Serikali yapinga hukumu ya fidia ya Sh260 bilioni

Dar es Salaam. Serikali imewasilisha pendekezo katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), la kufuta hukumu inayoelekeza kulipa fidia ya Dola 109 milioni za Marekani (Sh260 bilioni).
Hukumu hiyo iliyotolewa na ICSID Julai 14, mwaka huu iliitaka Serikali ya Tanzania kulipa fedha hizo kwa Kampuni ya Madini ya Indiana Recources.
Indiana inanufaika na fidia hiyo kutokana na umiliki wa asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili (Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited) zilizokuwa zikimiliki leseni ya kuhodhi ardhi katika eneo la Mradi wa Nikel wa Ntaka Hill, uliokuwa Wilaya ya Nachingwea.
Pingamizi hilo lililobeba hoja zaidi ya 15 linaomba pia zuio la kuanza utekelezaji wa hukumu hiyo, inayoielekeza Serikali kuanza kulipa kuanzia Julai 14 mwaka huu, ikiendana na ongezeko la asilimia mbili kila siku hadi itakapomaliza malipo yote.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Serikali italipa baada ya mwekezaji kudai kupata hasara itokanayo na uamuzi wa kufuta leseni ya kuhodhi ardhi katika eneo hilo la mradi bila kujali gharama alizowekeza.
Msingi wa madai hayo unatokana na ukiukwaji wa Mkataba wa Uwekezaji (BIT) uliyosainiwa kati ya Serikali na UK & Ireland ya Kaskazini mwaka 1994, unaohusisha wanahisa wenza wa Indiana Resources waliomiliki leseni hiyo.
Kwa mujibu wa Indiana, wanahisa waliishawishi Serikali kurejesha leseni yao lakini haikuwezekana, kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 yanayoelekeza kuzifuta.
Jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi alilithibitishia gazeti hili kwa ushahidi wa nyaraka ya ICSID, inayojulisha wahusika wote wa kesi kuhusu ombi la kubatilisha utekelezaji wa hukumu hiyo chini ya kifungu cha 50(2)(a) na (b) cha Mkataba wa ICSID.
“Kwa mujibu wa kanuni ya 52(1) ya usuluhishi, nitamwomba mwenyekiti wa Baraza la Utawala la ICSID kuteua wajumbe wa kamati ya dharura itakayozingatia maombi ya kubatilisha uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 52(3) ya ICSID,” inaeleza taarifa hiyo ya ICSID.
“Ombi hilo pia linahusisha ombi la kuzuia utekelezaji wa adhabu chini ya kifungu cha 52(5) cha Mkataba wa ICSID. Kanuni ya 54(2) ya usuluhishi ya ICSID inatamka katibu mkuu pamoja na taarifa ya kusajiliwa ombi hilo, atajulisha wahusika kuhusu kusimamishwa kwa muda kwa adhabu hiyo. Kwa hivyo, ninakufahamisha kwamba utekelezaji wa tuzo (hukumu) umesitishwa kwa muda.”
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniphace Luhende alisema zuio hilo linahusisha uwezekano wa kutoshikiliwa ndege za Serikali mpaka utaratibu wa pingamizi utakapokamilika.
Alipoulizwa Serikali imeweka pingamizi hilo kwa ujasiri gani, Dk Luhende alisema: “Huwezi kuweka pingamizi bila sababu, tunazo sababu zaidi ya 15, kwa hiyo tumerudi ulingoni, ni mapambano na inatoa relief (ahueni). Sababu ni siri hatuwezi kuweka wazi kama ambavyo haukuona sababu za ushindi wa Indiana.”
Akitoa maoni kuhusu uamuzi huo wa Serikali, Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Nishati na Madini (Numet), Nicomedes Kajungu aliunga mkono uamuzi huo unaoweza kuwa na matumaini ya kushinda kutokana na alichodai mchezo mchafu uliotumika katika leseni za kuhodhi ardhi katika rasilimali iliyogunduliwa bila kuendelezwa.
“Wawekezaji wanashinda kwa haki kutokana na kuchezewa sheria zetu. Serikali iliuona mchezo huo kwa kuchelewa. Mwekezaji anafanya utafiti, anapata data za madini yaliyopo kwenye ardhi kisha anachukua leseni hiyo ya kuhodhi ardhi kwa miaka kumi au zaidi bila kuendelezwa,” alisema Kajungu.
“Kumbe anatafuta mteja kuuza data za eneo hilo kwa thamani kubwa bila Serikali kupata mapato halisi, wakati huo imepoteza mapato mengi bila eneo kuendelezwa uzalishaji. Huo ulikuwa uhuni wa kisheria tu, ilitokea pia eneo la Buhemba na Butiama, tukijenga hoja tutawashinda.”
Hata hivyo, kumekuwa na maoni kutoka kwa baadhi ya watu wakishauri Serikali kuanzisha majadiliano ya kutafuta maridhiano na wawekezaji wenye uhalali wa kunufaika na fidia inayotokana na dosari hizo za Sheria ya Madini ya mwaka 2017, zilizoanza kuathiri Taifa kutokana na madai yaliyopo au ushindi wa kesi zilizoamuliwa.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Asasi za Kiraia zinazochambua Mikataba ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji (Tatic), tangu mwaka 1965 hadi 2019, Serikali imeshasaini mikataba 20 ya BITs, ikiwamo inayoendelea na utekelezaji wake hadi sasa, huku Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikishauri maboresho.
Serikali imeshakiri na kuanza kulipa fidia ya Dola 165 milioni (Sh380 bilioni) kwa Kampuni ya Eco Energy Group iliyoshinda kesi dhidi ya uamuzi wa kupokwa hatimiliki ya hekta 20,400 za mradi wa sukari Bagamoyo, ikiwa ni ukiukwaji wa mkataba wa aina hiyo kati ya Tanzania na Sweden.