Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh661 bilioni zapigwa kwa stakabadhi za kughushi

Muktasari:

Matokeo ya uchunguzi na ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA) mwaka 2022/23, yameonyesha bidhaa zenye thamani ya Sh661.68 bilioni zilinunuliwa kwa stakabadhi za kughushi.



Dodoma. Matokeo ya uchunguzi na ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA) mwaka 2022/23, yameonyesha bidhaa zenye thamani ya Sh661.68 bilioni zilinunuliwa kwa stakabadhi za kughushi.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dk Leonada Mwagike alisema hayo jana, alipokabidhi ripoti ya tathimini ya utendaji ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande.


Dk Leonada alisema kati ya taasisi 180 zilizokaguliwa na PPRA, 28 zilikuwa na matokeo ya kuridhisha, 109 zilikuwa na matokeo ya wastani na 43 zilikuwa na matokeo hafifu.


Alisema kati ya taasisi 43 zilizopata matokeo hafifu, 28 zilikuwa kwenye kundi la tawala za mikoa na Serikali za mitaa, nane ni mashirika ya umma, na saba zikiwa ni wizara, idara za Serikali zinazojitegemea na wakala wa Serikali.


“Katika mwaka wa fedha 2022/23, mamlaka ilifanya uchunguzi na ukaguzi maalumu kwa taasisi 12 na matokeo yanaonyesha Serikali ilipata hasara ya Sh8.77 bilioni kutokana na ukosefu wa uwajibikaji, ufanisi, uwazi na uadilifu kwenye taasisi zilizokaguliwa na kuchunguzwa,” alisema.


Dk Leonada alisema matokeo ya ukaguzi na uchunguzi maalumu ni pamoja na kuokoa kutoa zabuni zenye thamani ya Sh485 bilioni kwa wazabuni wasio na sifa. Pia kumebainika tathimini isiyo ya haki ya zabuni zenye thamani ya Sh366.07 bilioni.


Matokeo mengine ni kutokuwapo ushindani katika ununuzi wa umma wenye thamani ya Sh209.98 bilioni na ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Sh5.07 bilioni bila kuomba stakabadhi za kielektroniki (EFD).
Mengine ni ununuzi wa bidhaa wenye thamani ya Sh661.68 bilioni kwa stakabadhi za kughushi na usimamizi mbovu wa mikataba ya ujenzi yenye thamani ya Sh8.8 bilioni, uliosababishwa na kuchelewa na kutokamilika kwa miradi.


Alisema Serikali iliokoa fedha zenye thamani ya Sh2.26 bilioni kutokana na kurejeshwa kwa malipo ya awali, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kuzuiwa kwa malipo yaliyokiuka utekelezaji wa mikataba.


Dk Leonada alisema katika kushughulikia hayo, mamlaka ilitoa mapendekezo kadhaa kwa taasisi nunuzi husika, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika na manunuzi.


Pia, walishauri kufanya maboresho katika michakato ya manunuzi kutokana na upungufu uliobainishwa kwa lengo la kuongeza uwazi na ufanisi katika ununuzi wa umma.

Alichosema Chande
Chande aliziagiza taasisi nunuzi zote kuhakikisha zinafanya ununuzi wa umma kupitia mfumo mpya wa ununuzi wa NeST kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu.


Alisema atakayekwepa kutumia mfumo huo anamaanisha ana nia ovu, na kwamba Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kufanya ubadhirifu.


“Naagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote watakaokiuka maelekezo haya. Katibu Mkuu Hazina na Mlipaji Mkuu wa Serikali, nakuelekeza kuwa hili ulisimamie na kulifuatilia kwa karibu mno,” aliagiza.
Kuhusu hasara iliyopatikana, Chande aliagiza vyombo vinavyoshughulika na jinai, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchukua hatua stahiki kwa taasisi zote zilizokiuka sheria, kanuni na miongozo.


Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliackim Maswi alisema katika ripoti hiyo, taasisi 132 kati 864 hazikutumia mfumo wa ununuzi wa TANePS.
“Kwa mujibu wa Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma uliopitishwa na Bunge, suala la kutumia mfumo wa manunuzi halitakuwa la hiari bali ni lazima, usipotumia maana yake utawajibika kutokana na sheria na taratibu zilizowekwa,” alisema.