Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh5 bilioni kutunza mazingira Bwawa Nyerere

Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, Lutengano Mwandambo akiwafafanulia jambo viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) waliotembelea mradi huo

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati, January Makamba amesema wizara yake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wametenga Sh5 bilioni kwa ajili ya kusaidia utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo vya maji na mito inayopeleka maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP).

Rufiji. Waziri wa Nishati, January Makamba amesema wizara yake kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wametenga Sh5 bilioni kwa ajili ya kusaidia utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo vya maji na mito inayotiririsha maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere (JNHPP).

Makamba ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Julai 12, 2023 katika ziara ya viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) walioutembelea mradi huo uliojengwa kwa zaidi ya Sh6.5 trilioni, na unatarajiwa kukamilika mwakani na kuzalisha megawati 2,115.

Waziri Makamba amesema wameamua kushiriki kwenye uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili bwawa hilo lisiathirike na shughuli za bindamu zinazofanywa kwenye vyanzo vya mito, pamoja na maeneo ambako mito hupita kabla ya kufikia kwenye bwawa hilo.

“Fedha hizi zitatumika kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ili watunze mazingira na wasichepushe maji, na hivyo kuliwezesha bwawa kudumu kwa zaidi ya miaka 80.

“Fedha hizi pia tutazitumia kugharimia shughuli mbadala za uzalishaji mali kwa watu ambao wataacha au kuzuia kuchepusha maji kwenda kwenye kilimo au shughuli nyingine zenye athari kwa mazingira na uzalishaji wa umeme kwenye bwawa letu,” amesema.

Waziri Makamba amesema fedha hizo zimetengwa katika bajeti iliyopitishwa siku chache zilizopita na Bunge na kiwango chake kitaongezekana mwaka ujao kulingana na mahitaji.

“Miaka ya nyuma hatukutenga fedha kwa lengo la kulinda mradi huu na kutoa elimu kwa Watanzania lakini sasa tumefanya hivyo kwakuwa ukame unaosababishwa na shughuli za kibindamu zitaathiri uzalishaji wa umeme kwenye bwawa letu,” amesema.

Waziri huyo mwenye dhamana nishati nchini amesema wakati mwingine nchi inapata ukame mdogo lakini athari zake kwenye uzalishaji umeme huwa kubwa kutokana na shughuli za kibindamu zinazofanyika kwenye mito na vyanzo vya maji hivyo wamedhamiria kushirikiana na wadau kutunza na kuyahifadhi mazingira.

Naye, Kaimu Mufti Mkuu, Ali Khamis Ngeruka ameiomba Serikali itoe elimu ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo.

Amesema kuna miradi mingi yenye faida kwa Watanzania inajengwa lakini kwa kuwa watu hawana elimu nayo wanaipinga hivyo ni vema wakaelimishwa

“Leo hii sisi tumeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye bwawa hili ambalo si tu litatufanya tuwe na umeme wa uhakika lakini pia litatufanya tuwe nao wa ziada, hizi ni fedha zetu tunapaswa kujivunia kwa hatua hii lakini ni lazima umma uelimishwe kwa kina,” amesema.

Amesema ziara hiyo imewafungua macho na kuona jitihada kubwa na nzuri zilizofanywa na Serikali hivyo Bwakata watakwenda kuwaelimisha waumini wao.

“Hapa ni lazima tuipe ‘bravo’ Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan, wamefanya jambo jema sana, tunawaunga mkono na tutakuwa mabalozi wazuri wa kuelezea hiki kilichofanyika hapa,” amesema Kaimu Mufti Mkuu Ngeruka.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Hanifa Karamagi, kutoka Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (Juwakita) amesema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania kwa kuwa ndiye mnufaika mkuu.

“Ni fahari kuona tumejenga mradi huu mkubwa kwa kutumia fedha zetu na utatuondoa kwenye matatizo ya uhaba wa umeme yanayotukabili mara kwa mara,” amesema.

Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Lutengano Mwandamo amesema hadi sasa mita za ujazo wa maji katika bwawa hilo limefikia 163.8 kutoka usawa wa bahari.