Serikali yaombwa kupanua wigo elimu ya VVU

Muktasari:
- Watanzania wametakiwa kutumia vipaji na utalaamu wao katika mapambano dhidi ya VVU.
Dar es Salaam. Wakati Desemba Mosi ikiwa ni Siku ya Ukimwi Duniani, Serikali imeombwa kutanua wigo wa elimu kuhusu maambukizi ya Virusi ya Ukimwi (VVU) ili watu wajimbue kwa kuwa wengi wanaoambukizwa ni vijana wenye umri 18 hadi 20.
Ombi hilo lilitolewa na mwasisi wa 4A9 African Trust Clinick, Tr Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Mwasisi huyo ambaye hutoa matibabu mbadala alisema watu anaokutana nao wakitafuta tiba wengi wao ni vijana wenye umri huo, huku akiwaomba Watanzania kujilinda na maambukizi ya VVU akisema, “ukijilinda utamlinda mwenzako.”
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia mwaka 2021 watu wanaoishi na VVU duniani imefikia milioni 38.4 kutoka watu 30.8 mwaka 2010.
“Tatizo linavyoendelea kuwa kubwa tunapunguza nguvu kazi katika Taifa letu, Watanzania wanatakiwa kujitambua na kuwatambua watu wenye maambukizi,” alisema Tr.
Alisema takribani miaka 40 sasa, Taifa bado lipo kwenye mapambano ya maambukizi hayo huku akiwataka vijana kutumia jitihada katika mapambano hayo.
Msigwa aliiomba Serikali kuwashawishi Watanzania kuchukua hatua madhubuti katika maambukizi hayo, huku akisema sera zinapaswa ziangaliwe upya kuhusu tiba ya VVU.
Akitolea mfano alisema Rais mstaafu, Hayati Benjamini Mkapa alitangaza maambukizi ya VVU ni janga la Taifa kwa kuwa alikuwa akiwaandaa Watanzania ili wajue kuna changamoto ya ugonjwa huo na wajue namna ya kupambana.
“Kwa mfano, wakati wa maambukizi ya Uviko-19, vijana wa Iran walitumia vipaji vyao ni namna gani wanaweza kupambana na maambukzi hayo, walimchanja kiongozi wao dhidi ya virusi hivyo,” alisema Tr.
Aliwataka Watanzania kutumia vipaji na utalaamu wao katika mapambano dhidi ya VVU.
Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la mama Faraj alisema inasikitisha kuona vijana wenye umri mdogo wakiambukizwa ugonjwa huo.
Hata hivyo, aliwataka vijana kupima maambukizi hayo na kutumia kinga ili kujilinda kwa kuwa wao ndio Taifa la kesho.