Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaendelea na uchunguzi kesi ya vigogo TPA

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (wapili kutoka kushoto) akiwa na wenzake wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Muktasari:

  • Kipande na wenzake hao wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia TPA hasara ya Dola za Marekani 1.85milioni sawa na Sh4.2 bilioni, baada ya kutangaza zabuni bila kuwa na kibali cha bodi.

Dar es Salaam. Serikali imesema bado wanaendelea na upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande (66) na wenzake watano.

Hayo yameelezwa leo Januari 9, 2023 na Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Makamama ya Kisutu, Ramadhani Rugemalira.

Kipande na wenzake hao wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Dola za Marekani 1.85milioni sawa na Sh4.2 bilioni.

Kutokana na maelezo hayo, hakimu Rugemalira ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 7, 2023 itakapotajwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Mbali na Kipande, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 39/2022 ni Peter Gawile (58) aliyekuwa Ofisa Rasilimali Watu wa TPA na mkazi wa Mianzini; Casmily Lujegi (65) mkazi wa Mbezi Juu na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa TPA.

Wengine ni Mashaka Kisanta (59) Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na Kilian Chale (51) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na mkazi wa Mbezi Makabe pamoja na Andrew John.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi 2020 Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kuisababishia TPA hasara.

Shitaka la pili, kati ya Januari Mosi, 2015 hadi Februari 17, 2015 washitakiwa kwa pamoja wakiwa Maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia dola za Marekani zaidi ya 1.85 milioni.

Shitaka la tatu, inadaiwa kati ya Oktoba Mosi 2014 na Oktoba Mosi, 2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP) bila kupata kibali cha bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo.

Pia walishindwa kufuata kanuni za zabuni hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA hasara ya zaidi ya dola 1.8 milioni ambazo ni sawa na zaidi ya Sh4.2 bilioni.