Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Padri aliyekufa ajalini kuzikwa Manyoni Septemba 17

Muktasari:

  • Mazishi ya Paroko wa Parokia ya Mkula Jimbo la Ifakara, Padri Nicolaus Ngowi aliyefariki dunia juzi katika ajali ya gari akienda Marangu mkoani Kilimanjaro, yatafanyika Septemba 17, 2024 wilayani Manyoni mkoani Singida.

Dodoma. Paroko wa Parokia ya Mkula, jimbo la Ifakara, mkoani Morogoro, Padri Nicolaus Ngowi aliyefariki dunia katika ajali ya gari juzi jioni atazikwa Jumatano ya Septemba 17, mwaka huu kwenye makaburi ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, yaliyopo Manyoni, mkoani Singida.

Padri Ngowi alifariki papo hapo, Septemba 9, 2024 katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kiruru Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari lake aina ya Toyota Prado alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Kilenga.

Padri Ngowi alikuwa akitokea Ifakara mkoani Morogoro akielekea nyumbani kwao Marangu mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuhudhuria shughuli ya kifamilia iliyokuwa ifanyike Jumanne Septemba 10, 2024.

Akizungumza na Mwananchi leo jijini Dodoma, Mkuu wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Tanzania, Vedasto Ngowi amesema maziko ya padri huyo yatafanyika Jumanne Septemba 17, mwaka huu Manyoni mkoani Singida.

Amesema kabla ya kuelekea Manyoni, Jumatatu Septemba 16, 2024 asubuhi kutakuwa na Ibada ya kumuombea marehemu itakayofanyika Parokia ya Makomu, Marangu mkoani Kilimanjaro.

Amesema ibada hiyo itaanza saa 6:00 mchana na baadaye wataanza safari ya kwenda Manyoni mkoani Singida.

 “Jumanne, Septemba 17, misa ya mazishi itafanyika katika Parokia ya Manyoni kuanzia saa nne asubuhi. Baadaye maziko yatafanyika katika makaburi ya wamisionari wa shirika hilo,” amesema mkuu huyo wa shirika.

Padri Nicolaus alipata daraja la upadri mwaka 2004 na amefanya kazi zake za utume katika parokia za Boko, Kunduchi na Mtoni Mtongani za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Pia ametumikia Parokia za Itigi na Manyoni (Singida), Kondoa (Dodoma) na hadi umauti unamkuta alikuwa Paroko wa Parokia ya Mkula Jimbo Katoliki la Mahenge mkoani Morogoro.