Matumaini mapya CCM ikipanga kuja na chombo huru cha uchunguzi wa uhalifu

Muktasari:
- Katika ilani yake ya uchaguzi mwaka 2025 - 2030, CCM imepanga kuanzisha Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (NBI), chombo huru cha kuchunguza uhalifu, ili kuboresha utoaji wa haki. Mamlaka hiyo mpya itakuwa nje ya mfumo wa sasa wa polisi na inalenga kuimarisha uwajibikaji, kuondoa ushawishi wa kisiasa katika uchunguzi wa makosa ya jinai, na kuongeza imani ya umma.
Dar es Salaam. Mabadiliko makubwa katika mfumo wa haki jinai yanaweza kutokea nchini Tanzania ikiwa pendekezo la Chama cha Mapinduzi (CCM) la kuanzisha mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea (NBI), litatimia.
Ikumbukwe Mei 30, 2025, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alizindua Ilani ya uchaguzi ya chama hicho itakayotekelezwa kwa miaka mitano ijayo, yaani 2025 hadi 2030.
Kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni miongoni mwa yaliyoandikwa ambayo CCM inasema itachukua hatua katika utekelezaji wake, ambapo pamoja na mambo mengine, lengo ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua hali za maisha ya Watanzania, kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu katika nchi, na kudumisha demokrasia na utawala bora.
Aidha, Ilani imesema itaboresha mishahara na maslahi ya askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, na Uhamiaji, ikiwamo kupitia upya umri wa kustaafu na mafao ya pensheni.
Pendekezo hilo lililobainishwa kwenye Ilani linatoa wito wa kuanzishwa kwa mamlaka huru kuchukua jukumu la uchunguzi wa uhalifu unaoshughulikiwa sasa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ikiwa chini ya Jeshi la Polisi Tanzania.
"Kuanzisha mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (National Bureau of Investigation), itakayokuwa na jukumu la kupeleleza makosa yote ya jinai," imeandikwa katika ukurasa wa 33 wa Ilani hiyo.
Hata hivyo, wachambuzi wanaamini hatua hiyo inaweza kubadilisha utoaji wa haki, huku wakifafanua upya jukumu la polisi.
Katika mazungumzo ya hivi karibuni ya Café Talk, mwanachama mwandamizi wa CCM na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa chama hicho, Ally Hapi, alieleza kuwa kwa sasa, uchunguzi wa jinai unafanywa ndani ya polisi, ambapo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wote wanafanya kazi chini ya safu moja ya amri.
"Tunakusudia kutenganisha majukumu haya kwa kuunda wakala huru wa uchunguzi wenye bajeti yake, wenye uwezo wa kufanya kazi bila kuingiliwa, sawa na jinsi Ofisi ya Upelelezi ya Shirikisho ya Marekani (FBI) inavyofanya kazi," alisema Hapi.
Hata hivyo, wataalamu wa sheria wanasema bado yanahitajika mabadiliko makubwa katika mfumo wa haki jinai nchini, ingawa baadhi ya watu wanaona pendekezo la NBI kama hatua chanya ya kuiweka pazuri sekta ya uchunguzi.
Akiungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Julai 8, 2025, Kamanda wa Polisi mstaafu, Alhaj Jamal Rwambow, amesema katika Tume ya Haki Jinai ya Jaji mstaafu Mohamed Chande Othman, suala la taasisi huru ya upelelezi ni moja ya masuala yaliyokuwa yakizungumziwa, kwa hiyo Ilani inavyokuja na suala hilo hilo, ni jambo zuri kulingana na uhitaji wake.
Kuhusu rasilimali watu, amesema wako wa kutosha na wa aina nyingi katika utekelezaji wa majukumu hayo ya kipelelezi na kuunda chombo hicho.
"Kwangu mimi ni jambo zuri kwa sababu limeshapigiwa kelele na wadau mbalimbali, ikiwemo wananchi wenyewe kwa muda mrefu," amesema.
Kamanda huyo mstaafu amesema kama nchi haijachelewa kwa kuwa imekuja kwa wakati na hakuna haja ya kusema imechelewa, hata mchakato wa kuonyesha kwamba kuna haja ya kuwa na chombo kama hiki ni hatua nzuri ukilinganisha na mahitaji ya sasa.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen kwa njia ya simu, aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia, amelikaribisha pendekezo hilo akisema ni zuri ingawa limechelewa.
"Tumechelewa kuanzisha NBI. Kuna mageuzi mengine mengi yanayohitajika ndani ya mfumo wa haki jinai, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Haki Jinai chini ya Jaji Chande, hili ni moja tu kati yao. Ni tiba ya awali, lakini maradhi ni mengi," ameiambia The Citizen.
