombozi iliyopo Wilaya ya Same, Safael Tawel Elirehema kuwa alifaulu na kupangiwa kujiunga na kidato cha tano Shule ya Sekondari Namwai iliyopo Siha na aliporiti shuleni hapo alikuta nafasi yake imechukuliwa na mtu mwingine ambapo amesema taarifa hiyo imefanyiwa kazi na kesho itatolewa taarifa rasmi.
Mkenda ametoa taarifa hiyo jana Septemba 25 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari mkoani Kilimanjaro.
Amesema timu kutoka wizarani kwa kushirikiana na Tamisemi wamefuatilia taarifa hiyo na wameshakusanya taarifa za madai hayo na baadaye itatolewa taarifa rasmi.
"Tumeliona hili tangazo kwamba kuna mwanafunzi ambaye nafasi yake imechukuliwa kwenye shule aliyopangiwa, tumeshaifanyia kazi na kazi yenyewe ni kama tumeshaimaliza tutaitolea taarifa rasmi," amesema.
"Napenda kuwahakikishia Watanzania kwamba timu zetu kwa kushirikiana na Tamisemi tumeshalifuatilia vizuri tumekusanya taarifa zote baadaye tutatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu taarifa za huyu binti kwamba alitakiwa aende sekondari lakini nafasi yake ilichukuliwa na watu, kwa hiyo taarifa hii inaweza kutolewa kesho," amesema Profesa Mkenda.