Shahidi aeleza namna watuhumiwa kesi ya Milembe walivyokamatwa

Aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML), Milembe Suleman wakati wa uhai wake.
Muktasari:
- Baada ya kumkamata Dayfath alimtaja Safari Lubingo (mshtakiwa wa pili) waliyesuka naye mpango wa kumuua Milembe ambaye baada ya kumkamata alielekeza alipo Musa Libingo (mshtakiwa wa nne) ambaye naye alieleza aliko Genja Pastory (mshtakiwa wa tatu).
Geita. Shahidi wa 24 katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa GGMl, Milembe Suleman (43) aliyeuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini wake, ameieleza Mahakama namna walivyowakamata washtakiwa wanne wa kesi hiyo.
Shahidi huyo, Coplo Hashimu ambaye ni askari upelelezi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Geita, ameieleza Mahakama kuwa Mei Mosi, 2023 akiwa na timu ya kikosi kazi walienda Mwanza kwa ajili ya ufuatiliaji wa tukio la mauaji ya Milembe.
Amedai siku hiyohiyo walifika nyumbani kwa Milembe eneo la Usagara jijini Mwanza na kumkamata Dayfath Maunga (mshtakiwa wa kwanza) na mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Musa Fundikira na kuwapeleka kituo cha Polisi Nyamagana kwa mahojiano.
Amedai baada ya mahojiano, mshtakiwa wa kwanza aliwaeleza ili waweze kuwapata wauaji, wamtafute mtu aitwae Safari (mshtakiwa wa pili) kwa kuwa yeye ndiye aliyesuka naye mpango wa kumuua Milembe.
Kufuatia majibu ya Dayfath, timu ya kikosi kazi ilianza safari kurudi Geita na Mei 5, 2023 walifanikiwa kumkamata Safari Lubingo maeneo ya Butundwe wilayani Geita na aliwatajia alipokuwa mshtakiwa wa nne, Musa Lubingo.
Akiongozwa na mwendesha Mashtaka wa Serikali, Merito Ukongoji, shahidi huyo ameeleza baada ya kumpata Safari aliwasaidia kumpata Musa aliyekuwa Wilayani Kahama maeneo ya Bulyanhulu na aliwaeleza aliko mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory.
“Tulikwenda Bulyanhulu na kumkamata Musa ambaye naye tulipomuhoji alitaja washiriki wengine wanaopatikana Sengerema na kwa kuwa alikuwa eneo lenye watu tuliona tukitoka Buliyanhulu kwenda Sengerema tutachelewa na kufanya mawasiliano na askari wa Sengerema ili wamkamate Genja.”
“Baada ya hapo tulirudi Geita tukiwa na Safari na Musa na usiku huohuo tulipata taarifa kuwa mtuhumiwa Genja amekamatwa na Mei 6,2023 alisafirishwa kuja Geita,” amedai Hashimu.
Ameeleza baada ya Genja (mshtakiwa wa tatu) kufika alipewa maelekezo ya kumchukua alama ya vidole ili kufanya ulinganisho na vilivyopatikana kwenye chupa ya soda iliyokutwa eneo la tukio.
Shahidi wa 25 wa upande wa mashitaka, Simon Komela ambaye ni balozi wa eneo la Mwatulole ziliko nyumba za Milembe, amedai Mei 6, 2023 alipigiwa simu na mwenyekiti wa mtaa wa Mwatulole akimtaka afike zilipo nyumba za Milembe.
Amedai baada ya kufika alikutana na askari polisi wakiwa na mtuhumiwa aliyefungwa pingu na baada ya utambulisho, polisi alimuhoji mtuhumiwa iliko silaha waliyoitumia kumuua Milembe.
“Alipohojiwa alidai ipo karibu na mti kando ya barabara na akatuongoza hadi kwenye mti na kuonyesha alikoficha na polisi kuanza kupekua nyasi baadaye wakaona jambia lenye ncha kali na kuchukua sampuli ya vilivyopatikana kwenye jambia kisha kuondoka kurudi kituoni,” amedai Komela.
Juni 7, 2023 saa nne asubuhi, shahidi huyo alipigiwa tena simu na mwenyekiti akimueleza kazi waliyofanya jana yake haijaisha na kumtaka waongozane hadi kwenye nyumba za Milembe na kuwakuta askari wakiwa na mtuhumiwa Genja Pastor wakimuhoji zilipo simu za marehemu.
Mshtakiwa huyo aliwapeleka hadi ng’ambo ya barabara kwenye nyumba yenye choo nje na kudai alitumbukiza simu hizo kwenye choo na baada ya hapo wazamiaji waliingia ndani ya choo na kutoka na simu mbili na kuzikabidhi kwa polisi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka moja la kumuua Milembe Seleman.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti anayemtetea mshtakiwa wa pili, Elizabeth Msechu anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Erick Lutehanga na Yesse Lubanda anayemtetea mshtakiwa wa tano.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Juni 26 itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi.