Mahakama yapokea vielelezo vitatu ushahidi kesi ya Milembe wa GGML

Aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML), Milembe Suleman wakati wa uhai wake.
Muktasari:
- Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Juni 25, 2024 itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi na hadi sasa mashahidi 22 kati ya 32 wa upande wa mashtaka ndio waliotoa ushahidi wao.
Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita, imepokea vielelezo vitatu vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauji ya Milembe Suleman, aliyeuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Milembe (43) aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi katika Kampuni ya GGML, aliuawa usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani, usoni na mikononi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Seleman.
Katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina.
Vielelezo vilivyopokelewa ni pamoja na ramani ya eneo la tukio la mauji ya Milembe iliyopokelewa kama kielelezo cha ushahidi namba 14, kielelezo kingine ni hati ya kupokea sampuli za damu zilizokuwa kwenye jambia lililotumika kumuulia lililopokelewa kama kielelezo cha ushahidi namba 15 upande wa mashtaka.
Kielelezo kingine ni fomu ya sampuli ya vinasaba (DNA) ya mate ya mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory kilichopokelewa kama kielelezo cha 16 cha ushahid upande wa mashtaka.
Leo Juni 24, 2024, mashahidi wanne wametoa ushahidi wao mbele ya Jaji Mhina wakiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Wakili Merito Ukongoji akisaidiana na Grace Kabu.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Liberatus John (mshtakiwa wa kwanza), Laurent Bugoti anayemtetea mshtakiwa wa pili, Elizabeth Msechu anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Erick Lutehanga na Yesse Lubanda anayemtetea mshtakiwa wa tano.
Akitoa ushahidi wake, shahidi wa 19 ambaye ni askari kutoka kitengo cha upelelezi Geita,
Martine Biabusha ameieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyechora ramani ya eneo mauaji yalipotokea huko Mwatulole ambako Milembe alikuwa akijenga nyumba zake.
Shahidi wa 20, Sadock Mboya ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, amethibitisha kupokea sampuli za damu kutoka kwa askari Timo aliyechukua damu kwenye jambia lililotumika kumuua Milembe.
Shahidi mwingine, Zachia ameieleza Mahakama kuwa yeye ndiye aliyehusika kumkamata mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Dayfath Maunga kutoka nyumbani kwa Milembe eneo la Usagara jijini Mwanza na kumpeleka kituo cha Polisi Nyamagana.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Salala Bihemo ameieleza Mahakama kuwa Mei 7, 2023, alimchukua sampuli za vinasaba (DNA) za mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory kwa mujibu wa sheria ya DNA namba nane ya mwaka 2009.
Amedai kuwa baada ya mshatakiwa huyo kuonyesha alikoficha jambia alilotumia kumuua Milembe, zilichukuliwa sampuli za damu na mate kwa ajili ya uchunguzi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Juni 25, 2024 itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kuendelea na ushahidi na hadi sasa mashahidi 22 kati ya 32 wa upande wa mashtaka ndio waliotoa ushahidi wao.