Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheikh Walid, wenzake waundiwa tume ya uchunguzi

Muktasari:

  • Tume hiyo  yenye jopo la watu sita imepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kina ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuwasilisha taarifa yake kwa Mufti wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ali.

Dar es Salaam. Hatimaye Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeunda tume ya watu sita kuchunguza tuhuma zinazowakabili masheikh watatu waliosimamishwa kwa madai ya kuwa na mwenendo unaokiuka misingi ya uongozi wa baraza hilo.

Masheikh hao ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar, Sheikh wa Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassor Issa, na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Idi Kiburwa. Masheikh hao walisimamishwa Julai 14, 2026, kufuatia kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa.

Tume hiyo imepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kina ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuwasilisha taarifa yake kwa Mufti wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ali.

Wajumbe wanaounda tume hiyo inayotajwa inaenda kutafuta haki ni Sheikh Shaban Juma Abdallah, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, ambaye ndiye Mwenyekiti wa tume; Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mussa Hans; Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Dk Abdallah Tego; Wakili Ummi Azizi Kheri; Mkurugenzi wa Elimu Bakwata, Mwalimu Ally Abdallah; na Hamis Kalimwage, ambaye ni mjumbe wa kamati ya utatuzi wa migogoro ya misikiti na madrasa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Ulamaa kilichofanyika leo, Julai 21, 2026, Katibu wa Baraza hilo, Sheikh Hassan Saidi Chizenga, amesema uamuzi wa kuunda tume hiyo ulifikiwa katika kikao kilichoongozwa na Mufti wa Tanzania.

Amesema Mufti wa Tanzania, baada ya kushauriana na Baraza la Ulamaa na kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 84(17) ya Katiba ya Bakwata ya mwaka 1999, toleo la mwaka 2018, aliunda tume hiyo kwa ajili ya kuchunguza tuhuma zote zinazowakabili masheikh hao watatu.

"Tume imepewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha taarifa kwa Mufti wa Tanzania," amesema Sheikh Chizenga.

Sheikh Chizenga amewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu wakati tume hiyo ikiendelea na kazi yake. Pia aliwasihi watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kuziwasilisha kwa tume, huku akiwataka wote watakaoitwa kutoa ushirikiano ili uchunguzi huo ufanyike kwa ufanisi.

"Tunawaomba wote watakaohitajika na tume katika kukusanya taarifa muhimu watoe ushirikiano ili kufanikisha malengo ya tume hii, ambayo ni kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote," amesema.