Prime
Mateso barabara ya Kimara-Kibaha

Dar es Salaam. Shauku ya wananchi watumiao barabara ya Morogoro kuona ujenzi kipande cha Kimara Mwisho hadi Kibaha mkoani Pwani unakamilika inazidi kufifia kadri siku zinavyosonga mbele kutokana na kuendelea kuchomwa jua na kunyeshewa mvua wanaposubiri usafiri vituoni.
Barabara hiyo pia haina taa, hali inayotishia usalama wa watumiaji na kuleta usumbufu, hasa usiku.
Eneo la katikati ambalo limeandaliwa kwa ajili ya magari yaendayo haraka na ujenzi haujakamilika likiendelea kufungwa kwa kuwekwa mawe kuzuia vyombo vya moto visipite sasa limegeuzwa sehemu ya mazoezi.
Baadhi ya vikundi vya mazoezi ya viungo na mtu mmoja mmoja wamekuwa wakilitumia eneo hilo kufanya mazoezi ya kukimbia.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 19.2 ilianza kujengwa mwaka 2017 na ilitarajiwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya Sh141.5 bilioni, ikiwa na njia sita kabla ya mabadiliko ya kuifanya kuwa na njia nane na gharama kufikia Sh218 bilioni.
Majibu ya mkandarasi
Meneja kutoka kampuni ya Estim inayojenga barabara hiyo, Mhandisi Freddy Nyenga, alisema kila walichotakiwa kufanya katika mradi huo kimekamilika isipokuwa ufungaji wa taa.
“Barabara ya katikati si sehemu ya mkataba wetu, lakini inatakiwa kujengwa. Hadi tumemaliza kujenga hatujapewa kazi, pengine tunaweza kupewa kwa kuwa tupo kwenye uangalizi wa mwaka mmoja wa mradi huo hadi Julai mwakani,” alisema.
Nyenga alisema kilichosababisha taa kutofungwa kwa wakati ni kwamba, sokoni hakuna taa zenye uwezo wa kufungwa kwenye barabara ya njia nane.
Alisema zilizopo zinafaa njia mbili, hivyo wameagiza taa maalumu kiwandani kwa ajili ya mradi huo.
“Kilichojitokeza taa zilikuwa zije lakini zilizotakiwa kuja mwanga wake usingeweza kuangaza sehemu yote. Hizi zinazoonekana humu ni za njia mbili tu, ukitaka za njia nane ni maalumu za umeme. Taa za umemejua zina changamoto yake, lazima ziwe kubwa sehemu ya kuchukua mwanga wa jua na betri zake,” alisema.
Alisema walishaleta taa za mfano lakini zilionekana kuwa ndogo, hivyo zinahitajika kubwa zaidi.
Nyenga alisema wameshatoa oda maalumu kiwandani kwa ajili ya taa za njia nane na kwamba, wapo kwenye mchakato wa mwisho wa hatua za manunuzi.
Akizungumzia vituo, alisema walishakamilisha ujenzi, ukiwamo wa Mloganzila na Kibwegere. Pia kituo cha kuegesha malori kilichopo Mbezi Kibanda cha Mkaa.
Novemba 3, mwaka huu, Mwananchi lilizungumza na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa juu ya maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo alisema kila jambo linakwenda kwa utaratibu wake na kama lilivyopangwa.
Kauli ya Tanroads
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta alipoulizwa kuhusu mradi huo alisema haujakwama, akimtaka mwandishi amtafute ofisa habari wa taasisi hiyo kwa ajili ya ufafanuzi.
Hata hivyo, ofisa habari wa Tanroads makao makuu, Aisha Malima, alipoulizwa alisema hayuko tayari kulizungumzia
Naye Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Herson Edward, hakuwa tayari kuzungumzia ujenzi huo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa katika ofisi hiyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema hatima ya mradi huo haijulikani kwa kuwa hakuna fedha.
“Hatuna fedha ya kukamilisha shughuli ndogondogo tulizosema na tumekuwa tukiiomba Serikali watusaidie kumalizia ujenzi kufikia asilimia 100,” alisema.
Alisema hadi ujenzi uliposimama ulikuwa umefikia asilimia 94, kazi zilizosalia zikiwa kujenga barabara ya katikati, kuweka taa na kujenga vituo vya abiria.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, makosa yalifanyika mwanzoni kwa kuongeza mkataba kuwa njia nane kwa bajeti iliyopangwa awali ya njia sita.
Alisema bajeti iliyokuwapo imeishia njiani, hivyo wanaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
Machi 22, mwaka huu, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kufanya ziara katika mradi huo, aliyekuwa mtendaji wa Tanroads, Rogatus Mativila, alinukuliwa na Mwananchi akisema ujenzi ulitarajiwa kukamilika Aprili 15, 2023.
“Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 94, baada ya kuongezeka kwa shughuli ndogondogo ikiwamo ujenzi wa maegesho ya malori ya mizigo, kuweka taa, ujenzi wa barabara ya katikati,” alisema na kuongeza:
“Wakati ujenzi ukiendelea tuliona mahitaji, tukaona tuboreshe ili barabara iwe na tija zaidi na kuondoa kabisa msongamano. Ilipendekezwa kuwekwe na daraja la juu eneo la Mbezi Mwisho.”
Mativila alisema, “Eneo lingine ni ujenzi wa barabara ya maingilio kwenye stendi kuu ya Magufuli, stendi eneo la Kibamba na taa 460 za barabara ambazo ziko kwenye mchakato.”
Ujenzi ulipozinduliwa
Barabara hiyo iliyoanza kupanuliwa mwaka 2017 iliacha machungu na vilio kwa wakazi waliokuwa wakiishi kando mwa barabara kuanzia Kimara Stop-over jijini Dar es Salaam hadi Kiluvya mkoani Pwani, baada ya nyumba kubomolewa kupisha ujenzi pasipo kulipwa fidia.
Siku ya uzinduzi wa barabara hiyo, Desemba 19, 2018, Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, alisema ujenzi huo ulitakiwa kufadhiliwa na mataifa ya nje, lakini Serikali ilijitosa baada ya kuona unachelewa kukamilika.