Sababu zinazokwamisha vijana kuzifikia ndoto zatajwa

Muktasari:
- Vijana nchini watakiwa kujengewa uwezo ili kuishi katika misingi ya ndoto zao kwa ajili ya kujipanga na maisha ya baadaye kwa kutafuta taarifa sahihi kuhusiana na afya ya uzazi.
Dar es Salaam. Vijana wametakiwa kujengewa uwezo ili kuishi kwenye ndoto zao kwa kujipanga na maisha ya baadaye kwa kutafuta taarifa sahihi kuhusiana na afya ya uzazi ili waweze kuwa na maamuzi sahihi.
Kutokupata taarifa sahihi za afya ya uzazi ni moja ya changamoto inayokwamisha vijana kushindwa kufikia malengo yao kwa sababu wanafanya maamuzi ambayo wakati mwingine hayana uhakika.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Programu wa Afya ya Uzazi kwa Vijana kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Fatina Kiluvia na kushauri umuhimu wa vijana kupata taarifa sahihi ili waweze kujilinda na kujikinga dhidi ya maradhi na changamoto nyingine za maisha.
Kiluvia alikuwa akizungumza hayo wakati akiwahusia vijana kwenye kilele cha maadhimisho ya maonesho ya Amua Accelerator yaliyofanyika Dar es Salaam leo Januari 14, 2024 yakihudhuriwa na baadhi ya wasanii wa uchoraji.
Amesema zaidi ya asilimia 75 ya idadi ya watu nchini Tanzania ni wenye umri chini ya miaka 35 na sera ya maendeleo ya vijana inatambua vijana ni watu wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 35.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila ujauzito unahitajika na kila uzazi ni salama. Kijana akipata ujauzito katika umri sahihi, uzazi wake utakuwa salama na pia ataweza kutimiza malengo yake, asipate maradhi ya ngono, atamaliza elimu na atapata ajira,”amesema.
Amua Accelerator ni mradi unaosaidia wajasiriamali wanaochipukia kwa kufadhili mafunzo na ukuzaji wa ujuzi, uliopo chini ya Mpango Endelevu wa Vijana (SYP) na UNFPA na unatekelezwa na Sahara Ventures na mwaka huu umelenga kutoa elimu ya kina ya jinsia kwa kutumia ubunifu wa sanaa ya uchoraji.
Amesema washiriki wote kwenye mradi huo wanatambaliwa na shirika hilo pamoja na taasisi nyingine za Umoja wa Mataifa (UN) nchini na litakuwa dirisha la kuweza kupata fursa nyingi zaidi.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Maria Msigwa amesema elimu waliyopata ya ujinsia, afya ya kupitia mradi wa ubunifu kwenye sanaa ya uchoraji utamjenga.
“Kwenye upande wa sanaa ya uchoraji, mradi huu umeniwezesha kujiamini kwa sababu mimi nilikuwa nachora kama sehemu ya kujifurahisha tu na siyo kazi, mimi ni mfanyabiashara ndogondogo lakini nimesomea diploma ya uhifadhi mradi huu umeniongezea fursa,” amesema.
Amesema kwa sasa anajua anaweza kuwafikia vijana wengine kwa kutumia michoro nakusambaza elimu ya afya ya uzazi aliyoipata na anaweza akatumia kipaji chake kuongeza kipato.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema wanategemea kuona kuna wasanii wakubwa baadaye ambao chimbuko lao ni mradi wa Amua.