Sh500 milioni zatumika kuondoa adha ya daraja Marangu Mtoni

Muktasari:
- Daraja hilo limekuwa likitumiwa na mamia ya watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu pamoja na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao mbalimbali kutoka vijijini kwenda mjini Moshi na maeneo mengine, ambalo limegharimu zaidi ya Sh500 milioni.
Moshi. Wananchi wa Kijiji cha Arisi, Kata ya Marangu Mashariki, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja la kisasa katika eneo la Marangu Mtoni, lililogharimu zaidi ya Sh500 milioni, hatua iliyowaondolea adha ya usafiri na ajali za mara kwa mara zilizokuwa zikijitokeza nyakati za mvua.
Daraja hilo linaunganisha barabara ya kuelekea lango la Marangu katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) na maeneo mengine ya uchumi, likitumika na watalii, wakulima na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao kwenda mjini Moshi.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Kijiji cha Arisi, Heriel Naiman alisema daraja hilo ambalo awali lilijengwa kwa mbao mwaka 1960, lilikuwa bovu na nyembamba kiasi cha kushindwa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja.
“Kwa miaka yote hiyo tumeteseka. Magari yalikuwa hayawezi kupishana, na ajali zilikuwa ni jambo la kawaida. Tunaishukuru Serikali kwa kutujengea daraja imara na salama. Sasa magari yanapita bila tatizo,” amesema Naiman.
Naiman aliongeza kuwa, kupitia ushirikiano wa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei, wananchi wa eneo hilo wameondolewa adha iliyodumu kwa zaidi ya miaka 60.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Thomas Chonjo alisema daraja hilo ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kivutio cha utalii kwani linaunganisha barabara inayotumiwa na watalii kuelekea hifadhi ya Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu.
“Linaunganisha mamia ya wananchi wanaojishughulisha na biashara na kilimo. Tangu lijengwe hatujasikia ajali yoyote. Maisha yamekuwa bora zaidi,” amesema Chonjo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Marangu Mashariki, Jonas Mawala ameeleza kuwa jumla ya miradi 38 ya maendeleo imetekelezwa katika kata hiyo kwa kipindi cha miaka minne na nusu, ikiwemo daraja hilo lililojengwa kwa zaidi ya Sh500 milioni.
“Tunamshukuru Mbunge wetu kwa kushirikiana na Serikali kuleta fedha hizi. Daraja limekamilika na linapitika vizuri. Kata yetu imepata miradi mingi kutokana na jitihada hizi,” amesema Mawala.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei, Katibu wake Gulatone Masiga alisema kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne na nusu, Jimbo hilo limepokea zaidi ya Sh52 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Amesema pia kuwa Dk Kimei ametoa zaidi ya Sh325 milioni kwa shughuli za kijamii, zikiwemo misaada kwa wahitaji, wanafunzi, shughuli za kidini na kuwawezesha wananchi kiuchumi.