Serikali yakusanya mabilioni biashara ya mtandao

Muktasari:
- Serikali imekiri inaitambua biashara mtandao ambapo kuna maelfu ya mitandao iliyosajiliwa.
Dodoma. Kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, Serikali imekusanya kiasi cha Sh192.78 bilioni kutoka kwenye biashara mtandao ambayo inajumuisha michezo ya kubahatisha ya mtandaoni.
Takwimu hizo zimetolewa leo Jumanne Aprili 29, 2025 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ambaye ameliambia Bunge Serikali inatambua biashara mtandao.
Kigahe alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rita Kabati ambaye ameuliza ikiwa Serikali inatambua biashara ya mtandao ni kampuni ngapi zimejisajili na mapato kiasi gani yamepatikana.
Katika swali la nyongeza, Kabati ameuliza ni njia ipi inatumiwa na Serikali kuzuia udanganyifu unafanywa na utapeli wa mitandaoni, pia ameuliza namna Serikali inavyoweza kuzuia bidhaa feki kupitia kwenye mitandao ya kijamii.
Kigahe amesema hivi sasa kuna kampuni 1,820 zilizosajiliwa, ambapo kampuni 1,075 za biashara mtandao ni shughuli yao kuu na 745 biashara mtandao ni shughuli nyingine.
“Kwa sasa Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu za kuwa na mfumo madhubuti utakaosimamia biashara hiyo ambazo zimeanza kuzaa matunda,” amesema.
Amesema ili kuhakikisha Taifa linakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwenye biashara, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Biashara Mtandao (National Electronic Commerce Strategy) ambao upo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.
Naibu Waziri ametaja maeneo yatakayofanyiwa kazi katika utekelezaji wa mkakati huo ni uboreshaji wa miundombinu ya Tehama, uboreshaji wa sera, sheria na kanuni, uboreshaji wa huduma za mawasiliano, usafirishaji na uchukuzi, uimarishaji wa huduma za miamala kwa njia ya mtandao na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu biashara hiyo ili waitumie kujinufaisha.
Akijibu maswali ya nyongeza kutoka kwa mbunge huyo, Kigahe amesema mbali na changamoto zilizopo, lakini Serikali imekuwa na mkakati wa kukomesha mambo hayo kupitia taasisi zake.