Serikali yakiri ukata kuchelewa barabara Kimara-Kibaha

Muktasari:
- Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2 iliyoanza kujengwa mwaka 2017 ilipangwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya Sh141.5 bilioni, ikiwa na njia sita kabla ya mabadiliko ya kuifanya kuwa na njia nane na gharama kufikia Sh218 bilioni.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2 iliyoanza kujengwa mwaka 2017 ilipangwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya Sh141.5 bilioni, ikiwa na njia sita kabla ya mabadiliko ya kuifanya kuwa na njia nane na gharama kufikia Sh218 bilioni.
Kutokukamilika kwake kumesababisha kero kwa abiria wanaoitumia wakikosa vibanda vya kujihifadhi wakati wa jua na mvua wanaposubiri usafiri vituoni, huku pia barabara hiyo ikikosa taa na kuhatarisha usalama wa watumiaji.
Akizungumza Novemba baada ya kutembelea mradi huo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alisema mradi wa upanuzi wa barabara hiyo mwanzoni haukuzingatia mahitaji ya mabasi yaendayo haraka.
Amesema baada ya kuonekana kuwa kuna uhitaji kwa wananchi wa Kibaha na Hospitali ya Mloganzila walikaa na Wakala wa barabara nchini (Tanroads) kujadiliana ili kuona uwezekano wa kufikisha huduma hiyo katika maeneo hayo.
"Baada ya tathimini tuliyofanya, ilionekana fedha zilizopo haziwezi kutosheleza kujenga barabara ya katikati ya kutumia mabasi yaendayo haraka, pamoja na vituo na mahitaji yake mengine," amesema.
Amesema baada ya kubaini upungufu wa fedha waliendelea kujenga maeneo mengine na kuliacha la katikati na kulishafanyika usanifu wa awali katika maeneo maalum ambayo mabasi yatakuwa yanashusha na kupakia abiria.
"Maeneo mnayoona kuna vituo vidogo wametuachia sehemu za kujenga vituo vya kukatia tiketi za abiria na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inafanya mazungumzo na wizara ya fedha kupata fedha ya kujenga barabara ya katikati na mahitaji yake," amesema.
Amesema wakati wakisubiri fedha ili kuwapunguzia kero abiria wa eneo maeneo hayo wanatarajia kujenga vituo vidogo 21 na tayari wamekamilisha usanifu wa vituo 11 wakiwa wanasubiri ujenzi wa barabara kubwa.
Waziri wa Ujenzi na Viwanda, Innocent Bashungwa amesema, mradi huo umekamilika kwa asilimia 99 tangu Juni 16, mwaka huu, na sasa kilichobakia ni vitu vidogo ikiwemo taa za kuongozea magari kwenye makutano ya barabara.
"Kulikuwa na sehemu za makutano ya barabara tisa, tayari tano zimeweka taa zimebaki nne, tulishaagiza na Miata sasa tunasubiri taratibu za kuzifunga," alisema.
Pia alisema wanatarajia kuweka taa za barabarani 450 kwa mfumo wa kutazamana iliziangaze maeneo yote na kuwarahisishia watembea kwa miguu na wenye usafiri hususan nyakati za usiku.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema barabara hiyo kwa mabasi yaendayo haraka hadi magomeni inahitaji mabasi 177 na kuna njia nyingine zinazongezwa zinahitaji mabasi 775.
Katika ziara hiyo alikuwepo pia Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Fanuel Kalugedo.