Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vigogo wa vyama wawapa somo vijana wanaotaka kufanya siasa

Muktasari:

  • Vijana  wanaohitaji kuingia huko wameshauriwa kujiendeleza kwenye fani zingine,  badala ya kutegemea shughuli za kisiasa pekee kama sehemu za kuwatoa kimaisha.

Dar es Salaam. Vijana nchini wameshauriwa  kujiendeleza na kuwekeza kwenye fani zingine,  badala ya kutegemea shughuli za kisiasa pekee kuwainua kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na viongozi tofauti wa kisiasa kwenye majadiliano yaliyoandaliwa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) yaliyokuwa yakiangazia  changamoto zinazowakabili vijana wa sasa kwenye siasa na uongozi na kujenga uelewa wa pamoja kati ya vizazi tofauti ili kuleta mabadiliko mazuri katika sera za nchi.

Katika majadiliano hayo baadhi ya viongozi walidai kuna wimbi kubwa la vijana wanaomaliza vyuo kuingia kwenye vyama vya siasa wakihitaji nafasi za uongozi kwa fikra kwamba watabadilisha maisha yao jambo ambalo ni tofauti na uhalisia wake.

Katika majadiliano hayo, Mwenyekiti wa (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amesema mtindo wa vijana kutegemea siasa,  kubadilisha maisha utasababisha wapoteze mwelekeo kimaisha.

 “Kama unasoma vumilia umalize hakikisha unakuwa na utaalamu fulani na unapoingia kwenye siasa usije ukawa unapoteza muda wako wote. Ni vizuri ukawa unafanya kwa muda lakini ukawa na sehemu nyingine unayoitegemea kuingiza kipato kuendesha maisha,” amesema.

Katika maelezo yake,  Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),amesema vijana wakisema waendeshe maisha yao kwa kutegemea siasa wanaweza kuwa na mwisho mbaya kimaisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic (UDP), John Cheyo amesema  litakuwa jambo rahisi kwa vijana kufilisika kimaisha kama watategemea siasa kubadilisha maisha yao.

“Siku hizi kuna tafsiri mbovu imeingia kichwani kwa vijana ukiingia kwenye siasa unakuwa tajiri, niwaambie wanaoonekana wana fedha wale ni wezi tu,” amesema.

Cheyo amebainisha kuwa vijana wanapaswa kuendeleza fikra za kusaidia watu na si kujinufaisha wao binafsi,  huku akieleza kwa mfumo wa chaguzi uliopo sasa usipokuwa na fedha hupati.

Amesema wakati yeye anaingia kwenye siasa,  shabaha yake ilikuwa kuwasaidia wakulima wa zao la pamba waliokuwa wanalazimishwa kupeleka kwenye vyama vya ushirika lakini walikuwa hawalipwi.

“Wengine hadi miaka mitano hawalipwi kuanzia hapo nilianza kuendesha kampeni kupigania haki ya wakulima kama huna fedha taslimu hupati pamba nilikuwa nawafundisha wananchi wangu kuongea kwenye kampeni zangu,” amesema.

Cheyo ameongeza ili kijana awe mwanasiasa mzuri,  lazima uwe na moyo wa kutaka kubadilisha mambo kwenye jamii yake kwanza huku akieleza hata alivyokuwa bungeni alisimamia maslahi ya wakulima zaidi. 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi-Bara, Joseph Selasini amewashauri vijana kutoingia kwenye siasa kama bendera ifuatavyo upepo kwa kuona mtu fulani kwa kuwa ana mafanikio hivyo ni rahisi hata wao wakiingia huko.

“Unapaswa kujipima ni wito wako huwezi kulazimisha kitu. Wote ni Waislamu lakini sheikh na imamu ni mmoja tu kwa sababu ni wito wake unaweza ukawa umesoma Quran  lakini ukashindwa kupata usheikh, sawa na Wakristo ni wengi lakini padri ni mmoja tu,”amesema.

Katika maelezo yake amesema kazi ya uongozi na siasa ina wito ndani yake na kipimo cha kujitazama kama kweli ni mwanasiasa,  ni mapenzi na namna unavyoweza kushughulika na matatizo ya jamii hata kama huna cheo chochote.

“Kama umekosa mapenzi hayo basi jitazame vizuri. Sasa hivi siasa imekuwa kama fasheni vijana wanaona siasa ni fursa hapa chuo kikuu vijana wanamaliza vyuo wanakuja kwenye vyama hawajawahi kuwa wanachama lakini wanataka kugombea ubunge,” amesema.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema kama kijana ana ndoto ya kuwa kiongozi ikiwemo ubunge inaweza kutimia kama atajiamini.

“Zamani tulikuwa na kasumba watu walikuwa wanaona vijana hawastahili kuwa viongozi,  lakini sasa hivi watu wanapenda viongozi vijana. Kama una ndoto ya kugombea,  kata shauri,” amesema.

Katika nasaha zake kwa vijana Mnyika amewataka vijana kuwa wavumilivu kwa sababu mapito ya kisiasa ni magumu na yamejaa  mambo mengi na ukikata tamaa katikati hawawezi kutimiza ndoto zako.

Mnyika amesema hata kama hawana nguvu kifedha lakini uwezo wao utabainika kwa mfumo wa watu kuwashawishi wawaunge mkono katika kugharamia kampeni ili wawachague kuiongoza jamii.

Naye Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amesema aliweka pembeni nafasi ya utumishi wa umma, ili ajiunge na siasa  kuikomboa jamii  na changamoto alizokuwa anaziona.

“Wakati nazunguka kwenye shughuli zangu za afya,  nilikuwa nazunguka nchi nzima unakuta watu wanakuambia hawana maji na mahitaji mengine. Unajikuta unaacha kazi yako ya msingi na kuanza kufanya kazi nyingine,” amesema.