Serikali yatoa maagizo kwa wakurugenzi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene
Muktasari:
- Serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri 18 zinazotekeleza Mradi wa Timiza Malengo kusimamia afua mbalimbali za mradi huo, lengo likiwa ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wasichana balehe na wanawake wenye umri wa miaka 10 hadi 24.
Dodoma. Serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri 18 zinazotekeleza Mradi wa Timiza Malengo kusimamia afua mbalimbali za mradi huo, lengo likiwa ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wasichana balehe na wanawake wenye umri wa miaka 10 hadi 24.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vishikwambi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kwenye mradi wa timiza malengo.
Ameyataja mambo wanayotakiwa kusimamia kwa ufanisi ni kuanzishwa na kuimarisha klabu za Ukimwi ambazo zitawezesha wanafunzi kujadili na kujifunza mada zilizowekwa katika vishikwambi na kusimamia matumizi sahihi ya zana kwa uendelevu wa mradi kwenye halmashauri husika.
Mengine ni kusimamia na kufuatilia uwajibikaji wa maofisa ugani katika kusimamia maendeleo ya mradi huo kwa walengwa na kuwawezesha kwenye mfumo wa wanawake, vijana na wenye ulemavu (4-4-2).
“Nichukue fursa hii kutoa rai kwa vijana wote nchini hasa walio katika eneo la mradi hususan wasichana ambao wanalengwa na mradi huu mfanye juhudi za kujikinga na maambukizi mapya ya VVU,”amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema anaamini vishikwambi hivyo vitatumika vizuri kuongeza maarifa kwa wanafunzi pamoja na ufaulu.
“Sasa hivi vitabu vyote vinapatikana mtandaoni sasa kupitia vishakwambi hivi naamini vitahusika kuwekwa pia programu za vitabu ili wanafunzi wajifunze kupitia Tehama,”amesema.
Naye, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko amesema lengo la Mradi wa Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana unalengo la kuwasaidia wasichana walio ndani na nje ya shule.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa fikra, maarifa ili wakati wote wabaki salama dhidi ya maambukizi ya VVU na waweze kulijenga Taifa imara.