Serikali yaombwa kurejesha nchini mafuvu ya kale yaliyopo Ujerumani

Muktasari:
Serikali imeshauriwa kutoa tamko kuhusu kurejeshwa nchini Tanzania kwa vifaa vya utamaduni yakiwemo mafuvu yaliyopo nchini Ujerumani kwa kushirikiana na Balozi za Marekani, Uholanzi na Ufaransa
Moshi. Serikali imeshauriwa kutoa tamko kuhusu kurejeshwa nchini Tanzania kwa vifaa vya utamaduni yakiwemo mafuvu yaliyopo nchini Ujerumani kwa kushirikiana na Balozi za Marekani, Uholanzi na Ufaransa
Pia, imetakiwa kurejesha vifaa hivyo ikiwemo jiwe la asili ya mkoa wa Kilimanjaro linalotakiwa kukombolewa kwa euro 200,000 .
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Machi 5, 2021 na ofisa misitu Mkoa wa Kilimanjaro, Immanuel Kiyengi katika kikao cha kamati ya ushauri Mkoa Kilimanjaro.
Amesema Serikali inatakiwa kutoa tamko kuhusu nia ya kurejeshwa kwa vifaa na mafuvu hayo kama ilivyofanya nchi nyingine ikiwemo Namibia ili kujenga heshima, uzalendo, umoja na kutunza historia.
Amesema Serikali itoe tamko kuhusu masalia ya mafuvu ya binadamu na vifaa mbalimbali vya utamaduni vilivyochukuliwa Moshi na sasa vipo katika jumba la makumbusho huko Berlin, i Ujerumani chini ya taasisi ya Prussin culture heritage.
Amebainisha kuwa vikirejeshwa nchini vitasaidia kuwa chachu ya kutunza historia na kumbukumbu na mwanzo mzuri wa kuanzisha makumbusho mjini Moshi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameshauri kijengwe kituo cha utamaduni katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kia) na eneo la KDC Wilaya ya Moshi.