Sungusia amesema mfumo wa haki jinai unajumuisha sehemu 11 zilizounganishwa, kuanzia kudhibiti na kugundua uhalifu hadi kuunganisha tena wahalifu na kuzuia kurudia makosa.
"Ikiwa sehemu moja katika mnyororo ni dhaifu, mfumo mzima huathirika," amesema. Miongoni mwa mapendekezo yake, Sungusia amesisitiza umuhimu wa kubadilisha Jeshi la Polisi kutoka muundo wake wa zama za ukoloni na kuwa huduma inayozingatia jamii.
Amesema jeshi hilo inabidi kushushwa na kuliweka chini ya Serikali za mitaa ili kuunda polisi wa wananchi wanaolingana zaidi na mipango ya manispaa na utoaji wa huduma.
Pia, ametoa wito wa kuunda chombo huru cha uangalizi wa polisi, kama ilivyo nchini Kenya na Afrika Kusini, ili kutoa uwajibikaji na kushughulikia utovu wa nidhamu ndani ya jeshi.
Kwa kuongezea, Sungusia amesema anaamini mageuzi lazima yalingane na taasisi zilizopo. Kwa maoni yake, NBI ingepaswa kuundwa sambamba na Huduma ya Taifa ya Mashtaka (NPS), ambayo hufanya kazi chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
Amesema mfumo huo utafanana na ule wa Uingereza, ambapo Shirika la Kitaifa la Uhalifu hufanya kazi sambamba na Huduma ya Mashtaka ya Crown ili kuhakikisha mashtaka huru na yenye ufanisi.
"Ninaamini NBI imechelewa kwa sababu ingepaswa kuletwa sambamba na NPS.
"Pendekezo hili linakuja baada ya miaka mingi ya malalamiko kutoka mashirika ya kiraia na vikundi vya upinzani, ambao wanadai kuwa uchunguzi wa polisi wakati mwingine huathiriwa na ushawishi wa kisiasa," amesema.
Maswali muhimu
Hata hivyo, maswali muhimu yanabaki kuhusu namna ofisi hiyo itakavyofanya kazi. Haijulikani kama NBI itaanzishwa kupitia sheria maalumu ya Bunge na kama mamlaka yake yatapunguzwa kwa uhalifu mkubwa kama rushwa, ugaidi na uhalifu uliopangwa, au kama pia itahusisha uchunguzi wa kawaida wa uhalifu.
Wasiwasi pia upo juu ya kama nchi ina rasilimali na utaalamu unaohitajika kuajiri na kuendesha wakala wa uchunguzi wenye kiwango cha juu.
Kuna sintofahamu zaidi kuhusu jinsi majukumu ya ofisi hiyo yataundwa ili kuepuka mwingiliano na huduma zilizopo za polisi na mashtaka.
Ofisa wa Polisi, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema wanaunga mkono mageuzi ya kimsingi yaliyokusudiwa, lakini akaonya kuwa mamlaka yanayoingiliana yanaweza kusababisha vita vya kitaasisi.
"Kuna hatari ya kuchanganyikiwa isipokuwa sheria itaeleza wazi nani anafanya nini," amesema ofisa mmoja mwandamizi katika Jeshi la Polisi.
Nchi kama Kenya, ambayo ina Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai chini ya huduma yake ya Kitaifa ya Polisi, na Marekani, ambapo FBI inafanya kazi kwa kujitegemea, zinatoa mifano ambayo Tanzania inaweza kujifunza.
Matarajio ya umma
Baadhi ya wananchi katika mitaa ya Dar es Salaam wameonyesha matumaini huku wakitarajia NBI inaweza kuleta uchunguzi wa haraka na wa kuaminika zaidi, hasa katika kesi za rushwa na zenye hadhi ya juu.
"Mara nyingi tunasikia kwamba kesi zinakwama kwa sababu ya ushawishi wa kisiasa. Labda chombo huru kinaweza kufanya kazi bila hofu," mfanyabiashara, Rashid Juma, ameiambia The Citizen.
Wengine, hata hivyo, wameonyesha wasiwasi juu ya gharama na kama mamlaka hiyo mpya inaweza kuakisi tu upungufu wa taasisi zilizopo.
Kwa wengi, swali kuu linabaki: je, mamlaka hiyo mpya inaweza kutoa uhuru na uadilifu ambao Watanzania wamekuwa wakidai kwa muda mrefu kutoka kwenye mfumo wao wa haki jinai?