Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali, wadau wahimizwa kujenga vyoo bora kwenye vituo vya afya

Muktasari:

  • Katika kuadhimisha siku ya choo duniani inayoadhimishwa kila Novemba 19 kila mwaka, Shirika la WaterAid Tanzania limetoa msaada wa vifaa vya kusafishia vyoo katika vituo vya afya katika manispaa ya Temeke.

Dar es Salaam. Serikali na wadau wa maendeleo nchini wamehimizwa kuelekeza rasilimali kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya kwa kujenga vyoo bora vinavyotosheleza mahitaji kwenye eneo husika

 Wito huo umetolewa jana Novemba 26, 2023 Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Sera, Uraghabishi na Ushawishi kutoka WaterAid Tanzania, Christina Mhando wakati akikabidhi vifaa vya usafi wa vyoo kwenye halmashauri ya manispaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vyoo.

Vituo vya afya vitakavyonufaika na msaada huo ni pamoja na kituo cha afya cha Mkondogwa kilichopo Chamazi na kituo cha afya cha Goroka kilichopo Mbagala na vifaa vilivyotolewa ni mafagio, sabuni za kusafishia, glovu, ndoo na vyombo vya kuhifadhia takataka.

Akizungumza wakati akitoa msaada huo, jana, Mhando alisema changamoto zilizobainika ni ubora wa vyoo au kutokuwa na matundu ya kutosha kwenye vituo vya huduma za afya au vyoo kuwa mbali na sehemu ambazo huduma za mama na mtoto zinatolewa

“Tunaendelea kuiomba Serikali na wadau mbalimbali waelekeze rasilimali kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kila kituo cha kutolea huduma hiyo kiwe na vyoo bora na vyenye kukidhi mahitaji ya wateja na wahudumu wa afya katika vituo hivyo,” alisema.

Mhando alieleza kwamba katika kutekeleza hilo, vitu vitatu haviwezi kutenganishwa ambavyo ni maji, usafi binafsi na vyoo bora. Alisema vyoo vinavyohudumia watu wengi vinahitaji uangalizi wa karibu na kuhakikisha vina maji na safi wakati wote.

Mkuu huyo wa idara, aliipongeza Serikali kwa hatua iliyopigwa kwani takwimu za utafiti wa afya na idadi ya watu nchini (TDHS) ya mwaka 2022 inaonyesha kwamba kuna ongezeko la vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 75 mwaka 2022.

“Hiyo ni hatua kubwa ambayo Tanzania imefikia, lakini bado Watanzania wanahitaji kuendelea kuhamasishwa na pia kuhamasishwa kuendeleza tabia hiyo ya matumizi ya vyoo bora. Tunaamini kila mahali huduma hizo zipo zinaendelea na ni muhimu,” alisema.

Alisisitiza kwamba inawezekana kufanya suala la vyoo bora kuwa la kawaida kwa kila mtu kwa kuwa kuna watu hasa maeneo ya pembezoni ambao wanaona suala la vyoo bora siyo la kawaida kwao wakiwa sehemu zao za kazi, majumbani, shuleni au masokoni.

Kwa upande wake, kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Temeke (DMO), Timothy Bende alishukuru kupokea vifaa hivyo na kueleza kwamba vitepelekwa kwenye vituo vya afya vipya vya Goroka na Mkondogwa.

Alisema vituo hivyo ni vipya na vimeanza kutoa huduma mwaka huu na alieleza sababu ya kuchagua vituo hivyo kuwa ni kutokana na idadi kubwa ya watu mathalani kituo cha Mkondogwa kinachohudumia watu zaidi ya 200,000.

“Tunawashukuru kwa msaada huu mkubwa wa kuhakikisha kwamba huduma na usafi kwenye vituo vyetu hivi unakwenda kuimarika zaidi. Bado tuna uhitaji kwenye vituo vyetu vingine, tunakaribisha wadau wengine kujitokeza kusaidia,” alisema.