Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magufuli akumbuka barabara 10

Dk Magufuli alisema Serikali imetenga Sh605 milioni kukamilisha kazi zilizobakia kwa Barabara ya Kawawa - Msimbazi na makutano ya Jangwani na Twiga.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Dk Magufuli alisema Serikali imetenga Sh605 milioni kukamilisha kazi zilizobakia kwa Barabara ya Kawawa - Msimbazi na makutano ya Jangwani na Twiga.

Dodoma. Wizara ya Ujenzi imetenga Sh28.94 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kujenga, kufanya upanuzi na kukarabati barabara 10 za mchepuko katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa magari.

Akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2014/2015 bungeni Dodoma juzi jioni, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema mradi huo utahusisha barabara zenye urefu wa kilometa 109.35.

Barabara zitakazohusika katika mradi huo ni Kawawa kwenda Bonde la Msimbazi hadi makutano ya Jangwani na Twiga ambayo itakuwa na urefu wa kilometa 2.7.

Nyingine ni Jet Corner kwenda Vituka hadi Devis, kilometa 10.3, sehemu ya Tabata Dampo kilometa 2.25 na Kimara –Kilungule – External, kilometa tisa.

Barabara nyingine ni Mbezi - Marambamawili – Kinyerezi –Banana, kilometa 14, Tegeta – Kibaoni - Wazo Hill - Goba hadi Mbezi, Barabara ya Morogoro ambayo itakuwa na urefu wa kilometa 20.

Nyingine ni Tangi Bovu - Goba kilometa tisa, Kimara – Baruti - Msewe, Kibamba - Kisopwa, Banana - Kitunda-Kivule – Msongola, kilometa 14.7.

Mradi huo unahusisha pia barabara nyingine ya Ardhi - Makongo yenye urefu wa kilometa 4 na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka na vituo vyake unaoendelea

Fedha zilizotengwa

Dk Magufuli alisema Serikali imetenga Sh605 milioni kukamilisha kazi zilizobakia kwa Barabara ya Kawawa - Msimbazi na makutano ya Jangwani na Twiga.

Pia alisema Sh1.29 bilioni zimetengwa kulipa sehemu ya madai kwa ajili ya mkandarasi anayejenga Barabara ya Jet Corner - Vituka hadi Devis Corner.

Pia Waziri huyo alisema Serikali imetenga Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Barabara ya Ubungo – Maziwa - External na Tabata Dampo - Kigogo.

Mbali na bajeti hiyo, alisema Serikali pia imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Barabara ya Kimara – Kilungule - External na Sh6 bilioni kwa ajili ya Mbezi – Marambamawili - Kinyerezi hadi Banana.

Katika mgawo huo, alisema Serikali imetenga Sh3 bilioni kwa ajili ya Barabara ya Tangi Bovu - Goba, Sh1.5 bilioni kwa Barabara ya Kimara Baruti - Msewe hadi Changanyikeni.

Serikali pia imetenga Sh1.5 bilioni kwa Barabara ya Kibamba - Kisopwa, Sh1 bilioni kwa Barabara ya Banana – Kitunda - Kivule-Msongola na Sh1.5 bilioni za Barabara ya Ardhi - Makongo.

Katika mwaka huo wa fedha, Sh4.95 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na kazi ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni na Sh2.5 bilioni kuanza ujenzi wa Barabara ya maingilio ya Mjimwema - Vijibweni.

Serikali pia imetenga Sh150 milioni kwa ajili ya kupanua Barabara ya Nyerere sehemu wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) - Pugu kuwa njia sita.

Waziri Magufuli alisema mradi huo upo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na utagharimiwa na fedha kutoka vyanzo vya ndani.

Alisema pia katika mwaka huo wa fedha, Serikali itaanza kufanya usanifu wa upanuzi wa Barabara ya Kimara - Kibaha na usanifu huo umetengewa Sh250 milioni.

Kadhalika, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa Barabara ya Pugu – Kifuru - Mbezi Mwisho - Mpiji Magoe - Bunju yenye urefu wa kilometa 34 ambao umetengewa Sh1 bilioni.

Katika bajeti hiyo, Serikali pia imetenga Sh8 bilioni kukarabati na kupanua barabara ya lami sehemu ya Gerezani Kamata - Bendera Tatu kutoka njia mbili za sasa hadi njia nne.

Barabara ya juu Tazara

Waziri Magufuli alisema Septemba mwaka huu Serikali ilitangaza kuanza ujenzi wa barabara ya juu (flyover) katika eneo la Tazara ambao umetengewa Sh16 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 ili kupunguza msongamano.

Kati ya Sh16 bilioni zitakazotumika katika mradi huo, Sh1 bilioni zitakuwa ni fedha za ndani wakati Sh15 bilioni zitatoka kwa wahisani.

Wizara hiyo iliomba kuidhinishwa Sh1.2 trilioni kwa ajili ya matumizi ya ndani na miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara.