Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shehena ya kemikali bashirifu yazuiwa kuingia Tanzania

Muktasari:

  • Kemikali zilizozuiwa ni kilo 4,000 za 1-Boc-4-piperidone na kilo 10,000 za Acetic anhydride ambazo zikichepushwa hutumika kutengeneza dawa za kulevya.

Dar es Salaam. Kilo 14,000 za kemikali bashirifu zinazotumika katika utafiti na utengenezaji wa dawa kutoka barani Asia, zimezuiwa kuingia nchini kutokana na kukosekana vielelezo kuonyesha matumizi yake.

Kemikali hizo ni kilo 4,000 za 1-Boc-4-piperidone na kilo 10,000 za Acetic anhydride ambazo zikichepushwa hutumika kutengeneza dawa za kulevya.

Uzuiaji huo umefanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (INCB).

Baada ya wahusika wa kemikali hizo kukamatwa na kuhojiwa walieleza zilikuwa zinapelekwa wilayani Igunga, mkoani Tabora walikotaka kuanzisha maabara bubu ya kutengeneza dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2025 Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema majaribio mengi ya uingizaji wa kemikali bashirifu yamekuwa yakifanyika lengo likiwa kutengeneza dawa za kulevya za viwandani, ambazo upatikanaji wake nchini umepungua kwa kiasi kikubwa.

Amesema endapo kemikali hizo zingeingia kwenye mzunguko zingetumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya fentanyl na heroini.

“Hii ina maana kuwa, kiasi cha kilo 10,000 za acetic anhydride kilichozuiwa kingeweza kutumika kutengeneza kilo 3,704 za heroini, wakati kilo 4,000 za 1-Boc-4-piperidone kingeweza kutengeneza kilo 8,000 za dawa za kulevya aina ya fentanyl.

“Pia kemikali hiyo inaweza kutumika kuzalisha kemikali nyingine bashirifu ambazo zinaweza kutumika kuzalisha dawa za kulevya za mandrax na methamphetamine,” amesema.

Amesema matumizi ya kiasi hicho cha fentanyl ambazo zingezalishwa zingeweza kusababisha vifo kwa watumiaji bilioni nne, ikizingatiwa kuwa kilo moja ya dawa hizo inaweza kusababisha vifo kwa watu 500,000 kutegemea uzito, afya na historia ya mtumiaji. Inakadiriwa miligramu mbili zinaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja.

Lyimo amesema uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa unaendelea kubaini mitandao zaidi ya usafirishaji haramu wa kemikali bashirifu zinazoweza kuchepushwa na kutengeneza dawa za kulevya.


Pipi zenye sumu

Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imemkamata raia wa Uganda, Herbert Kawalya akiwa na pakiti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa dawa za kulevya aina ya bangi, yenye kiwango kikubwa cha sumu ya tetrahydrocannabinol (THC).

Kawalya, mmiliki wa kampuni ya Hoxx Wells Lux Tour Limo, alikamatwa pamoja na gari aina ya Mercedes Benz lililokuwa likisafirisha pipi hizo kuingia nchini kutokea Afrika Kusini.

“Mfanyabiashara huyu tulipomuhoji alisema hii ni mara yake ya kwanza, ndiyo alikuwa anajaribu kuingiza pipi hizi kuona kama atapata biashara. Mpango wake ni kwenda kuziuza kwenye hoteli, tunaendelea kulifanyia kazi hili kubaini ukubwa wake.

“Utengenezaji wa pipi hizi zenye kiwango kikubwa cha sumu aina ya THC ni ushahidi wa nia ovu ya wahalifu kulenga kuharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa. THC iliyopo kwenye pipi hizi ni asilimia 92, hatujawahi kushuhudia kiwango kikubwa hivi, skanka ina THC asilimia 40 hadi 60, bangi ya kawaida ni asilimia 10 hadi 13,” amesema.

Lyimo amesema mamlaka imebaini kuendelea kuingizwa, kusafirishwa na kulimwa dawa za kulevya nchini ni matokeo ya kuwapo mianya ya rushwa kwa watendaji wanaopaswa kuzuia dawa hizo haramu zisiingie kwenye jamii.

Amesema: “Tunafanya operesheni kadhaa lakini bado tunakuta mashamba ya bangi, kemikali bashirifu na dawa za kulevya za viwandani. Hii inamaanisha kwamba, kuna rushwa inaendelea kwa sababu hizi dawa zinapitaje kama wahusika wote wanaopaswa kudhibiti wangefanya kazi yao ipasavyo.

“Kuanzia sasa tumekubaliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nao waingie ili kuwashughulikia watumishi, watendaji na wasimamizi katika maeneo yote ambayo dawa hizi itabainika zimepita, hili litawagusa pia viongozi wa vijiji na mitaa ambayo kuna mashamba ya bangi na viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya.”

Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Uchunguzi Takukuru, Thobias Ndaro amewaonya watumishi wa umma ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya katika kufanikisha biashara zao.

“Tunafahamu wanaofanya biashara hutumia fedha nyingi kuhakikisha mambo yao yanakwenda, sasa wewe mtumishi wa umma ukiingia kwenye huu mnyororo hauwezi kuwa salama, tumekubaliana na DCEA tusimame imara kukomesha biashara hii.

“Kwa ushirikiano huu hakuna yeyote atakayehusika kwenye biashara hii akabaki salama, mzigo ukikamatwa tutafuatilia mnyororo mzima na kama ulipita katika eneo lako la kazi ni lazima uwajibike kutueleza ulipitaje,” amesema.