Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haki Elimu kumsomesha msichana pekee aliyefaulu sekondari Mpwapwa

Muktasari:

  • Katika jitihada za kuhakikisha idadi ya wanawake wasomi inaongezeka nchini, Shirika la HakiElimu limeahidi kumlipia gharama zote za ada, Mariam Malangusi ambaye ni mwanafunzi pekee aliyefanikiwa kupata daraja la kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari Ving’hawe iliyopo Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.


Dar es Salaam. Katika jitihada za kuhakikisha idadi ya wanawake wasomi inaongezeka nchini, Shirika la HakiElimu limeahidi kumlipia gharama zote za ada, Mariam Malangusi ambaye ni mwanafunzi pekee aliyefanikiwa kupata daraja la kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari Ving’hawe iliyopo Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Licha ya kupitia changamoto kubwa za maisha, Malangusi alifanikiwa kupata daraja la kwanza la alama 11 na sasa anasubiri kupangiwa shule ya kujiunga kidato cha tano huku ndoto zake zikiwa ni kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati.

Akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo na kupata ushuhuda kutoka kwa mkuu wa shule hiyo Mwalimu Daud Elias, Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk John Kalage amesema amefikia uamuzi huo ili iwe chachu na hamasa kwa mabinti wengine kuendelea kufanya vizuri katika masomo yao.

Dk Kalage alisema amefurahi sana alipotembelea shule hiyo na kusikia shule imepata mwanafunzi aliyefaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza.

“Sasa huyu binti nataka niahidi leo kwamba, Haki Elimu litakulipia ada yako yote katika miaka miwili utakayosoma ‘A level’ kwa kuwa mfano bora kwa watoto ambao wanafanya vizuri, “

“Najua A level kuna ada, kule chini serikali imeondoa lakini kule juu unapaswa kulipa ada.  tutawasiliana, na tutaangalia mambo mengine ambayo tunaweza kuyafanya kwako wewe ili iwe mfano kwa watoto wengine wa kike kwamba kumbe ukijitahid kufanya vizuri unaweza ukaonekana na ukapata fursa nyingie zaidi,” amesema Dk Kalage.

Amesema kuwa binti huyo ni mfano mzuri kuwa watoto wa kike wanaopewa mazingira mazuri ya kusoma.

Kalage ameongeza kuwa binti huyo ni zao la vilabu vinavyojulikana kama Vinara vilivyopo kwenye shule takribani 127 Tanzania bara vikiwa vinaasisiwa na shirika hilo zikiwa na lengo la kusaidia wanafunzi wa kike kufanya vizuri katika sekta ya elimu.

Ameongezea kuwa mbali na kuanzisha vilabu hivyo vilevile shirika hilo kwa kushirikiana na wananchi limeweza kukamlisha mradi wa choo cha kike cha kisasa chenye chumba maalumu kwaajili ya kujisitiri wanafunzi wa kike pamoja na mradi wa maji kwenye shule ya msingi Idilo.