Tamisemi: Hakuna mwanafunzi aliyenyang'anywa haki yake

Muktasari:
- Serikali kupitia ofisi ya Rais-Tamisemi imesema hakuna mwanafunzi aliyenyang'anywa haki yake ya kuendelea na kidato cha tano katika shule ya Sekondari Namwai iliyopo Wilaya ya Siha na kwamba taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuhusisha mwanafunzi Sifika Daniel Reuben kwamba nafasi yake ilichukuliwa na mtu mwingine sio za kweli.
Moshi. Baada ya kusambaa mitandaoni kwa taarifa inayomuhusu mwanafunzi Sifika Rubern ambaye aliyedaiwa kunyang’anywa haki ya kuendelea na masomo na nafasi yake kupewa mwanafunzi mwingine, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imejibu tuhuma hizo ikisema sio za kweli na kwamba zipuuzwe.
Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Tamisemi, Nteghenjwa Hosseah, imesema wamefuatilia taarifa hizo kwa kina kutoka Shule ya Sekondari Mkombozi alikosoma (O’level), mpaka Shule ya Sekondari Namwai anakodaiwa kupangiwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na kubani kuwa anayelalamika mitandoni anaitwa Sifaeli Tawel Elirehema.
Taarifa imeeleza kuwa Sifaeli alisoma shule moja na Sifika Daniel Rubern, hata hivyo binti huyo (Sifaeli) namba yake ya mtihani ilikuwa ni S.850/135 alipata Div IV: 34 (Zero) na kwamba alisoma masomo ya sanaa, ilihali Sifika namba yake ya mtihani ni S.850/136 na alisoma masomo ya sayansi na katika mtihani wake wa kidato cha nne, alipata Division 1:10.
“Binti anayelalamika mitandaoni alifikishwa shuleni hapo na wazazi/walezi kuripoti akiwa hana viambatanisho vyovyote na alipohojiwa ilibainika kuwa amewadanganya walezi wake kuanzia jina mpaka matokeo yake,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;
“Na kwa sababu walimchukua kama msaidizi wa nyumbani, hawakufahamu ukweli wa taarifa walizopewa na binti huyo, hakuna aliyenyang’anywa haki yake ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na taarifa zilizotolewa na binti huyo ni za uongo na zipuuzwe na mwanafunzi Sifika Daniel Ruben anaendelea na masomo yake” imesema taarifa hiyo.