Serikali yawataka vijana kujitosa katika siasa

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe akizungumza wakati wa uzinduzi wa mdahalo wa nane wa vijana wa Afrika Mashariki unaofanyika Chuo cha Ardhi kilichopo jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Muktasari:
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe amesema vijana kwa nchi za Afrika Mashariki ni karibu asilimia 70 ambao ndio wa kushika mustakabali wa maendeleo ya jumuiya hiyo
Dar es Salaam. Serikali imewaasa vijana kushiriki moja kwa moja katika michakato ya siasa ikiwamo uchaguzi ili kuondokana na tabia ya kuwa mashujaa kwenye mitandao ya kijamii pekee.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 25, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati akizindua mdahalo wa vijana wa vyuo vikuu kutoka nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam.
Profesa Mdoe amesema idadi ya vijana kwa nchi za Afrika Mashariki ni karibu asilimia 70, hivyo wao ndio wa kushika mustakabali wa maendeleo ya Jumuiya.
"Na ili jumuiya iweze kutengemaa vizuri lazima kuwe na usalama pamoja na amani na suala hili liko katika siasa, hivyo tukiwa na demokrasia amani inapatikana,”amesema Profesa Mdoe.
"Nimewahusia wajadili vizuri katika hili ili wawe wanashiriki katika michakato ya siasa," amesema Profesa Mdoe katika mdahalo huo wenye mada kuu ya Utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kujenga umoja na usalama.
Amesema imeshazoeleka vijana kuzungumza kwenye mitandao ya kijamii, lakini hawashiriki kwenye masuala kama ya uchaguzi, hivyo wanapaswa kushiriki kuanzia kupeana hamasa na kutoa elimu juu ya mambo ya demokrasia.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi, Profesa Evaristo Liwa amesema masuala ya vijana yanapaswa kuzungumzwa na vijana, hivyo wamewapa uwanja wa kujadili mambo mbalimbali kwa ajili ya kuandaa kesho yao.
"Waache vijana waongee wajue wanataka kuelekea wapi na hapa kutakuwa na maazimio ambayo yatatokana na vijana wenyewe mfano suala la ajira maana yake nini na njia nyingine ni ipi, hivyo watakuja na majibu," amesema Profesa Liwa.
Ofisa Mwandamizi Idara ya Siasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, David Onen amesema midahalo hiyo imeanza tangu mwaka 2012 na mwaka huu unafanyikia Tanzania; ni mdahalo wa nane kuwakutanisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki.
Amesema jumuiya ina mipango ya kuangazia namna ya kupata mipango mizuri ya amani na usalama, hivyo katika mdahalo huo Jumuiya inategemea kupata mawazo na michango yao.
"Tunawanafunzi 42 katika mdahalo huu na tutapata kijana balozi wa amani na usalama wa jumuiya," amesema.
Balozi wa Uswizi nchini Tanzania, Didier Chassot amesema mkutano huo wa vijana kutoka nchi mbalimbali za EAC ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha mshikamano.
Amesema watapata maarifa katika masuala ya siasa, teknolojia, kijamii, pamoja usawa wa kijinsia.